Wednesday, February 15, 2017

Wizara yapokea mrejesho wa mradi wa afya ya uzazi wa Thamini Uhai

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu (katikati) na Dr Hussein Kidanto - Kaimu Mkurugenzi wa idara ya huduma za kinga Wizara ya Afya (kushoto) wakishauriana  na Mkurugenzi mtendaji wa Thamini Uhai, Dr Nguke Mwakatundu (Kulia) wakati wa mkutano wa mrejesho wa shirika la Thamini Uhai, leo jijini Dar-es-Salaam 

Dar es Salaam. Wizara ya afya imepokea mrejesho wa mradi wa afya ya uzazi uliofanywa na Thamini Uhai na kufanikiwa kuboresha mahudhurio ya wanawake katika vituo vya afya, kuongeza ujuzi wa uzalishaji kwa wahudumu na kuboresha huduma za uzazi wa dharura na watoto wachanga.

Jumla ya vituo 15 vya afya na hospitali 5 zimejengwa katika maeneo ya vijijini na kukarabatiwa huku zahanati 18 zikinufaika na huduma ya maji katika mradi huo.

Akizunguma wakati wa kukabidhi mrejesho huo Mkurugenzi Mtendaji wa Thamini Uhai, Dk Nguke Mwakatundu amesema Moja ya mafanikio  muhimu katika shughuli zao ni jinsi walivyoweza kuleta mabadiliko katika maisha ya wagonjwa katika nyaja zinazowahusu.

“Tumeona vifo vya uzazi na rufaa zikipungua kwa kiasi kikubwa na katika maeneo haya, pamoja na kuona ongezeko la wanawake wanaoamua kujifungua katika vituo vya huduma za afya”, amesema Dk Mwakatundu

Amesema Matumizi ya kituo cha afya kwa ajili ya uzalishaji yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka wanawake 21,661 waliojifungua mwaka 2011, hadi wanawake 26,189 waliojifungua mwaka 2015.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Ummy Mwalimu amesema Thamini Uhai imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha kina mama wanajifungua kwa usalama katika mikoa iliyofikiwa.

“Naelewa kuwa mmefanya kazi kubwa hususani katika kuboresha mifumo ya huduma za dharura katika vituo vya afya na hospitali iliyoenda sambamba na  kampeni za kuimarisha mawasiliano ya mifumo ya rufaa kutoka vituo vya afya kwenda hospitali”, amesema Ummy

 

-->