TBL yataka marejeo kesi ya Sh50 milioni

Muktasari:

TBL inadai kuwa kuna makosa ya dhahiri katika kumbukumbu za uamuzi huo ambayo yamesababisha haki kutokutendeka. Kiwango hicho cha fidia ya zaidi ya Sh50 milioni ni pamoja na riba tangu hukumu ilipotoka.

 

Dar es Salaam. Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), imeiomba Mahakama ya Rufani ifanye marejeo ya hukumu inayoitaka kuwalipa fidia ya zaidi ya Sh50 milioni wafanyakazi wawili walioachishwa kazi miaka 24 iliyopita.

TBL imefungua maombi hayo kujinusuru na utekelezaji wa hukumu iliyotokana na kesi ya kashfa dhidi ya mkurugenzi mkuu wake wa zamani, Arnold Kilewo iliyofunguliwa Mahakama Kuu na walalamikaji hao waliofukuzwa kazi mwaka 1992.

Maombi hayo yamefunguliwa kupitia kwa Wakili Rosan Mbwambo, akiiomba mahakama hiyo ifanye marejeo na hatimaye kubadilisha au kurekebisha uamuzi wake au kutoa amri nyinginezo kadri itakavyoona inafaa.

TBL inadai kuwa kuna makosa ya dhahiri katika kumbukumbu za uamuzi huo ambayo yamesababisha haki kutokutendeka. Kiwango hicho cha fidia ya zaidi ya Sh50 milioni ni pamoja na riba tangu hukumu ilipotoka.

Kwa mujibu wa maombi hayo, uamuzi wa mahakama haukuzingatia ukweli kwamba wajibu maombi hawakumuita shahidi kuthibitisha kuwa Kilewo alichapisha maneno waliyodai ni kashfa dhidi yao, kama inavyotakiwa na sheria za ushahidi na kashfa.

 Hivyo, maombi hayo yanaeleza kuwa wakati mahakama ikijihakikishia kuhusu tafsiri ya kashfa, haikutoa maelezo kuwa viwango vilivyowekwa katika tafsiri ya kashfa vilifikiwa.

 Maombi hayo ya marejeo yanayotokana na hukumu ya Mahakama ya Rufani katika rufaa iliyokatwa na mkurugenzi huyo mahakamani hapo, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu, iliyomwamuru kuwalipa fidia ya Sh20 milioni wadai katika kesi ya msingi.

 Wadai hao katika kesi hiyo ya msingi namba 28 ya mwaka 1995, walikuwa ni wafanyakazi wa kampuni hiyo Boniface Kakiziba na mwenzake John Assenga.

Katika kesi hiyo ya msingi walikuwa wakiiomba Mahakama Kuu imwamuru aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TBL wakati huo, Kilewo, awalipe fidia hiyo kama fidia ya madhara ya jumla kutokana na maneno ya kashfa aliyotoa kwenye vyombo vya habari.

Walikuwa wakidai kuwa Kilewo alitoa taarifa zilizochapishwa kwenye magazeti ya Daily News na Uhuru, akieleza kuwa wafanyakazi hao wameachishwa kazi kutoka na kuuza matairi matano ya kampuni hiyo wakidai kuwa ni mabovu na kutumia fedha hizo kwa masilahi yao.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Augustine Shangwa Januari 4, 2010, ilimwamuru Kilewo kuwalipa Kakiziba na Assenga fidia ya Sh20 milioni kila mmoja, baada ya kuridhika kuwa alitoa taarifa za kuwakashifu kwenye magazeti hayo.