Mwanasheria Mkuu aviwakia vyombo vya usalama sakata la Ben Saanane

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju akizungumza wakati akichangia katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka 2017/2018 mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Masaju ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kumshangaa kwa kufanya kazi ya kuitetea Serikali bungeni badala ya kuhakikisha inatekeleza majukumu yake.

Dodoma. Hatimaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju amevunja ukimya wa sakata la kutoweka kwa kada wa Chadema, Ben Saanane, akieleza kuvishangaa vyombo vya usalama kutochukua hatua sahihi ili kupata ukweli.

Masaju ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kumshangaa kwa kufanya kazi ya kuitetea Serikali bungeni badala ya kuhakikisha inatekeleza majukumu yake.

Mchungaji Msigwa alisema hayo wakati akichangia hotuba za bajeti za Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

       Jana, AG Masaju aliinuka na kuzungumzia kutoweka kwa Saanane, ambaye ni msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na pia kujibu hoja za wabunge wa upinzani.

Akizungumzia matukio ya utekaji jana, Masaju aliliambia Bunge kuwa hafahamu sababu za suala hilo kujitokeza mara kwa mara ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

“Mambo ya utekaji yanajitokeza sana hapa, sijui kwanini? Mimi naomba kushauri mheshimiwa mwenyekiti, polisi waendelee kushirikiana na watu walio karibu sana na huyu mtu anayedaiwa kupotea,” alisema.

“Waisaidie polisi ili tupate ukweli. Kwanza familia yake na watu ambao amekuwa akifanya nao kazi kwa karibu watoe ushirikiano kama ambavyo wabunge wameshauri. Katika suala hili hatuwezi kuwa na double standard (kigeugeu).”

Saanane alitoweka katika mazingira ya kutatanisha Novemba 15 mwaka jana na licha ya wazazi, Chadema na wanaharakati kuhoji alipo, Jeshi la Polisi limekuwa halitoi taarifa hadi linapoulizwa na waandishi wa habari.

Hali hiyo imefanya mjadala wa kutoweka kwake uendelee kukua na wabunge kuamua kuhoji mamlaka husika kuhusu alipo, huku wakisema hofu inaongezeka kutokana n a matukio mengine ya utekaji, uvamizi na mbunge kutishiwa bastola siku moja baada ya kuachwa katika Baraza la Mawaziri.

Mjadala huo ulifikia hatua ya wabunge kuihusisha Idara ya Usalama wa Taifa na matukio hayo, jambo lililomlazimu Naibu Spika Tulia Ackson kupiga marufuku kuizungumzia taasisi hiyo.

Jana, Masaju alisema Mbowe alisema alikuwa akijua kuwa polisi wanafanya kazi, lakini hajui siku hizi wanafanyaje kazi.

Alisema watu walio karibu na familia wangesaidia kutoa taarifa Jeshi la Polisi.

“Mtu yeyote aliyeko kwenye public (umma) atusaidie halafu, we will take action accordingly (tutachukua hatua kadri inavyotakiwa). Mimi nilivyojua polisi walikuwa wanafanya kazi. Siku hizi sijui wanafanyaje kazi,” alisema Masaju.

“Sasa hivi tungekuwa na watu wanaoisaidia polisi kwa karibu mno. Sasa how we can handle this matter so much successfully ( ni vipi tunaweza kulishughulikia jambo hili kwa mafanikio)?” alihoji Masaju akionekana kumaanisha kuwa kama polisi wangekuwa wanafanya kazi vizuri, wananchi wangejitokeza kusaidia kutoa taarifa.

Alisema Mbowe amesaidia katika suala hilo katika hotuba yake ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

“Mheshimiwa Mbowe ametusaidia katika hotuba yake. Hakuna mtu aliye juu ya sheria,” alisema Masaju.

“Moja, watatueleza tangu lini mtu huyu anayedaiwa kupotea au kufariki, alipotea? Ilichukua muda gani kutoa taarifa? Halafu familia na watu waliokuwa karibu na huyu mtu na hii familia wameshapeleka suala hilo katika vyombo vya habari kwamba huyu mtu amepotea?”

Masaju alisema watu waliokuwa wanafanya kazi na Saanane, watu wake wa karibu na familia yake watoe taarifa katika vyombo vya dola ili vifanyie kazi kwa karibu.

Pia Masaju amewashukia wabunge wa upinzani kuwa wamekuwa wakiwatukana mawaziri wakati wanawaomba waende majimboni mwao kutatua kero zao.

Kuhusu uhuru wa mijadala ndani ya Bunge, Masaju alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano iko wazi kuhusu mijadala ya Bunge.

“Isome ibara ya kwanza na ya pili, unayo haki tu katika mijadala wakati wa kutekeleza majukumu yako ya Bunge ukizingatia Katiba na sheria za nchi,” alisema.

