Tuesday, December 27, 2016

Viwanda zaidi kujengwa Rungwe mwakani

 

By Amanyisye Ambindwile, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Rungwe. Ile kaulimbiu ya ‘Tanzania ya Viwanda’ huenda ikapata nguvu zaidi baada ya wadau wa maendeleo wilayani Rungwe kuazimia kuongeza viwanda zaidi.

 Wadau hao wamekubaliana kujenga viwanda vidogo kutoka saba vya sasa hadi 70 kuanzia mwakani.

 Makubaliano hayo yamefikiwa kwenye kongamano lililotathmini maendeleo wilayani humo likiwa na mada: ‘Tulikotoka, tulipo na tunakokwenda’ na kuwashirikisha wataalamu na wajasiriamali wa ndani na nje ya wilaya.

 Mwalimu wa Chuo cha Biashara na Ujasiriamali, Exaut Mwakihaba amesema wilaya hiyo ina rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa vyema zitawaongezea wananchi kipato.

 Mwakihaba amesema malighafi zinazozalishwa zinatosheleza mahitaji ya kuanzishwa viwanda vidogo 70 hadi 700 kwa kadri uzalishaji unavyokua.

 Mjasiriamali kutoka mjini Tukuyu, Yunis Samu amesema wakazi wa Rungwe wanazalisha maziwa, ndizi, mboga na miti ambayo ni mazao yanayoweza kutumika viwandani kama malighafi ya kuzalisha bidhaa nyingine hivyo ameiomba Serikali iwasaidie kwa kuwapa utaalamu na mitaji.

 Ofisa Tawala wa Wilaya, Eliud Mwandemele amewataka wadau hao kujua idadi ya wakazi, shughuli za uzalishaji na kipato cha mtu mmoja mmoja kwa mwaka.

-->