Wednesday, July 18, 2018

Mgombea aahidi kubadili jina la Zimbabwe

 

Si mara ya kwanza kwa nchi hiyo kubadili jina na hata baadhi ya nchi za Afrika nazo pia zimebadili majina yake kwa sababu mbalimbali

Harare, Zimbabwe. Zikiwa zimebaki siku chache kufanyika uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe, kiongozi wa MDC-T ameapa kubadili jina la nchi hiyo.

Kiongozi huyo, Nelson Chamisa ameapa kuwa atalibadilisha jina la nchi hiyo na kuwa ‘Great Zimbabwe’ akieleza kuwa lile la sasa la nchi hiyo lina laana.

“Zimbabwe haiwezi kuendelea kuwa Zimbabwe kwa sababu imegeuzwa kuwa gofu la Zimbabwe,” Chamisa aliwaambia maelfu ya wafuasi wake katika mkutano wa hadhara mashariki mwa mji wa Mutare.

“Jina la Zimbabwe limelaaniwa kama mnavyoona timu yetu ya Taifa ya soka inashindwa kila mashindano, hata mchezo wa kriketi tunashindwa.”

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 40 ana lengo la kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa kwanza utakaofanyika Julai 30 tangu alipoondoka madarakani Robert Mugabe.

Kwa mujibu wa Shirika Utangazaji la Uingereza (BBC), suala la kubadili jina kwa Zimbabwe si mara ya kwanza kwani awali ilijulikana kama Rhodesia Kusini kati ya mwaka 1898-1964, ambalo ni la wakoloni wa Kiingereza.

Mwaka 1960, wazalendo walianza kuliita taifa hilo Zimbabwe. Jina hilo linalotokana na maneno mawili “dzimba” na “dzamabwe” yenye maana ya nyumba ya mawe kwa lugha ya Kishona inayozungumzwa maeneo mengi nchini humo, limekuwa utambulisho wa mafanikio ya nchi hiyo.

Nchi ya Burkina Faso ilipewa jina hilo na Rais Thomas Sankara akiibadili kutoka Upper Volta Agosti 1984.

Alilichagua jina hilo ambalo ni maneno mawili “Burkina” na “Faso” kutoka makabila mawili makuu yanayozungumzwa nchini.

Jina la zamani la Upper Volta lilitoka Ufaransa iliyokuwa ikiitawala nchi hiyo kutokana na mto wa Volta uliopita katika eneo hilo.

Burkina katika lugha ya Moore lina maana ya “wanaume wenye heshima” na Faso katika lugha ya Dioula lina maana “alikozaliwa baba” na yakichanganywa inakuwa Burkina Faso.

Tanganyika ndilo lililokuwa jina la Tanzania Bara ya sasa hadi mwaka 1964 liliporithiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Zanzibar ya zamani, kwa upande mwingine ilijumuisha visiwa vya Bahari ya Hindi vya Unguja na Pemba.

Ghana ilibadilisha jina lake kutoka Gold Coast mwaka 1957 kuendana na hadhi yake mpya ya kuwa jamhuri baada ya kupata uhuru kutoka kwa Waingereza.

Kiongozi wa kwanza wa Ghana, Dk Kwame Nkrumah alilipa Taifa hilo jina jipya muda mfupi baada ya kujinyakulia uhuru.

Kwa sasa Ghana inajivunia jina hilo lenye ishara ya mafanikio na uzalendo.

Nchi ya Swaziland ndilo Taifa la hivi karibuni kubadili jina ambalo Aprili, 2018 liliamua kujiita Jamhuri ya Ufalme wa eSwatini.

Jina hilo jipya lilitolewa na mfalme wa nchi hiyo, Mswati III katika sherehe za kuadhimisha miaka yake 50 na pia miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo.

eSwatini yenye wakazi milioni 1.3 inapakana na Afrika Kusini na Msumbiji.

Wednesday, July 18, 2018

Trump adai Urusi haikuingilia uchaguzi wa Marekani 2016

 

Vigogo wa Congress wadai ameitia aibu Marekani, vyombo vya habari vyamshukia

Helsinki, Finland. Rais wa Marekani, Donald Trump ameitetea Russia na tuhuma kwamba iliingilia uchaguzi wa rais nchini mwake mwaka 2016.

Baada ya mazungumzo ya ana kwa ana na Rais wa Russia, Vladmir Putin yaliyodumu kwa saa mbili, Rais Trump aliyapinga mashirika ya ujasusi ya Marekani akisema hakukuwa na sababu yoyote ya Russia kuingilia uchaguzi wa Marekani.

Kwa upande wake, Rais Putin alisisitiza kwamba kamwe nchi yake haijawahi kuingilia uhusiano wake na Marekani kwa nia ya kuuharibu.

