Serikali yaongeza mrabaha wa dhahabu kutoka asilimia nne hadi sita

Muktasari:

Mbali na dhahabu, pia mrabaha huo utahusisha madini ya shaba na fedha.

Dar es Salaam. Wizara ya Nishati na Madini imetangaza kuongezeka kwa mrabaha wa dhahabu kutoka asilimia nne hadi sita.

Akizungumza leo, Ijumaa Julai 21, Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa James  Mdoe amesema kupanda kwa mrahaba kunafuatia marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010.

Amesema pamoja na dhahabu, pia mrabaha huo utahusisha madini ya shaba na fedha.

Amesema mrabaha wa madini ya Tanzanite, rubi umepanda kutoka asilimia tano hadi asilimia sita.

Mdoe amesema kupitia marekebisho hayo mtu au kampuni itakayosafirisha madini nje ya nchi atakaguliwa na kuthaminishwa kwa kulipa ada ya asilimia moja ya thamani ya madini yanayosafirishwa.

Amesema baada ya kufutwa kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), shughuli zote za madini zitasimamiwa na Kamishna wa Madini.

Amesema Serikali imesimamisha utoaji leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini hadi Tume ya Madini itakapoundwa.

Amesema baada ya kuvunjwa kwa TMAA, watumishi ambao hawana tuhuma wataendelea na kazi wakiwa chini ya wizara hiyo.

Profesa Mdoe amewataka wananchi na wadau wa madini kuendelea kuwapa ushirikiano watumishi hao ili waweze kukusanya mapato ya Serikali.