Viongozi wa vijiji, vitongoji watajwa biashara ya wahamiaji haramu

Wahamiaji haramu zaidi ya 45 kutoka nchini Ethiopia wakiwa kwenye uwanja wa ndani wa ofisi za Uhamiaji mkoani Tanga baada ya kukamatwa katika eneo la Mombo, wilayani Korogwe walipokuwa wakisafirishwa kupelekwa Dar es Salaam kwa lori aina ya Fuso. Picha ya Maktaba

Muktasari:

Wahamiaji hulipa fedha nyingi kwa ajili ya usafiri na kujihifadhi kwa wenyeji wanaposubiri safari ya kwenda nchi za Kusini mwa Afrika.

Moshi. Baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji maeneo ya mpakani mwa Kenya na Tanzania, wametajwa katika mtandao wa kuwapokea na kuwahifadhi wahamiaji haramu kutoka Somalia na Ethiopia.

Uchunguzi wa gazeti hili umeelezwa kuwa kila mhamiaji hulipa kati ya Sh100,000 na Sh200,000 kwa ajili ya kuhifadhiwa katika nyumba za wenyeji wakati mawakala wakiwatafutia usafiri kwenda Mbeya. 

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, mawakala wakubwa wa kusafirisha wahamiaji hao wapo Kenya na Somalia na kila mhamiaji hulipa kati ya Dola 3,000 na 5,000 za Marekani.

Fedha hizo ni kwa ajili ya usafiri na gharama nyingine kutoka Kenya na kuingia Tanzania, kisha kusafirishwa hadi Tunduma, Mbeya kwa ajili ya kwenda Afrika Kusini.

Vijiji vinavyotajwa zaidi kutumika kama uchochoro wa kuingia kwa wahamiaji hao ni Kitobo, Holili na Tarakea wilayani Rombo na Madarasani, Kitobo na Riata, Wilaya ya Moshi.

Mbali na maeneo hayo, vijiji vya Jipe, Toloha, Ndea, Ngulu na Butu Usangi vinatajwa kuwa uchochoro wa wahamiaji haramu huku Kitongoji cha Mnoa kikitajwa kuwa kinara.

Pamoja na wahamiaji wengi kukamatwa wakiwa kwenye magari au nyumba za watu, hakuna gari wala nyumba ambayo imeshataifishwa na Serikali kama sheria ya mwaka 2008 inavyoelekeza.

Sheria hiyo inataka kutaifishwa kwa nyumba inayokutwa imehifadhi wahamiaji haramu au chombo cha usafiri kinachotumika kuwasafirisha.

“Hata ukitazama kila siku watu wanakamatwa kwenye malori, niambie ni lori la nani limetaifishwa au nyumba ya nani imetaifishwa na Serikali. Huu ni mtandao mpana,” alidokeza mtoa habari wetu.

Chanzo hicho kimedokeza wengi wanaoshtakiwa ni watu wadogo, lakini wale wanaopanga na kushiriki katika mtandao huu huwa hawaguswi na upelelezi kutokana na kutoa hongo.

“Polisi wanatengeneza mazingira kuwa ooh unajua mmiliki wa lori alikuwa hajui au mwenye nyumba hajui ni mpangaji tu aliwaingiza lakini ukweli ni kwamba anajua kila kitu,” alidai mtoa habari huyo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu cha 4(1), mtu yeyote anayewapokea, kuwasafirisha, kuwahamisha, kuwahifadhi wahamiaji haramu anatenda kosa na anaweza kufungwa jela au kutozwa faini.

Sheria hiyo imefafanua kuwa yeyote anayepatikana na hatia atatozwa faini ya kati ya Sh5 milioni na Sh100 milioni au kifungo cha kati ya mwaka mmoja hadi saba jela.

Lakini, pamoja na ukali wa sheria hiyo, bado baadhi ya viongozi wa vijiji, mgambo na mawakala wanadaiwa kugeuza suala la kuwaingiza, kuwatafutia hifadhi na kupanga mipango ya safari ya wahamiaji hao kama mradi wa kujiingizia kipato.

