Mwili uliookotwa baharini waacha hofu mkoani Tanga

Pangani. Hofu imetanda kwa wakazi wa Wilaya ya Pangani mkoani Tanga baada ya mwili wa mtu mmoja uliovunjwa mikono kufunikwa na mifuko ya plastiki usoni na kufungwa kuokotwa Bahari ya Hindi karibu na  Kijiji cha Kipumbwi huku akiwa hajulikani aliuawa wapi na kutoswa majini.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba ni kuwa mwili huo wa mwanaume anayekadiriwa kuwa na miaka 40 uliokotwa jana saa 4.00 usiku na wavuvi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kipumbwi, Subiri Masanga alilifahamisha Mwananchi kuwa wavuvi waliokuwa wakiendelea na shughuli zao katika Bahari ya Hindi waliona kitu kikielea na walipofuata walikuta kuwa ni mwili wa binadamu.

“Waliponipigia simu kunijulisha nilituma boti kwenda kumchukua huku nikiwasiliana na jeshi la polisi ambao walikuja na daktari ambapo baada wa kuwasili walimpima na kuamuru uzikwe hapa kijijini kwa kuwa ulikuwa umeharibika sana,” alisema Masanga.

Mwenyekiti huyo alisema kutokana na mwelekeo wa upepo wa bahari ni kwamba

mwili huo unahofiwa kukokotwa kutokea maeneo ya Tanga au Mombasa na kama usingeonwa na wavuvi uingeweza kufika Bagamoyo au Dar es salaam.

“Kulingana na mwelekeo wa upepo tunahisi alitoswa eneo la Tanga au Mombasa baada ya kumuua na kumfunga kamba,” alisema Masanga.

Diwani wa Kata ya Pangani Magharibi, John Semnkande alisema hofu imetanda miongoni mwa wakazi wa Pangani baada ya kusikia taarifa hiyo kwa sababu ameuawa kikatili na haijulikani sababu za kumuua na kumtosa baharini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Wakulyamba alisema jeshi hilo linafanya uchunguzi kubaini wapi aliuawa na kuhakikisha walitoenda mauaji hayo wanatiwa mikononi mwa dola ili hatimaye hatua za kisheria dhidi yao zichukuliwe.

 “Jeshi la polisi limeanza kufanyia uchunguzi tukio hili, tunataka kwanza kuwakamata waliohusika na mauaji haya na baada ya hapo tutajua sababu.

“…niwahakikishie tu kwamba nitawapa taarifa zote tutakapochunguza,” alisema

Wakulyamba.