Dart yajipanga kutatua changamoto ya kadi mabasi ya mwendokasi

Muktasari:

Mhandisi wa Rwakatare alitoa kauli hiyo jana (Ijumaa) baada ya kutembelea kituo kikuu cha Kimara mwisho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma.

Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Mhandisi Ronald Rwakatare amesema wapo mbioni kumpata mtoa huduma ya ukusanyaji mapato atakayekuwa na jukumu la kushughulikia suala la kadi ili kuondoa  changamoto mbalimbali  zinazowakabili watumiaji wa mabasi hayo.

Mhandisi wa Rwakatare alitoa kauli hiyo jana (Ijumaa) baada ya kutembelea kituo kikuu cha Kimara mwisho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma.

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mathew Kwembe  imeeleza kuwa Mhandisi Rwakatare amesema katika kipindi hicho cha mpito, mabasi yaendayo haraka yameweza kusafirisha watu 200,000 kila siku kutoka watu 50,000 waliokuwa  mwaka jana wakati mradi ukiaanza.

“Natambua kuwa kadi zimeisha na wakala unalishughulikia jambo hili na tutahakikisha kuwa tunaongeza kadi. Nawasihi wananchi watambue kuwa tupo katika kipindi cha mpito, mapungufu mengi yaliyojitokeza tutayarekebisha,” amesema Mhandisi Rwakatare.

Amefafanua kwamba, suala la kadi limechukua muda mrefu kwa sababu  mchakato wake unahusisha mfumo wa kibenki na hivyo amewataka  wananchi wa Dar es salaam kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki na kwamba jambo litapata ufumbuzi.