Alisema hadi sasa Serikali haijakataza vyombo vya habari kuripoti mambo yanayoendelea bungeni.

“Niwashauri waheshimiwa wabunge kama mtataka kurudi kwenye Bunge hili teteeni mambo yanayowahusu wapigakura wenu. Bunge la mwaka 2010 lilikuwa na hiyo live broadcasting lakini wabunge wengi hawakurudi,” alisema.

Kuhusu wateule wa Rais, Masaju alisema Rais John Magufuli amekuwa bungeni tangu 1995, mawaziri wanaomsaidia ni watumishi wa umma walikuwepo humu tangu kipindi hicho.

“Mimi nimeanza kazi mwaka 1994, kinachobadilika ni wanasiasa na nyie wenyewe mlienda kuomba kura, mkashindanishwa msio na uzoefu na walio na uzoefu. Walio na uzoefu wakashinda na wameunda Serikali,” alisema.

Alisema Serikali hii inaongozwa na watu wanaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi na ndio maana imeweza kutekeleza mambo yake kabla hata ya miaka miwili.

Kuhusu ushirikiano, Masaju alisema lazima uanzie bungeni na kupanuka hadi majimboni.

“Hamuwezi kuwa mnawatukana mawaziri, mnamtukana hapa Mwanasheria Mkuu, waziri mnamtukana halafu kesho mnamwambia aje jimboni kwako, kufanyaje huko?” alisema huku akipigiwa makofi na wabunge wa CCM.

Wakati akisema hayo, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema alisimama kuomba mwongozo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alimtaka aketi na kumpa fursa Masaju aendelee.

“Unasema waziri hana uwezo, sasa unamuitia nini jimboni?” alihoji.

Alisema Serikali haiwezi kuruhusu watu wachache wakaharibu amani ya Taifa kwa vitendo ama kwa kauli zao ama kwa nyendo zao.

“Ni lazima turudishe nidhamu ndani ya Bunge hili. Lazima amani itawale na usalama,” alisema Masaju.

Akichangia makadirio hayo, Mbunge wa Mtera (CCM), Job Lusinde alishauri kuanzishwa kwa dawati maalumu litakaloshughulikia upotevu wa watu.

“Naamini kuna watu wengi wamepotea. Leo tukiwauliza wabunge kila mmoja katika jimbo lake kuna mtu aliyepotea (watasema yupo). Hivyo endapo litaanzishwa dawati hilo, litasaidia kufanikisha kupatikana ufumbuzi,” alisema.

Akihitimisha mjadala wa hotuba yake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene alisema bado kuna matatizo mengi katika halmashauri mbalimbali kuhusu manyanyaso ya Machinga ambao wanafukuzwa kila mahali na kuwafanya washindwe kuchangia uchumi wa nchi yao.

“Hawa ni watu ambao wanachangia kwa sehemu kubwa uchumi wetu kama tutawapanga vizuri na kuwajali katika biashara zao, duniani kote watu hawawezi kuwa na uchumi rasmi, lazima wengine wawe nyuma na ndiyo hao Machinga,” alisema Simbachawene

Waziri aliwataka wakurugenzi kote nchini kuangalia namna bora ya kutenga maeneo mazuri ya kufanyia biashara na kuweka miundombinu mizuri ya maeneo hayo ikiwemo umeme na barabara ambayo yatakuwa na kivutio kikubwa cha watu wengi kukimbilia huko.

Kwa upande wake Waziri wa Utumishi, Angela Kairuki alisema suala la uwajibikaji na utawala bora limeimarika kwa kiasi kikubwa ikiwemo nidhamu ndani ya utumishi wa umma.

Aliwaagiza waajiri wote kufuata taratibu za uwajibishaji kwa watumishi wa chini yao ikiwemo kuzingatia muda wa kushughulikia matatizo ndani ya muda usiozidi siku 120 ili kuwapa nafasi watumishi kujua hatma yao. Kuhusu watumishi kupewa mafunzo, alisema utaratibu huo bado unaendelea na kwa mwaka wa fedha 2015/16 watumishi 395 walipewa mafunzo wakati kwa mwaka 2016/17 jumla ya watumishi 654 walipewa mafunzo ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuboresha utumishi wao.

Waziri alitaja idadi ya watumishi 54,236 kwamba wataajiriwa kwa mwaka wa fedha 2017/18 baada ya watumishi hewa zaidi ya 19,708 kuondolewa katika mfumo ambao uliwezesha kuokolewa kwa Sh 19.8 bilioni ambazo zingetumika kwa mishahara na watumishi.

Alisema tayari jumla ya watumishi 1595 walioshiriki kuongeza watumishi wamewajibishwa na wengine kufukuzwa kazi na kesi ziko mahakamani huku kukiwa na marejesho ya Sh 9 bilioni ambazo zimelipwa na watumishi hao.