Majaliwa akerwa na wingi wa mabango kwenye mikutano ya viongozi wakuu

Mwananchi wa kijiji cha Landanai wilayani Simanjiro  akiwasilisha kero yake kwa njia ya bango akidai mawasiliano ya simu za mkononi wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  aliposimama na kuwasalimia wananchi wa kijiji hicho waliokusanyika  barabarani. Alikuwa akitoka  Orkesimet kwenda  Mererani Februari 16, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mirerani.Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wingi wa mabango katika mikutano ya hadhara  ya viongozi wakuu ni ishara ya wazi kuwa  watendaji wa  halmashauri  hawawatembelei  wananchi na kutatua kero zao.

Akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa mikutano wa Mererani mkoani Manyara jana jioni, Majaliwa alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro na watendaji wake kukusanya mabango  yaliyokuwa yakionyeshwa na wananchi kwani mengi ya matatizo yanapaswa kumalizwa na viongozi hao  na aliwaagiza  kurejea Mererani siku inayofuata ili waitishe mkutano na  kujibu bango moja baada ya jingine.