Trump akwama tena kubatilisha Obamacare

Muktasari:

Mpango huo wa bima ya afya mara ya kwanza ulikataliwa Machi na sasa umekataliwa tena na hivyo kuwa pigo jingine kwa Rais Trump na Serikali yake.

Washington, Marekani. Juhudi za Rais Donald Trump kutaka mswada wa sheria ya bima ya afya maarufu kama Obamacare ufanyiwe marekebisho zimegonga ukuta katika Baraza la Seneti baada ya kukosa kura za kutosha.

Maseneta watatu wa Republican, John McCain, Lisa Murkowski na Susan Collins waliungana na maseneta wa Democratic kupinga marekebisho katika muswada huo.

McCain, ambaye Jumatatu aliunga mkono muswada huo uendelee baada ya kurejea kutoka kwenye matibabu alikofanyiwa operesheni ya uvimbe wa ubongo, siku nzima juzi alikuwa na vikao vya mashauriano pamoja na mkutano na waandishi wa habari ambapo alishutumu juhudi zilizosababisha kupigwa kura leo alfajiri.

Ingawa mabunge yote mawili yanadhibitiwa na wanachama wa Republican bado mabadiliko katika muswada huo mpya hayashawishi hata wafuasi wa chama hicho. Kwa mara ya kwanza ulikataliwa Machi.