China, Tanzania zatofautiana ujenzi Bandari ya Bagamoyo

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani

Dar es Salaam.  Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing amesema tofauti kati ya Serikali ya Tanzania na ubalozi wa China umesababisha kukwama kwa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Mchakato wa ujenzi wa bandari hiyo ulianza kipindi cha Awamu ya Nne ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete na ulitarajiwa kuhusisha Serikali za Tanzania, China na Oman.

Akizungumza katika mahojiano na baadhi ya waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alisema, “Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na ukanda wa viwanda wilayani humo ni uwekezaji mkubwa kati ya China na Tanzania katika miaka ya karibuni na umeorodheshwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21).

“Kutokana na umuhimu wake unaohusisha Serikali za Tanzania, China na Oman, ushirikiano kati ya maofisa kutoka idara za Serikali ya Tanzania na ubalozi wa China wanazishauri pande zinazohusika kukunjua moyo na kumaliza tofauti  ili uweze kuendelea kukiwa na makubaliano kwenye mambo ya msingi,” alisema Lu.

Hata hivyo, kwa sasa jitihada zinafanywa ili ikiwezekana makubaliano hayo katika nusu ya mwaka huu na ujenzi uanze ndani ya mwaka huu.

Akizungumzia hilo kwa njia ya simu jana, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alikiri kutofatiana na Wachina katika ujenzi huo.

“Unajua vitu vingine mnapenda kuvikuza bila sababu. Sisi tuliiruhusu Serikali ya China kujenga Bandari ya Bagamoyo kwa kitu kinachoitwa PPP na ule ujenzi ulikuwa na mambo mengi kama maeneo ya viwanda ili kupata uhakika wa mizigo. Wachina wakatuletea kampuni kwamba sasa ongeeni na kampuni hii, tukawa tunaongea tunaangalia terms au unataka tuwape hivi hivi? Alihoji.

Waziri Ngonyani alisema baadaye Wachina walileta Serikali ya Oman kwenye mradi huo.

“Hivyo vingine vyote wanatafuta tu sababu ya kutuchelewesha. Mara ya mwisho tumewaambia lazima yale maeneo tuliyobishania tukubaliane ifikapo Februari 28. Kwa hiyo tunatarajia kupata taarifa ya mwisho ya ujenzi wa bandari hiyo kutoka kwa contractors wa China na Oman,” alisema.