Saturday, February 18, 2017

Walanguzi Mexico watumia manati kuingiza dawa za kulevya Marekani

Manati hii ambayo ni mfano wa ndogo

Manati hii ambayo ni mfano wa ndogo zinazotumiwa na watoto ilifunguliwa kwa kukata kwa umeme kutoka mahali ilipochomelewa mahsusi kwenye ukuta kwa ajili ya kurusha dawa kuingia ndani ya Marekani. 

Arizona, Marekani.Walanguzi wa dawa za kulevya nchini Mexico wamebuni njia mpya ya kusafirisha hadi Marekani kwa kutumia manati kubwa yaliyoundwa mahsusi kwa ajili ya kurusha mihadarati hiyo.

Haijafahamika njia hiyo imetumika kwa muda gani, lakini iligunduliwa wiki hii na maofisa wa Marekani waliokuwa wanalinda doria.

Manati, ambayo ni njia ya kienyeji kabisa ilikuwa imefungwa kwenye ua ulio kwenye mpaka wa taifa hilo na Mexico na imekuwa ikitumiwa na walanguzi wa dawa za kulevya kurusha dawa hizo hadi ndani ya Marekani ambako kundi jingine huchukua.

Kugundulika kwa manati hiyo ya aina yake ni mafanikio mengine kwa Marekani ambayo imekuwa ikikabiliana na walanguzi wa dawa za kulevya na wahamiaji kutoka Mexico.

Rais Donald Trump ameahidi kujenga ukuta mrefu kuzuia wahamiaji na walanguzi wa mihadarati kuingia Marekani, lakini wamekuwa wakirusha dawa kupitia ukuta uliopo.

Habari zinasema manati hiyo iligunduliwa na maofisa hao kusini mashariki mwa Tucson, Arizona, wiki iliyopita.

Maofisa hao walisema waliwaona wanaume kadhaa wakitawanyika na kutoroka walipokuwa wanakaribia eneo husika.

Baada ya kufanya ukaguzi katika eneo hilo, maofisa hao  waligundua vifurushi viwili vya bangi vilivyokuwa na uzito wa kilo 21 vikiwa havijapakiwa na kurushwa na manati hiyo iliyobomolewa.

Ukuta

Hadi sasa umejengwa ukuta katika mpaka wa Mexico na Marekani umbali wa kilomita 1,770. Pamoja na mikakati ya Trump kutaka kujenga ukuta mrefu, walanguzi wamekuwa wakitumia mbinu tofauti kusafirisha dawa za kulevya hadi Marekani bila kukamatwa.

Njia nyingine zinazotumiwa ni kusafirisha kwa ndege ndogo zisizo na rubani na wakati mwingine kuchimba njia za chini kwa chini zinazofika hadi Marekani.

Machi mwaka jana, maofisa wa Marekani waligundua njia ya chini kwa chini ya umbali wa mita 380 kutoka kwenye mgahawa mmoja Mexico hadi kwenye jumba moja lililopo California.

Januari mwaka huu, maofisa waliokuwa wanafanya doria eneo la Pharr, Texas walikamata bangi yenye thamani ya Dola 789,467 za Marekani kwenye shehena ikisafirishwa kama ndimu. Bangi hiyo ya uzito wa pauni 3,947 ilisindiliwa katika ndimu ‘feki’ zaidi ya 34,000.

Mwaka jana katika mpaka huo huo, mamlaka zilikamata bangi ya uzani wa pauni 2,493 iliyokuwa ikisafirishwa kama karoti kwenye magari mawili aina ya Ford. Bangi hiyo ilikuwa na thamani ya Dola 500,000.

-->