Viwanda vya saruji vyalia gharama usafirishaji makaa ya mawe nchini

Muktasari:

Kampuni ya Twiga Cement inatumia gesi asilia huku Dangote ikipewa machimbo yake ya makaa ya mawe

Dar es Salaam. Wakati viwanda vya saruji vikitekeleza agizo la Serikali la kutumia makaa ya mawe yanayochimbwa nchini, gharama za usafirishaji zimeelezwa kuwa changamoto mpya.

Maoni hayo yalitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simba Cement, Reinhardt Swart alipozungumza na waandishi wa habari za biashara kuhusu mwenendo wa sekta hiyo nchini.

“Ubora unaridhisha, lakini gharama za usafirishaji zipo juu,” alisema Swart.

Akifafanua kuhusu changamoto hiyo, Swart alisema kiwanda chake kinatumia tani 12,000 za makaa ya mawe kwa mwezi, hivyo malori 400 yenye kubeba tani 30 yanatakiwa kutoka Ngaka mkoani Ruvuma mpaka Tanga kila siku.

Alisema hata kama watasafirisha kupitia Bandari ya Mtwara, gharama zitakuwa juu kutokana na ushuru unaotozwa. “Utalazimika kulipa ushuru wa bandari za Mtwara na Tanga. Hivyo, gharama zitaendelea kuwa juu,” alisema.

Licha ya makaa ya mawe kwa kampuni zilizo mbali na machimbo, Swart alisema baadhi wameunganishwa na gesi asilia hivyo kupunguza gharama za uzalishaji kwa kiwango kikubwa.

“Baadhi ya wazalishaji wa saruji wanatumia gesi asilia tofauti na sisi ambao tunalazimika kusafirisha makaa ya mawe kutoka mbali. Mwisho wa siku, sote tunategemea soko moja,” alibainisha.

Tanzania inajitosheleza kwa mahitaji ya saruji na kwa miaka kadhaa sasa imekuwa ikizalisha ziada inayouzwa nje ya nchi, ambako ushindani ni mkubwa hasa kutoka nchi zilizoendelea. Kuanzia mwaka 2014, saruji ya ziada inayozalishwa nchini ni zaidi ya tani milioni mbili.

Kampuni hiyo ya kwanza kusajiliwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kutoka sekta ya saruji, kwa miaka sita iliyopita imelipa kodi ya mapato zaidi ya Sh252 bilioni. Ili kuendelea kufanya vizuri sokoni, mkurugenzi huyo aliiomba Serikali kuangalia namna nzuri ya kupunguza gharama za uendeshaji ili ufanisi wa sekta hiyo uwe na tija.

“Saruji yetu ya ziada tunaiuza nchi za Rwanda, Burundi na DRC (Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo) ambako mataifa ya nje kama Iran na Brazil yanapeleka bidhaa zao ingawa kampuni zao zinazalisha kwa gharama ndogo kuliko sisi. Ushindani ni mkubwa,” alisisitiza.

Wazalishaji saruji

Baadhi ya kampeni nyingine za uzalishaji saruji Mbeya, Lake na Camel.