Madaktari 258 walioomba kazi Kenya, wapewa ajira, watakiwa kuripoti

Muktasari:

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Mpoki Ulisubisya ilisema kuwa kwa wale waliopangiwa na TAMISEMI wanatakiwa kufika katika ofisi hizo zilizopo mjini Dodoma na waliopangiwa Wizarani waripoti ofisi ndogo za wizara Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Ajira 258 za madaktari walioomba kwenda kufanya kazi nchini Kenya, zimetolewa asubuhi hii na wanatakiwa kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi siku 14 kuanzia tangazo hilo kutoka.

Majina hayo yametangazwa kupitia tovuti ya www.moh.go.tz

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Mpoki Ulisubisya ilisema kuwa kwa wale waliopangiwa na TAMISEMI wanatakiwa kufika katika ofisi hizo zilizopo mjini Dodoma na waliopangiwa Wizarani waripoti ofisi ndogo za wizara Dar es Salaam.

Imeelezwa kuwa wahusika wanatakiwa kuripoti wakiwa na cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti halisi vya elimu ya sekondari, vyeti halisi vya taaluma, kwa madaktari vyeti halisi vya usajili wa Baraza la madaktari na kwa wafamasia vyeti halisi kutoka Baraza la wafamasia Tanzania.

Kwa wale ambao umri wao hauzidi miaka 45 wataajiriwa katika masharti ya kudumu na malipo ya uzeeni na kwa waliozidi umri wa miaka 45 kwa mkataba ambao itakuwa unarejewa kila baada ya miaka miwili.