Kati ya Januari na Aprili, 2015, zaidi ya wahamiaji 200 kutoka Ethiopia na Somalia walikamatwa, lakini idadi hiyo inatajwa kuwa ndogo kulinganisha na wale wanaokwepa vyombo vya Dola.

“Wanatumia pikipiki kuwavusha (wahamiaji) kutoka upande wa Kenya kuja Tanzania na kila pikipiki inayokodishwa inalipiwa kati ya Sh50,000 na 150,000 kwa kichwa,” alidokeza mtoa habari wetu.

“Wakishawavusha wanawatafutia malazi kwenye nyumba za wenyeji maeneo ya Kifaru, Chekereni na Njiapanda na kila mwenye nyumba analipwa kati ya Sh50,000 na Sh100,000 kwa kichwa.”

Kwa mujibu wa chanzo kingine katika eneo la mji mdogo wa Himo, mawakala wakubwa ambao wako maeneo ya Taveta, Holili na Tarakea upande wa Tanzania na Kenya ndiyo wanaolipa fedha hizo.

Uhamiaji watoa kauli

Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Ebrosy Mwanguku alithibitisha kuwa baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wamekuwa wakiwasaidia wahamiaji hao hata wengine kuwatambulisha mamlaka za Serikali.

Mwanguku alisema wahamiaji haramu wako wa aina mbili, moja ni Wasomali na Waethiopia wanaopita kwenda Kusini na raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria.

“Wapo walimu 10 wanafundisha shule za English Medium (mchepuo wa Kiingereza), ambao kesi zao zipo mahakamani na wana vitambulisho vyote hadi vya kupigia kura,” alisema Mwanguku.

Hata hivyo, alisema wengi wanaoingia nchini na kufanya kazi bila vibali ni raia wa Kenya na huwa na nyaraka halali za Tanzania na wanapobanwa na uhamiaji ndipo hutoa pasi za kusafiria za Kenya.

“Watendaji wengine wamekuwa wakisimamia hadi uuzwaji wa ardhi kwa watu ambao si raia na wanawafichia siri huku wengine wakila yamini na kutoa ushahidi kuwa ni ndugu zao,” alisema.

Kuhusu kama kuna chombo cha usafiri au nyumba imewahi kutaifishwa kutokana na biashara hiyo, Mwanguku alisema, jambo hilo ni la kisheria kwani linahitaji amri ya mahakama.

Alisema yapo magari mawili ambayo walitakiwa kuyataifisha lakini ilitoka amri ya mahakama ikiwataka wayarejeshe magari hayo kesi iliyofunguliwa haikujieleza vizuri.

“Unakuta kesi inaendelea na tunapofika katikati inakuja amri ya mahakama turejeshe gari hilo mara moja kwa muhusika na sisi hatuna pingamizi tunarejesha na tunabaki na wahamiaji,” alisema.

Hata hivyo, alisema kwa sasa imekuwa vigumu kwa wahamiaji haramu kuingia nchini kutokana na idara yake kudhibiti njia zilizozoeleka ingawa alisema sasa wamebuni njia mpya ya kupitia Mkomazi.

Alisema baadhi ya watendaji wa vijiji wamekuwa wakiwahifadhi wahamiaji hivyo kufanya kazi ya kuwakamata kuwa ngumu kwani wengine wanapewa hadi vitambulisho vya mkazi.

Polisi wazungumza

Alipoulizwa kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita alisema hakuna gari, pikipiki au nyumba iliyotaifishwa katika kipindi cha miaka mitano na kwamba jeshi hilo huwakamata wahamiaji na kuwafikisha mahakamani wakiwa na vielelezo muhimu.

“Sheria iko wazi kuwa vyombo vya usafiri na nyumba zinazohusika na biashara za binadamu zitaifishwe, nitafuatilia kwa karibu kwa nini vielelezo hivyo vinashindikana kutaifishwa,” alisema Moita.

Hata hivyo, alikana madai kwamba polisi hupokea rushwa na kuandika maelezo ya kuwatoa katika kesi, wamiliki wa magari na nyumba akisema vielelezo hivyo hupelekwa mahakamani.