Tuesday, May 22, 2018

Marekani,China zapatana

 

Washington, Marekani. Marekani na China zimetangaza kusitisha vita vya kibiashara kati yao, baada ya kukubaliana kuondoleana vitisho vya ushuru na kufanya kazi pamoja kupata makubaliano mapya.

Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin na mshauri mkuu wa Rais Donald Trump kuhusu uchumi, Larry Kudlow wamesema maofisa wa nchi hizo mbili walifikia muafaka wa kuchukua hatua za kuondoa nakisi ya biashara baina ya nchi zao.

Baada ya mkutano uliofanyika mjini Washington, wajumbe wa pande mbili walitangaza mpango ambamo China itaagiza bidhaa za kilimo na nishati kutoka Marekani ili kupunguza nakisi ya dola bilioni 335 kila mwaka katika biashara baina ya nchi hizo.

Katika mkutano huo, Marekani ilitaka China ipunguze nakisi hiyo kwa kiasi cha dola bilioni 200 ifikapo mwaka 2020. Imearifiwa kuwa Waziri wa Biashara wa Marekani, Wilbur Ross anapanga safari ya kikazi nchini China katika muda ambao haukubainishwa.

Mazungumzo

Akihojiwa na televisheni ya Marekani Fox News, Mnuchin alisema Marekani na China zimepata maendeleo katika mazungumzo ya kiuchumi na kibiashara kati ya pande mbili yaliyomalizika hivi karibuni. Aliongeza kuwa pande hizo mbili zitaendelea na mawasiliano kuhusu masuala ya biashara.

Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki ilisema nchi hizo mbili zimeahidi kuwa hazitazusha vita vya kibiashara dhidi ya upande mwingine na zitachukua hatua madhubuti kupunguza kwa kiwango kikubwa urari wa Marekani kwenye biashara na China.

Tuesday, May 22, 2018

China yapitisha sheria ya uzazi

 

Beijing, China. Serikali inafikiria kufuta sera ya sasa inayowabana wazazi kuzaa mtoto mmoja, ofisa mmoja katika ofisi ya uzazi wa mpango amesema akitaja sababu kuwa kukabiliana na ongezeko la wazee katika jamii na pengo la kijinsia.

Sheria tata, ambazo zilikuwa zikiwabana wanandoa wengi wa mijini kuzaa mtoto mmoja na vijijini kuzaa wawili tu, zilianzishwa miaka ya 1970 katika juhudi za taifa hili kubwa kudhibiti ongezeko la watu waweze kuendana na raslimali zilizopo.

Lakini sasa naibu waziri katika Tume ya Taifa ya Idadi ya Watu na Mpango wa Uzazi Zhao Baige alisema maofisa wanapitia maelezo ya kina kuhusu athari za kimazingira, kijamii na nyinginezo katika kubadili sheria.

Alipoulizwa ikiwa wana mpango wa kufuta sera ya kuzaa mtoto mmoja Baige aliwaambia wanahabari jijini Beijing kwamba kuna “mchakato mkali” wa kiutafiti hivi sasa.

Sababu za kupitia upya

Baraza la Taifa, ambalo ni Baraza la Mawaziri limeamuru ufanyike utafiti kuhusu madhara ya kuondoa sera hiyo iliyodumu karibu miongo minne ikitaka kuweka mabadiliko ya kitaifa, walisema watu walioomba wasitajwe majina wakati serikali inafanya majadiliano ili iweze kufikia uamuzi.

Uongozi unataka kupunguza pengo la wazee na kuondoa chanzo hicho kikubwa cha ukosoaji wa kimataifa, mtu mmoja alisema.

Mtu huyo alisema mapendekezo yanayojadiliwa kwa sasa yatakuwa mbadala wa sera ya kudhibiti idadi ya watu ambapo mmoja ameita kuwa ni “uhuru wa uzazi” kuwaruhusa watu kuamua idadi ya watoto wa kuzaa.

Mtu mwingine alisema uamuzi huo unaweza kutolewa mapema iwezekano robo ya nne yam waka naakaongeza inawezekanao tangazo rasmi linaweza kusogezwa hadi mwaka 2019.

Wednesday, May 16, 2018

Kagera waanzisha madawati upimaji Ebola mipakani

 

By Alodia Dominick, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

 Mkoa wa Kagera umechukua tahadhari ya ugonjwa wa Ebola ulioibuka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) kwa kuanzisha madawati ya afya katika maeneo yote ya mipakani kwa ajili ya kuwapima wanaoingia Tanzania kutokea nchini humo.

