Jinsi Sh31.7 trilioni za bajeti zitakavyotumika kwa miezi 12

Mkazi wa Kata ya Sabasaba Manispaa ya Morogoro, Omari Mkwizu akisikiliza bajeti kupitia redio wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018, bungeni Dodoma juzi. Picha na Juma Mtanda

Muktasari:

Katika fedha hizo, jumla ya mapato ya ndani yakijumuisha ya halmashauri, yanatarajiwa kuwa Sh19.97 trilioni sawa na asilimia 63.0 ya bajeti. Makusanyo ya kodi yanatarajiwa kuwa Sh17.1 trilioni na mapato yasiyo ya kodi Sh2.18 trilioni huku vyanzo vya halmashauri vikichangia Sh687.3 bilioni.

Dodoma. Takriban theluthi moja ya bajeti mpya ya Serikali ambayo ni Sh31.7 trilioni itakayotumika kwa miezi 12 ijayo kuanzia Julai Mosi, itatumika kulipia Deni la Taifa.

Katika fedha hizo, jumla ya mapato ya ndani yakijumuisha ya halmashauri, yanatarajiwa kuwa Sh19.97 trilioni sawa na asilimia 63.0 ya bajeti. Makusanyo ya kodi yanatarajiwa kuwa Sh17.1 trilioni na mapato yasiyo ya kodi Sh2.18 trilioni huku vyanzo vya halmashauri vikichangia Sh687.3 bilioni.

Washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh3.97 trilioni ambayo ni asilimia 12.5 ya bajeti yote, na ili kufanikisha bajeti hii, Serikali inatarajia kukopa Sh7.76 trilioni kutoka ndani na nje kwa masharti ya kibiashara.

Akiwasilisha bajeti hiyo juzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ili kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo awamu zinazofuata za ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge na uboreshaji wa bandari mbalimbali nchini.

Yapo mengi mazuri kwenye bajeti hii ya pili kwa Serikali ya Awamu ya Tano iliyo chini ya Rais John Magufuli lakini kadri deni la Taifa linavyozidi kuongezeka, ndivyo malipo yake yanavyokua.

Waziri Mpango alisema Serikali inapanga kutumia Sh19.71 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh11.9 trilioni zitaelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Katika fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, Dk Mpango alisema, “Sh7.2 trilioni zitatumika kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma na Sh9.46 trilioni kulipia deni la Taifa.”

Kiasi hicho kinachoelekezwa kulipa deni la Taifa ni asilimia 29.8 ya bajeti nzima. Waziri Mpango alisema hadi Machi mwaka huu, deni hilo lilikuwa limefika Sh50.8 trilioni. Wakati ikilipa kiasi hicho, mwaka huu, Serikali itakopa tena Sh7.76 trilioni.

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi, mwaka 2016, kulikuwa na wananchi milioni 48.67 Tanzania Bara ambao wastani wa pato la kila mmoja kwa mwaka ni Sh2.13 milioni. Deni la Taifa likigawanywa kwa idadi hiyo ya Watanzania, kila mmoja atakuwa anadaiwa zaidi ya Sh1.04 milioni hivyo nusu ya kipato chake kinatumika kulipa deni hilo.

Mishahara itakayolipwa, bila shaka itawajumuisha zaidi ya watumishi wapya 15,000 ambao Serikali imeahidi kuwaajiri baada ya kukamilika kwa uhakiki wa wafanyakazi hewa waliokuwa wanaiongezea gharama.

Vipaumbele

Katika utekelezaji wa bajeti ya 2017/18, matumizi ya Serikali yanatarajiwa kufikia asilimia 26.2 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 23.7 iliyokuwapo mwaka 2016/17 na kuhakikisha fedha zinaelekezwa kwenye maeneo ya vipaumbele ili kutekeleza mpango wa maendeleo wa mwaka.

Maeneo ya kipaumbele ambayo fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitaelekezwa ni pamoja na kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda na kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu.

Vilevile, Serikali imepanga kujenga mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mpango.

Miradi itakayopewa kipaumbele ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kuendeleza mradi wa chuma Liganga na makaa ya mawe mchuchuma na kuanzisha kanda maalumu za kiuchumi.

Mingine ni mradi wa gesi kimiminika (LNG), uendelezaji wa kituo cha biashara cha Kurasini na shamba la Mkulazi. Baada ya kukamilisha awamu mbili za usambazaji wa umeme vijijini, Serikali imesema itaendelea na awamu ya tatu ya mradi huo.

Serikali imetenga Sh1.052 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara kuu zenye urefu wa kilomita 720 kwa kiwango cha lami, madaraja 13 na ukarabati wa kilomita 150 kwa kiwango cha lami. Kiasi kingine, Sh30 bilioni zimetengwa kwa ajili ya barabara za mikoa zenye urefu wa kilomita 58.4 kwa kiwango cha lami.