Mahakama yakataa ombi la Serikali Manji kuhojiwa TRA

Muktasari:

Yusufali Manji na wenzake watatu walikamatwa Julai mosi katika eneo la Chang’ombe  jijini Dar es Salaam na Julai 5 walipandishwa kortini kwa mara ya kwanza.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema haiwezi kumruhusu mfanyabaishara Yusufu Manji kuhojiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu suala la kodi.

Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha alisema jana kuwa hawezi kukubaliana na ombi hilo kwa sababu kesi iliyopo mbele yake ni ya uhujumu uchumi  isiyohusiana na masuala ya kodi.

Awali, upande wa mashtaka uliiomba mahakama hiyo kuruhusu Manji anayekabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi akahojiwe na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusiana na masuala ya kodi.     

Ombi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkeha na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa.

Wakili Kishenyi alidai waliomba agizo la mahakama la kumuita Manji, lakini kwa sababu za kiafya hakuweza kufika.

Alidai kwamba kwa sababu bado yupo mahakamani ni ombi lao achukuliwe na TRA kwa ajili ya mahojiano hayo na kwamba, ndani ya muda wa kazi atakuwa amerudishwa.

Wakili anayemtetea Manji, Alex Mgongolwa alidai ombi hilo kwa jana halikuwa sahihi kwa kuwa walikuwa wamefanya mawasiliano ya kimaandishi na mamlaka hiyo ya mapato.

Pia, Mgongolwa alidai kuwa mawakili wa Manji wanaoshughulikia masuala ya kodi siyo wao, hivyo anahitaji kuwasiliana nao ili mahojiano hayo yawe na manufaa na kwamba, maombi hayo yangeeleza anatakiwa Manji au kamupuni zake.

Hata hivyo, Wakili Kishenyi alidai  kuwa anayetakiwa ni Manji na siyo kampuni zake na akifika TRA akiona kuna haja ya kuwa na wataalamu wake atasema. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 18 kwa ajili ya kutajwa.

Katika kesi hiyo, Manji na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa Taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania vyenye thamani ya zaidi ya Sh 200 milioni na mihuri.

Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Deogratius Kisinda, Abdallah Sangey na Thobias Fwere.

Kesi hivyo ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi ambaye amefiwa na mama yake hivyo ilitajwa kwa Hakimu Mkeha.

Manji na wenzake wanadaiwa kuwa Juni 30 katika eneo la Chang’ombe ‘A’ Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam kwa pamoja walikutwa na polisi wakiwa na mabunda 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania vyenye thamani ya Sh192.5milioni na kwamba mali hiyo ilipatikana kinyume cha sheria.

Katika shtaka la pili, wanadaiwa kwamba Julai mosi katika eneo hilo walikutwa wakiwa na mabunda manane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania vyenye thamani ya Sh44 milioni.

Shtaka la tatu, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Juni 30 katika eneo hilo  walikutwa na muhuri wa Jeshi la Wananchi Tanzania wenye maandishi yanayosomeka “Mkuu 121 Kikosi cha JWTZ” bila ya kuwa na uhalali kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.

Aidha katika shtaka la nne, Maji na wenzake hao siku hiyo walikutwa wakiwa na muhuri wenye maandishi “Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupola Dodoma”.

Katika shtaka la tano, Manji na wenzake hao wanadaiwa kuwa siku hiyo katika eneo hilo walikutwa na muhuri wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania wenye maandishi “Commanding Officer 835 KJ Mgambo P.0. Box 224 Korogwe”.

Shtaka la sita inadaiwa kwamba washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa na polisi wakiwa namba ya usajili wa gari SU 383 ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.

Katika shtaka la saba washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Julai Mosi kwenye eneo hilo walikutwa na polisi wakiwa na namba za usajili wa gari SM 8573.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo. Mawakili wa utetezi ni Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Semi Malimi.