Kabla ya mkutano huo, viongozi wa Demokratic walimuonya Trump wakimtaka awe mwangalifu dhidi ya Putin huku wengine wakisema kuwa haukuwa uamuzi mzuri kwa rais wa Marekani kufanya mkutano wa aina hiyo.

Trump alitakiwa na mwandishi kueleza baada ya kuandika mapema kwenye mtandao wa Twitter kuwa Marekani inalaumiwa kwa hali tete ya sasa kati yake na Russia.

Alisema pande zote zilifanya makosa lakini akakataa kugusia mambo kadhaa yakiwemo kuhusika kwa jeshi la Russia nchini Ukraine na kulimega eneo la Crimea, shambulizi la kutumia kemikali ya novichok kusini mwa England na kushtakiwa kwa raia wa Russia kwa kuingilia kati uchaguzi wa Marekani.

Badala yake, alisisitiza kuwa hakukuwa na ushirikiano kwa njia yoyote ile kati ya timu yake ya kampeni na Russia.

Alipoulizwa ikiwa anaweza kuishutumu Russia na Putin moja kwa moja kwa kuingilia kati uchaguzi, Trump alisema maofisa wake wa ujasusi, akiwemo mkurugenzi Dan Coats walimwambia kuwa wanafikiri kuwa ni Russia, lakini baadaye Putin alimwambia nchi yake haikuhusika.

Viongozi wamjia juu

Kiongozi wa wachache katika Bunge la Senate, Chuck Schumer aliitaja hatua ya Trump kuwa ya aibu ambayo ilikuwa hatari na dhaifu.

John Brennam, mkurugenzi wa CIA wakati wa uongozi wa Barack Obama alisema Trump alifanya makosa ya ‘uhaini’.

Mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2008 nchini Marekani, John McCain alisema alichofanya Trump ni kitendo kibaya zaidi na hakijawahi kufanywa na rais wa Marekani.

Baada ya kukutana katika mkutano wake wa kilele na mwenzake wa Russia nchini Finnland, Trump alisema dunia inatamani kuona uhusiano mwema baina ya mataifa hayo. Mkutano huo uliofanyika mchana ulikuwa ukifuatiliwa kwa karibu na viongozi wa dunia na hasa barani Ulaya.

Trump alifungua mkutano huo kwa kusema kwamba ulimwengu unataka kuiona Russia na Marekani zikiwa katika uhusiano mzuri.

Upande wake, Putin alisema amekuwa akiwasiliana kwa simu na Trump pamoja na kukutana katika matukio ya kimataifa, lakini umewadia wakati wa kuwa na majadiliano ya kina kuhusu matatizo mbalimbali ya kimataifa.

Spika wa Bunge la Congress nchini Marekani, Paul Ryan alisema katika taarifa yake kuwa Russia iliingilia uchaguzi na inaendelea kujaribu kuikandamiza demokrasia nchini Marekani na duniani kote.

Alisisitiza kuwa Marekani lazima ijikite katika kuiwajibisha Russia na kumaliza mashambulizi yake mabaya ya demokrasia.

Kiongozi wa wachache wa Congress, Nancy Pelosi alisema udhaifu wa Trump mbele ya Putin ulikuwa wa kutia aibu.

Pia kiongozi huyo wa Democratic alisema tabia ya Trump inadhihirisha kuwa Russia wana kitu fulani dhidi ya kiongozi huyo cha binafsi, kifedha au kisiasa.

Vyombo vya habari

Shirika la Habari la ABC lilisema Trump alikubali madai ya Putin kuwa Taifa la Russia halijawahi kuingilia uchaguzi wa Marekani na alikataa fursa ya kuliwajibisha kwa makosa ambayo yalifanyika katika nchi ambayo anaiongoza.

Gazeti la Washington Post liliandika kuwa Rais Trump hawezi kupinga upingaji wa Putin, lakini amemkaribisha vizuri rais huyo wa Russia na kuendelea kulalamikia uchunguzi wa mamlaka za kiitenligensia za Marekani.

Uchaguzi wa Rais wa Marekani, mwaka wa 2016 ulikuwa wa 58 katika historia ya nchi hiyo. Ulifanyika Novemba 8, 2016.

Katika uchaguzi huo, Trump aliyepeperusha bendera ya Republican pamoja na makamu wake, Mike Pence alimshinda mgombea wa Democratic, Hillary Clinton aliyekuwa na mgombea mwenza, Tim Kaine.

Wednesday, July 18, 2018

Wanajeshi waliomng’oa rais wapewa tuzo

 

Cairo, Misri. Bunge la Misri limepitisha sheria ambayo inaweza kuwafanya maofisa waandamizi wa jeshi kuwa na kinga kuhusiana na ghasia ambazo zilisababisha kung’olewa Rais Mohamed Morsi mwaka 2013.

