Waziri Mkuu wa Pakistan ajiuzulu

Waziri Mkuu wa Pakistan aliyejiuzulu Nawaz Sharif

Muktasari:

Kujiuzulu kwa kiongozi huyo baada ya kubainika kwamba alisema uwongo kuhusu utajiri wake kunakipa nafasi chama chake kuteua mtu mwingine wa kushika wadhifa huo.

Islamabad, Pakistan. Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif amejiuzulu wadhifa wake muda mfupi baada ya Mahakama ya Juu kumzuia kuendelea kushikilia ofisi hiyo kama kiongozi mkuu wa serikali.

Uamuzi huo umetolewa leo baada ya uchunguzi kuhusu utajiri wa familia yake na ufichuzi wa mwaka 2015 wa wanasheria walioupa jina la Panama Papers, uliohusisha watoto wake na akaunti za benki ugenini.

Jopo la majaji watano wa Mahakama ya Juu walitangaza hukumu mbele ya umati mkubwa wa watu waliofurika katika chumba cha mahakama.

"Ameondolewa kuwa mmoja wa wabunge na kwa hiyo anakoma kuanzia leo kuwa Waziri Mkuu,” alisema Jaji Ejaz Afzal Khan katika ukumbi uliokuwa umefurika watu jijini Islamabad.

Kuondolewa kwa Sharif, kwa hoja kwamba alisema uongo kuhusu mali anazomiliki wakati alipochunguzwa kuhusu tuhuma za rushwa, ina maana sasa kwamba chama chake cha Pakistan Muslim League-Nawaz (PML-N) ambacho kina wabunge wengi, kinalazimika kuteua kiongozi mwingine wa Serikali.

Serikali inaweza pia kuitisha uchaguzi wa mapema, ingawa uchaguzi mkuu utafanyika Agosti mwaka ujao.