Thursday, January 12, 2017

Hukumu ya mama kumuita mtoto mchawi Februari

 

By Brandy Nelson,Mwananchi bnelson@mwananchi.co.tz

Mbeya. Mahakama ya Wilaya ya Mbeya inatarajia kutoa hukumu Februari 6 ya kesi inayomkabili mwanamuziki wa nyimbo za injili mkoani Mbeya, Aman Mwasote (39) ya kumwita mchawi mtoto wa kike wa miaka tisa.

Hukumu hiyo itatolewa baada ya pande zote mbili kumaliza kutoa ushahidi wake.

Mwasote  ambaye  ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza  wa masomo ya uchungaji katika Chuo cha Biblia cha Southern (SBC) anadaiwa kutenda kosa hilo  Septemba 20 mwaka jana  saa tisa alasiri katika Viwanja  vya Shule ya Msingi Kalobe akiwa kwenye mkutano wa injili.

Mshtakiwa huyo akiwa ameambatana  na  mashahidi wake wawili,  Januari 10, mwaka huu alitoa ushahidi wake  akiongozwa na wakili wake, Sambwee Shitambala.

Akijitetea mahakamani hapo, Mwasote  alidai Mungu alimuonyesha kuna mtoto ana pepo wa uchawi na kuwaomba wachungaji wenzake waungane kumuombea.

Alidai wakati akimuombea mtoto huyo hakumtaja kuwa ni mchawi. 

Akiongozwa na Wakili Shitambala, shahidi Salustian Mkangala alidai anajisikia amani kwa sababu Mungu amenena katika maandiko yake kuwa watafikishwa mbele ya mabaraza kwa ajili ya kazi yake.

-->