Wizara ya Kilimo yazungumzia mbegu za mafuta

Muktasari:

Malema amesema kwa sasa wizara imekuwa na programu maalumu inayoshughulikia kusaidia uwekezaji wa mazao ya mafuta ya kula yakiwamo ya alizeti, kunde na pamba kwa kushirikiaana na Uganda, Kenya na Ethiopia.

Morogoro. Mkurugenzi msaidizi uendelezaji mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Beatus Malema amesema juhudi za uzalishaji wa mbegu za mafuta zinatakiwa kuongezeka.

Malema amesema hayo mjini Morogoro wakati wa mkutano na Chama cha Wanaojihusisha na Mbegu za Mafuta ya Kula Tanzania (Teosa) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV).

Amesema wakulima wamekuwa wakilima kwa kiwango cha chini kwa sababu hawatumii kanuni bora za kilimo.

 Malema amesema kwa sasa wizara imekuwa na programu maalumu inayoshughulikia kusaidia uwekezaji wa mazao ya mafuta ya kula yakiwamo ya alizeti, kunde na pamba kwa kushirikiaana na Uganda, Kenya na Ethiopia.

 Pia, amesema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa kampuni zitakazoleta mbegu feki za mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

 Mkulima ambaye pia ni mkurugenzi wa Kampuni ya Uzalishaji Mbegu za Alizeti, Stephen Henry amesema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakichangia mazao hayo kudumaa na kukosekana kwa uzalishaji mwingi.

 Amesema wakulima wanatakiwa kulima kilimo cha mkataba kitakachowawezesha kuongeza uchumi wao kulingana na ukulima, huku wakishirikiana na wenye kampuni za uchakataji mafuta.

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi