Polepole : Maoni ya Katiba Mpya yafanyiwa majaribio

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole

Muktasari:

Akizungumza katika kipindi cha Mada Moto kinachorushwa na televisheni ya Channel Ten, Polepole amesema mchakato wa kupata Katiba Mpya ni mgumu kuuendeleza kwa sasa hadi hapo Rais John Magufuli atakapoinyoosha nchi.

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema Serikali ya chama hicho inayatekeleza maoni yaliyotolewa na wananchi wakati wa mchakato wa Katiba Mpya kwa kuyafanyia majaribio.

Akizungumza katika kipindi cha Mada Moto kinachorushwa na televisheni ya Channel Ten, Polepole amesema mchakato wa kupata Katiba Mpya ni mgumu kuuendeleza kwa sasa hadi hapo Rais John Magufuli atakapoinyoosha nchi.

Mchakato wa Katiba Mpya ulizinduliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2011 alipounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na Polepole akiwa mmoja wa wajumbe.

Hata hivyo, mchakato huo uliishia kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambalo licha ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ambayo haijapigiwa kura ya maoni hadi leo, baadhi ya vyama vya upinzani vilijitoa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).