Jaji Warioba ataka utafiti wa UDSM utumike kupunguza matukio ya uhalifu

 Jaji mstaafu Joseph Warioba 

Muktasari:

Utafiti huo umetoa mependekezo ya njia za kukabiliana na matukio hayo.

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  (UDSM) ndaki ya sayansi na siasa imezindua utafiti unaoonyesha jinsi mfumo wa nyumba kumi unavyoweza kupunguza matukio ya uhalifu nchini.

Utafiti huo umekuja kukiwa na mfululizo wa matukio ya uhalifu na uvunjifu wa amani ambayo yamekuwa yakigharimu maisha ya watu ikiwamo walinzi wa usalama (polisi).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa utafiti huo, Jaji mstaafu Joseph Warioba amesema kuwa utafiti huo ni muhimu kwa sasa kutokana na kuenea kwa matukio ya uhalifu na uvunjifu wa amani duniani ikiwamo Tanzania.

Amesema mfano halisi ni tukio la mauaji yanayoendelea Mkoa wa Pwani .

Amesema alisema ulinzi wa amani unatakiwa uanzie kwenye nyumba kumi, ambao ni kiungo muhimu kati ya wananchi na Serikali.

"Haiwezekani katika eneo wauliwe askari na watu kadhaa kuendelea kuuawa halafu wakazi wa eneo hilo wasimjue muhusika hata mmoja", amesema Warioba.

Amefafanua  kuwa licha ya mfumo wa nyumba kumi kuwa wa CCM tangu kuanzishwa kwake, bado ipo namna ya kuuboresha usiwe wa kichama kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa amani.

"Wakati wa mabalozi wa nyumba kumi walikuwa na nguvu kama ambavyo ipo kwa baadhi ya maeneo ya vijijini, ilikuwa akiingia mgeni lazima wafahamu, na walikuwa wakitoa taarifa wanapohisi kuna kitu hakipo sawa.

Kamishna wa Polisi Jamii,  Ali Mussa Ali amesema wamekuwa wakitafuta kiungo kati ya jeshi hilo na wananchi ndiyo maana wajumbe wa nyumba kumi walipoondoka kutokana na kuwapo kwa vyama vingi wakahamishia madaraka yao kwa watendaji wa kata.