Sheria hiyo inampa Rais Abdel Fattah al-Sisi haki ya kuwateua maofisa ambao wanastahili tuzo ambayo ni pamoja na zawadi mbalimbali kutokana na jitihada zao hizo.

Pia inawapa kinga dhidi ya uchunguzi wa makosa yoyote yaliyofanywa kuanzia Julai 3, 2013 hadi Juni 8, 2014 katika kipindi ambacho Morsi aliondolewa madarakani hadi katika siku ya mwanzo ya al-Sisi kuwa rais.

Watu wengi waliuawa wakati majeshi ya usalama yalipovunja kwa nguvu maandamano ya kukalia eneo la Uwanja wa Rabaa mjini Cairo wakimuunga mkono Mursi Agosti 2013, katika mojawapo wa matukio yaliyomwaga damu kwenye historia ya Misri.

Akihutubia kwa njia ya televisheni mara baada ya mapinduzi hayo, al-Sisi aliyekuwa mkuu wa majeshi alisema katiba ya Misri imesitishwa kwa muda na mkuu wa mahakama ya katiba kuteuliwa kuwa kiongozi wa muda nchini.

Al-Sisi alitangaza kwamba jeshi lilikuwa linaangalia masilahi ya watu wa Misri baada ya maandamano makubwa ya upinzani yaliyomtaka Rais Morsi kujiuzulu.

Kufuatia hotuba yake hiyo katika televisheni, Morsi alitoa taarifa kupitia akaunti yake ya Twitter, akiita hatua ya jeshi ni “mapinduzi kamili”. Pia aliwasihi Wamisri wote kukataa hatua hiyo ya jeshi na kuwataka kuwa na amani.

Kama sehemu ya mwongozo mpya ulioungwa mkono na jeshi, al sisi alitaka uwepo uchaguzi wa rais na wabunge pamoja na jopo kutathmini katiba na kamati ya mashauriano kitaifa. Alisema mwongozo ulikubaliwa na makundi kadhaa ya kisiasa na pia kuwasihi watu wa Misri kuacha vurugu.

Jeshi lilimpa Morsi saa 48 kutatua matatizo ya kisiasa au kuwepo hatari ya jeshi kuingilia kati.

Morsi ni nani?

Morsi ni mwanasiasa wa Misri na rais wa tano wa Taifa hilo aliyetawala kuanzia Juni 30, 2012 hadi Julai 3, 2013 alipopinduliwa na al-Sisi kufuatia maandamano makubwa ya kupinga utawala wake.

Kiongozi huyo alikuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia katika historia ya Taifa hilo baada ya miaka mingi ya utawala usio na uchaguzi.

Morsi ni msomi aliyefikia ngazi ya PhD na alikuwa mwanachama mwandamizi wa kundi la Udugu wa Kiislamu. Awali, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa tawi la kisiasa la Chama cha Haki na Uhuru (FJP), kilichoundwa na Udugu wa Kiislamu baada ya mapinduzi ya mwaka 2012.

Sunday, July 15, 2018

#WC2018: Kylian Mbappe ashinda tuzo ya mchezaji bora wa Kombe la Dunia 2018.

Kiungo wa Ufaransa na Paris Saint-Germain,

Kiungo wa Ufaransa na Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe 

Moscow, Russia. Nyota imemuwakia. Hiyo ndio kauli unayoweza kutumia unapomzungumzia kiungo wa Ufaransa na Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe, baada kutangazwa kuwa ndiye mshindi wa tuzo ya mchezaji bora chipukizi katika fainali Kombe la Dunia 2018.

Licha ya kuvunja rekodi nne kwenye michuano hii, ikiwa ni pamoja tuzo ya mchezaji mwenye umri mdogo kuwahi kucheza kombe la dunia, rekodi ya kinda aliyewahi kufunga mabao mawili kwenye Kombe la Dunia, rekodi ya kinda aliyefunga kwenye mechi ya fainali na rekodi ya kutwaa kombe, Mbappe ndiye mchezaji bora wa mashindano haya.

Mbappe amekuwa mchezaji wa pili wa Ufaransa kuwahi kushinda tuzo hiyo, baada ya Paul Pogba aliyeshinda tuzo hiyo miaka minne iliyopita. Tuzo hiyo inaweza ikashindwa na mchezaji aliyezaliwa na baada ya Januari mosi.

Kigezo kingine kinachotumiwa kupata mshindi wa tuzo hiyo ni ufundi uwanjani, kasi, utundu udambwidambwi, mchango kikosoni na uungwana mchezoni, kwa mujibu wa kamati ya ufundi ya FIFA. Mbappe amefunga mabao manne kwenye michuano hii, ikiwemo bao la nne, katika ushindi walioupata kwenye fainali dhidi ya Croatia.

