Mgogoro wa mpaka K’njaro, Arusha wawekwa kiporo

Mkuu wa  Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo

Muktasari:

Kikao cha kwanza kuhusu mgogoro huo wa mpaka kati ya mikoa hiyo kilifanyika mkoani Kilimanjaro Desemba 30 mwaka jana kwa maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa ziara yake mkoani Arusha.

Arusha.  Mkuu wa   mikoa wa  Arusha, Mrisho Gambo na Said Meck Sadick wa Kilimanjaro wamekualiana kutafuta msuluhishi kutoka ngazi ya Taifa ili kumaliza mgogoro wa mpaka kati ya mikoa hiyo.

Kikao cha kwanza kuhusu mgogoro huo wa mpaka kati ya mikoa hiyo kilifanyika mkoani Kilimanjaro Desemba 30 mwaka jana kwa maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa ziara yake mkoani Arusha.

Gambo amesema mkoa wake umekusudia kumaliza migogoro yote ya ndani na ile inayohusisha mkoa huo na ya jirani ambayo ni Kilimanjaro, Mara na Manyara.

“Tumefikia hatua nzuri katika kutatua mgogoro huu, lakini tumekumbana na changamoto kubwa ya kutokupatikana kwa nyaraka mbili zilizotangaza mikoa hii miwili,” amesema.

Amesema nyaraka hizo ni tangazo la Serikali namba 450 lililoanzisha mkoa wa Kilimanjaro na jingine namba 456 lililoanzisha mkoa wa Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadick amesema mipaka hiyo ya kiutawala ipo kwa lengo nzuri na wao kama viongozi hawawezi kuvumilia migogoro hiyo iendelee kwa kuwa inakwamisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

“Tunaamini hao wapatanishi watatusaidia kupitia hayo matangazo ya Serikali yaliyoanzisha mikoa yetu yataainisha mkoa wa Kilimanjaro unaishia wapi na Arusha inapoishia,” amesema Sadick.

Mgogoro huo unahusu mipaka katika wilaya za Arumeru (Arusha) iliyoanzishwa mwaka 1980 na Siha (Kilimanjaro) iliyoanzishwa mwaka 2005.