Thursday, January 5, 2017

Waziri Mkuu aagiza mahindi yatunzwe kuepuka baa la njaaWaziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Songea. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea na kuagiza akiba ya mahindi iliyopo iendelee kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa NFRA Kanda ya Songea pamoja na viongozi na watendaji wa Mkoa wa Ruvuma mara baada ya kukagua akiba ya nafaka iliyomo kwenye maghala ya kituo hicho.

Waziri Mkuu alisema mabadiliko ya tabia nchi yamefanya mvua zichelewe kunyesha katika mikoa mingi nchini ukiwemo Ruvuma ambao kwa kawaida mwezi Januari mvua ya kutosha inakuwa imeshanyesha na huwa kuna baridi nyingi.

“Angalieni ninyi wenyewe hali ya joto iliyopo hivi sasa, kwa kawaida mvua ingeshaanza kunyesha mwezi huu na mahindi yangekuwa yameanza kurefuka. Lakini hadi leo (jana) naambiwa mvua imenyesha mara mbili tu na mahindi yaliyopandwa yameanza kunyauka,”

 “Kama mvua haijanyesha hadi leo, ni lazima tuchukue tahadhari, na hata mvua ikija hatujui itaendelea kunyesha hadi lini na kwa kiasi gani. RC, Ma-DC na ma-DED toeni elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula. Waambieni waachane na ngoma za unyago na sherehe za kipaimara ambazo hutumia kiasi kikubwa cha chakula,” alisisitiza.

“Msiruhusu kutoa mahindi yaliyopo na kuyauza. Hizo tani 10,500 zilizopo ziendelee kuhifadhiwa hadi tutakapoamua vinginevyo,” alisisitiza.

-->