Sunday, July 15, 2018

#WC2018: Luca Modric ndio mchezaji bora wa Kombe la Dunia 2018Nahodha wa Croatia, Luka Modric

Nahodha wa Croatia, Luka Modric 

Moscow, Russia. Licha ya kushuhudia timu yake ikishindwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia, nahodha wa Croatia, Luka Modric ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mashindano.

Kiungo huyo wa Real Madrid, ameshinda tuzo hiyo akiwabwaga Kylian Mbappe, Antoine Griezmann na nahodha wa Ubelgiji Eden Hazard ambao walikuwa wanapigiwa upatu kuibuka washindi hasa baada ya kuonesha kiwango kilichotukuka katika michuano hiyo iliyofika tamati rasmi leo, Jumapili, Julai 15, 2018.

Croatia walifungwa mabao 4-2 na Ufaransa katika mchezo mkai wa fainali uliopigwa katika dimba la Luzhniki ambao ni uwanja wa taifa wa urusi. Mabao ya Ufaransa yaliwekwa kambani na Mario Mandzukic (alijifunga), Antoine Griezmann, Kylian Mbappe na Paul Pogba huku Croatia wao wakijipatia mabao yao kupitia kwa Mario Mandzukic na Iva Perisic.

Wachezaji wengine ambao wamewahi kubeba tuzo hiyo ni pamoja na Lionel Messi, Zinedine Zidane, Ronaldo de Lima, Davor Suker, Diego Maradona na Paolo Rossi. Tuzo hii, inamuweka Modric katika nafasi nzuri ya kushinda tuzo ya mwaka huu ya Ballon d'Or.

Saturday, July 7, 2018

Ubelgiji yaing'oa Brazil, kucheza na Ufaransa Jumanne

 

Moscow, Russia. Ubelgiji imeingia nusu fainali ya Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Russia baada ya kuibanjua nje mabingwa mara tano Brazil kwa mabao 2-1, katika mechi kali.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ubelgiji kufikia hatua hiyo tangu 1986.

Vijana wa Roberto Martinez walitawala kwa kiasi fulani mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kazan ikiwa ni ushindi wake wa tano mfululizo.

Brazil iliyoruhusu bao moja katika fainali za Russia ilifungwa bao baada ya kona ya Nacer Chadli kumbabatiza Fernandinho na kujaa wavuni katika dakika ya 10 ikiwa ni bao la nane la kujifunga katika fainali za mwaka huu

Fernandinho ambaye anacheza pamoja na Kevin De Bruyne Manchester City alimwadhiri baada ya kupiga kombora la umbali wa mita 20 lililojaa kwenye wavu wa Brazil baada ya kazi nzuri ya Romelu Lukaku.

 

Ubelgiji sasa itacheza na Ufaransa nusu fainali ambao waliwatoa Uruguay kwa kuwachapa mabao 2-0. Nusu fainali itachezwa St Petersburg Jumanne ijayo kuanzia saa 3:00 Usiku.

Wednesday, June 27, 2018

Mnangagwa atuhumu wafuasi wa Grace kutaka kumuua

 

Harare, Zimbabwe. Rais Emmerson Mnangagwa anasema anahisi kundi lenye uhusiano na aliyekuwa mke wa Robert Mugabe, Grace Mugabe kwamba ndilo liko nyuma ya jaribio la kumuua lililoshindwa Jumamosi iliyopita katika mkutano wa hadhara mjini Bulawayo.


Watu wawili walifariki na wengine zaidi ya 40 walijeruhiwa kutokana na mlipuko wa bomu la mkono uliotokea karibu na mahali alipokuwa Mnangagwa muda mfupi baada ya kuhutubia umati wa watu katika eneo linalotajwa kuwa ngome ya upinzani.
Rais Mnangagwa alimwambia mwandishi wa shirika la habari la BBC, Fergal Keane kwamba analituhumu katika jaribio hilo kundi la G40, ambalo lilikuwa likimuunga mkono Grace katika juhudi zake za kutaka kuwa rais.
Mugabe aliondolewa madarakani kwa shinikizo la jeshi Novemba mwaka jana na nafasi yake ilichukuliwa na Mnangagwa. Ulienea uvumi kwamba Grace alikuwa amejipanga kurithi mikoba ya mumewe na kuwa mkuu wa nchi.
Mnangagwa hakumshutumu wala kumhusisha Grace katika jaribio hilo, lakini aliiambia BBC kwamba anatarajia wahusika watakamatwa hivi karibuni.
"Wala sijui kama ni mtu mmoja, nafikiri ni zaidi ya mtu mmoja. