Mfuko wa Rais Magufuli watoa Sh 2 milioni kwa walioacha dawa za kulevya

Rais Magufuli

Dar es Salaam.Mfuko wa Rais wa Kujitegemea umetoa mkopo wa Sh 2milioni kwa kikundi cha vijana  Amua Kuacha Dawa za Kulevya (Amkudaku), kwa ajili ya kujishughulisha na masuala ya biashara na ujasiriamali ili kujikwamua kiuchumi.

Mfuko Rais umeanzishwa kwa ajili ya kusaidia kundi maalumu linalowajumuisha vijana na  walemavu wanaoishi katika mazingira hatarishi, ukiwa na dhamira ya kuhakikisha wanaofanya shughuli hatarishi wanaziacha na kuzifanya shughuli rasmi.

Mkopo huo ulitolewa leo Ijumaa Agosti 11 na mkurugenzi mtendaji wa mfuko huo,  Hajath Kitala alipokutana na kikundi kinachotoka eneo la Kigogo Manispaa ya Ubungo.

Kitala amesema kabla ya kutoa mkopo huo kwa vijana hao, mfuko huo ulitoa mafunzo  ya  ujasiriamali, afya na madhara ya dawa za kulevya kwa  kikundi hicho.

"Katika fedha hizi za mikopo kila mmoja amepata Sh 200,000 na hatujawapa mikononi bali tumewawekea katika akaunti zao walizozifungua,"amesema Kitala

Amesema mikopo hiyo itasaidia kundi la vijana hao ambao waliathirika na dawa za kulevya kutokuwa Watazamaji bali watakuwa wazalishaji mali na kuwa mfano bora wa wenzao.

Mlezi wa kikundi hicho, Mchungaji Richard Hananja alimshukuru Rais John Magufuli kupitia mfuko huo kwani ameonyesha nia njema ya kuwasaidia vijana waliokumbwa na matatizo mbalimbali.