Timu Ethiopia na Timu Tanzania zabadilishana uzoefu uzalishaji wa umeme

Muktasari:

Rais Magufuli amesema timu hiyo inayoongozwa na Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia, Dk Seleshi Bekele imekuja nchini kubadilishana uzoefu na timu ya wataalamu wa Tanzania ambayo inasimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amekutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme iliyotumwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn kwa lengo la kubadilishana uzoefu na Tanzania.

Rais Magufuli amesema timu hiyo inayoongozwa na Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia, Dk Seleshi Bekele imekuja nchini kubadilishana uzoefu na timu ya wataalamu wa Tanzania ambayo inasimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).

Katika mazungumzo na timu hiyo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam leo 28 Juni, Rais Magufuli ameelezea nia yake ya kuhakikisha mawazo ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya tangu mwaka 1980 juu ya kuzalisha umeme kutoka maporomoko ya Mto Rufiji, yanatekelezwa haraka iwezekanavyo.

“Sasa hivi nchi yetu inazalisha megawatts 1,450 tu, lakini Stiegler’s Gorge itatuzalishia megawatts 2,100 umeme huo ni mwingi na utatusaidia katika viwanda, hivyo Serikali tumeamua kutekeleza mradi huu.

“Najua kutaanza kutokea vipingamizi mbalimbali, lakini naomba Watanzania tuwe na sauti moja, eneo litakalotumia ni Kilometa za mraba 1,350 ambalo ni sawa na asilimia 3 tu ya eneo lote la Hifadhi ya Selous yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 45,000,” amesema  Rais Magufuli.

Amesema mradi huo utakuwa na faida nyingi zikiwamo uvuvi, maji kwa ajili ya wanyamapori na kilimo.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia Dk Bekele amesema Ethiopia ambayo kwa sasa inazalisha megawatts 4,300 za umeme kwa kutumia maji, inayo miradi mingi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji ambayo itaiwezesha kufikia uzalishaji wa megawatts 17,000 ifikapo mwaka 2020.

Amesema yeye na watalaamu wa nchi hiyo wapo tayari kubadilishana uzoefu na Tanzania katika masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Dk Medard Kalemani na timu ya wataalamu wa Tanzania wanaosimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).