Hakimu apata msiba, kesi ya Escrow yapigwa kalenda

Dar es Salaam. Msiba aliyopata Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi anayesikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili wafanyabiashara, Harbinder Sethi na James Rugemarila, umesababisha kesi hiyo kupigwa kalenda.

Kesi hiyo iliahirishwa jana na Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha kwa niaba ya Hakimu Shaidi ambaye amefiwa.

Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 31, na watuhumiwa wataendelea kusota rumande.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai jana alidai mahakamani hapo kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Hivyo aliomba ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika.

Washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Rugemarila ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP wanadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jiji Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mashtaka yanayowakabili hayana dhamana, lakini wote wawili kwa nyakati tofauti walifungua maombi ya kusaka dhamana katika Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.

Hata hivyo, juzi Sethi alilazimika kuliondoa ombi lake mahakamani baada ya mawakili wake kutoka Afrika Kusini kukwama kumtetea kwa kukosa kibali cha Jaji Mkuu.