Serikali yatakiwa kujipanga kwa uwekezaji wa viwanda 200

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF,Godfrey Simbeye

Muktasari:

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema viwanda hivyo ni fursa muhimu kwa ajira na ukuaji wa uchumi nchini, hivyo kuitaka Serikali kuitumia vyema.

 Dar es Salaam. Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) umeitaka Serikali kuhakikisha inajipanga kwa uwekezaji wa viwanda zaidi ya 200 unaotarajiwa kufanywa na Serikali ya China nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema viwanda hivyo ni fursa muhimu kwa ajira na ukuaji wa uchumi nchini, hivyo kuitaka Serikali kuitumia vyema.

Jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi aliwasili nchini na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Simbeye alisema China ni nchi inayoongoza kwa kuwa na mitaji mikubwa kuliko nchi nyingine duniani, hivyo nchi haina budi kuhimiza mahusiano zaidi ili kuneemeka wakati huu wa Tanzania ya viwanda.