Akizungumza na MCL Digital Kaimu Ofisa Afya mkoa wa Kagera, Gerazi Ishengoma amesema hatua hiyo imechukuliwa tangu Aprili 8, 2018 ugonjwa wa Ebola uliporipotiwa kuibuka Congo.

Ametaja vituo vya mipakani vilikofunguliwa kuwa ni Mtukula wilaya ya Misenyi, Murongo wilaya ya Kyerwa, Kabanga na Rusumo wilayani Ngara.

Kwa mujibu wa Ishengoma, miongoni mwa dalili za ugonjwa wa Ebola ni homa kali, uchovu, maumivu ya koo, tumbo, misuli, kuumwa kichwa na viungo vingine, kichefuchefu na kuhara pamoja na figo kutofanya kazi vizuri.

Mtu anayeugua ugonjwa huo pia hutokwa na damu sehemu zote za wazi za mwili kuanzia kwenye vinyweleo, pua, mdomoni na masikio, dalili zinazoonekana kati ya siku mbili hadi wiki tatu baada ya kuambukizwa.

Inapofikia hatua ya juu, mgonjwa wa Ebola hupata mshtuko wa moyo, shinikizo la damu, mapigo ya moyo kwenda kasi, kupungua kwa mzunguko wa damu mwilini,maumivu ya viungo na hatimaye viungo kushindwa kufanya kazi.

Wednesday, May 16, 2018

Zuma ahusishwa na jaribio la kumuua mkuu wa polisi

 

Durban, Afrika Kusini. Tuhuma nzito zimetolewa kwamba maveterani wa zamani wa jeshi la ukombozi ‘Umkhonto weSizwe’ walipewa mkataba wa kumuua mkuu wa zamani wa polisi wa upelelezi wa Jimbo la KwaZulu-Natal Johan Booysen.
Tuhuma hizo zilitolewa bungeni Jumanne na Mbunge wa DA Dianne Kohler Barnard aliyedai maveterani hao walipewa makataba huo baada ya kukutana na rais wa zamani Jacob Zuma, katibu wa chama cha ANC wa KwaZulu-Natal, Super Zuma na aliyekuwa mratibu wa mpito wa ANC ya KwaZulu-Natal, Sihle Zikalala.
Akizungumza katika mjadala wa makadirio ya matumizi ya Jeshi la Polisi Kohler Barnard alidai: "Wenzangu, ikiwa mnadhani kwa hatimaye kuondolewa ndani ya Jeshi la Polisi (SAPS) bosi mhuni wa makosa ya jinai Richard Mdluli, kimiujiza kulikuwa kumefanikisha kuweka kando ya muunganiko wa serikali kugubikwa na ufisadi, mtakuwa mmekosea.
"Kwa nini mnafikiria Mamlaka ya Uendeshaji wa Mashtaka ya Taifa (NPA) imerejesha mashtaka dhidi ya Jenerali Johan Booysen, mashtaka ambayo tayari yalikuwa yametupwa na mahakama? Lengo ni kumzuia kufanya kazi pamoja na Waziri (wa Polisi Bheki) Cele."
Alisema Booysen "alikuwa na kinyongo kamili akafunua makaratasi yaliyojaa vumbi ya NPA na akatupatia tuchungulie".
"Je, unaweza kufikiri kwamba haya hayakuwa malipo kwa majaribio ya kumfunga Toshan Panday?" Panday ni mfanyabiashara wa Durban aliyehusishwa na rais wa zamani wa Zuma.
Alisema ofisa wa polisi ambaye alijaribu kumhonga Booysen rand milioni mbili (R2m) "fedha taslimu katika mfuko" bado alikuwa kazini.
Kohler-Barnard pia alidai majaribio mawili yalifanywa kutoa uhai wa mwendesha mashtaka mwandamizi baada ya kuwasilisha ripoti ya kurasa 200 kuhusu kwa nini mashtaka dhidi ya Mdluli hayapaswa kufutwa.
"Je, unajua ni nani! Huyo ni waziri wa kivuli wa Sheria Glynnis Breytenbach!" alisema.
"Kuna uthibitisho kutoka vyanzo vitatu vya kujitegemea na vya kuaminika kuwa mavaterani wa MK kutoka Cornubia karibu na Phoenix huko KwaZulu-Natal walichukuliwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo baada ya mikutano na watu si wengine zaidi isipokuwa rais wa zamani aliyeng’atuliwa Jacob Zuma, Super Zuma na Sihle Zikalala. Dudu Myeni pia amehusishwa baada ya kukutana na maveterani hao," alisema Kohler Barnard.

Wednesday, May 16, 2018

Wasichana 239,000 hufa kila mwaka India kwa kubaguliwa

 

New Delhi, India. Wastani wa watoto wa kike wapatao 239,000 wenye umri chini ya miaka mitano hufariki dunia nchini kila mwaka kutokana na wazazi wengi kupendelea watoto wa kiume dhidi ya wasichana.
Wanasayansi waliofanya utafiti huo na matokeo yake kuchapishwa Jumanne katika jarida la The Lancet walibaini uwiano mgumu kati ya wanaume na wanawake, na kwamba zaidi ya wanawake milioni 63 “kitakwimu wamepotea” kote nchini sababu inaweza kuwa matokeo idadi kubwa ya vifo vya wanawake, utafiti wa kiuchumi wa serikali umeonyesha.
Moja ya sababu zilizozoeleka zilizotajwa kuwa kiini cha idadi ya vifo vingi vya wanawake nchini India ni utoaji mimba wa kuchagua watoto, lakini uchunguzi ulibaini “ubaguzi wanaofanyiwa watoto wa kike," jambo linaloonyesha tatizo si kabla ya kuzaliwa kwao bali huendelea hata wakishazaliwa.
"Ubaguzi wa kijinsia wanaofanyiwa watoto wa kike hauwi tu kuzuia wasizaliwe bali unaweza kuharakisha kifo kwa waliozaliwa,” alisema mhariri mwenza wa utafiti huo Christophe Guilmoto wa Chuo Kikuu cha Paris Descartes.
"Usawa wa kijinsia hauhusu tu haki za elimu, ajira au uwakilishi kisiasa; bali pia unahusu matunzo, chanjo, na lishe kwa wasichana na hatimaye kuishi kwao,” alisema Guilmoto.
Utafiti huo umebaini kwamba maeneo ya vijijini ambako kuna watu wengi wanaokosa matunzo mazuri ni wasichana. Majimbo makubwa ya Kaskazini mwa India - Uttar Pradesh, Bihar, Rajasthan, na Madhya Pradesh – takwimu zinaonyesha ndiyo yana theluthi mbili ya vifo vya wanawake nchini India.

Monday, May 14, 2018

Mpinzani mkuu Iraq aongoza katika matokeo

 

Baghdad, Iraq. Kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa madhehebu ya Shia Muqtada al-Sadr, hadi kufikia mchana jana alikuwa akiongoza katika matokeo ya uchaguzi wa wabunge uliofanyika Jumapili.
Hadi nusu ya matokeo yakiwa yamehesabiwa na kutangazwa, kambi inayoongozwa na aliyekuwa kamanda wa vikosi vya angani na inayoungwa mkono na Iran ya Hadi al-Amiri ilishika nafasi ya pili huku waziri mkuu Haider al-Abadi akiangukia nafasi ya tatu.
Matokeo yote yalitarajiwa kutangazwa jana jioni baada ya kukamilisha kupokea na kuhesabu kura kutoka majimbo manane likiwemo la Nineveh ambalo ni la pili kuwa na viti vingi bungeni baada ya Baghdad.
Uchaguzi huo wa wabunge unatumika kama kura ya maoni tangu lilipoangushwa kundi la dola ya Kiislamu la ISIS mwaka 2017.

Monday, May 14, 2018

Kenyatta amwondoa Ruto kwenye Twitter

 

Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta ameondoa jina la makamu wake William Ruto kati ya washirika wake kwenye Twitter, hatua iliyoanza kuzua mjadala kwenye mitandao ya kijamii.
Kutokana na uamuzi huo rais sasa hawezi kusoma ujumbe wowote wa kwenye Twitter wa naibu wake huyo katika akaunti yake. Hadi mwishoni mwa wiki, Kenyatta bado alikuwa mmoja wa wafuasi wake.
Japokuwa hatua hii haina thamani yoyote kwa usoni, matumizi ya mitandao ya kijamii yanaonyesha tabia za watu hivyo suala hilo haliwezi kupuuzwa.
Kenyatta alianza kupunguza wafuasi wake tangu Aprili 2016, alipowaondoa watu 600 hadi akabaki na watu 11. Aliwaondoa viongozi wengi wa kimataifa, magavana na mawaziri.
Miongoni mwa hao 11 aliokuwa anaendelea kusoma habari wanazotuma kwa njia ya Twitter walikuwa naibu wake, mkewe Margaret Kenyatta na msemaji wa Ikulu Manoah Esipisu.
Jicho la mwanahabari wa Daily Nation Augustine Sang ambaye ni mtumiaji mkubwa wa mitandao ya kijamii ndilo lililobaini.
Katika siku za hivi karibuni imeelezwa kuna mvutano ndani ya Jubilee tangu Kenyatta aliposhikana mkono na kiongozi mkuu wa upinzani na aliyewahi kuwa waziri mkuu Raila Odinga.

Monday, May 14, 2018

Watu 19 wafa kwa mlipuko wa ebola

 

Kinshasa, DR Congo. Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo) umesababisha vifo vya watu 19, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema.
Shirika hilo limesema Jumatatu kwamba jumla ya matukio 39 ya maambukizi yameripotiwa mpaka sasa Kaskazini mwa jimbo la Ikweta. Wafanyakazi watatu wa afya ni miongoni mwa wanaougua maradhi hayo.
Wizara ya Afya kwa ushirikiano na WHO wanafuatilia watu waliogusana na waathirika na wanawapatia chanjo ya majaribio ya Ebola.
WHO inasema chanjo hiyo iitwayo rVSV-ZEBOV, imejaribiwa kwa maelfu ya waliojitolea Ulaya, Afrika na Marekani na ilipitishwa kwamba ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Virusi ambavyo vinasababisha homa ya kutoka damu husambazwa kwa njia ya kugusana na mwili wenye majimaji wa mtu au mnyama aliyeambukizwa.

Monday, May 14, 2018

Serikali Ethiopia yajadiliana na wapinzani wake

 

Addis Ababa, Ethiopia. Serikali ya Ethiopia imeanzisha rasmi mazungumzo kuhusu mageuzi ya kisiasa kwa kushirikisha kundi la upinzani lililoko uhamishoni la Oromo Democratic Front (ODF).
Taarifa ya ODF iliyotolewa Mei 13 imethibitisha kwamba ujumbe wa ngazi ya juu wa serikali ulikutana na viongozi wao Mei 11 hadi 12 na wakafanya majadiliano yaliyozaa matunda.
“Kwa kuzingatia msimamo wetu wa muda mrefu, ODF ilisisitiza dhamira yake ya kuongeza na kupanua mchakato wa mageuzi na demokrasia,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
ODF hawakutaja ni maofisa gani wa serikali walikuwa katika ujumbe huo lakini waliongeza kwamba serikali ilikubali kwamba iko tayari kushiriki katika juhudi zote zisizo za vurugu.
ODF ilisema kwamba hata hivyo ilikuwa hatua chanya na kwamba bado kuna mengi zaidi yanahitajika kufanyika.
“Pande zote mbili zilitilia mkazo kwamba majadiliano haya na ODF ni mwanzo wa ushirikishwaji mpana zaidi,” walisisitiza.
Taarifa ilisema kwamba chama kilikuwa tayari na shauku ya kuchukua jukumu la kuwezesha wadau wote kufanya mageuzi ambayo lazima yaongoze kuwa na mjadala wa pamoja katika kuelekea kwenye upatanisho wa kitaifa na maridhiano.
Walitangaza pia kwamba wajumbe watarejea nyumbani wakiwa na mpango wa kuanzisha mchakato kwa ajili ya mazungumzo ya kina. ODF watarejea na kuanza mchakato wa kusajili chama cha siasa nyumbani.

Sunday, May 13, 2018

Wagombea 7000 wapigiwa kura Iraq

 

Iraq, Ni historia ambayo inatarajiwa kuandikwa nchini Iraq siku chache zijazo baada ya wananchi kujitokeza kupiga kura kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo kutangaza ushindi dhidi ya kundi la Dola la Kiislam, IS.

Nchi hii ilifanya uchaguzi tangu mwaka 2003, zaidi ya wananchi milioni moja walipiga kura nchini humo jana Jumamosi huku wengi wakipuuza upigaji kura huo.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo (IHEC), idadi ya wapiga kura safari hii ni ndogo ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Tume hiyo imesema zaidi ya wagombea 7,000 walijitokeza kugombea majimbo 18 ili kuweza kuingia katika bunge lenye jumla ya viti 329 na matokeo hayo yanatarajiwa kutangazwa leo.

Waziri Mkuu, Heidar Abadi anapambana na vyama vya upinzani vya Kishia vyenye uhusiano wa karibu na Iran.

Mgombea mwingine mwenye nguvu anayechuana na Abadi alitajwa kuwa ni Waziri Mkuu Mstaafu Nouri al-Maliki.

Wananchi hao walionyesha fahari kwa kuweza kupiga kura kwa mara ya nne tokea kuangushwa kwa utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Saddam Hussein, lakini pia walisema hawana matumani kwamba kura hiyo inaweza kuleta utulivu katika taifa hilo.

Taifa hilo kwa sasa linakumbwa na migogoro mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi pamoja na rushwa.

 

-->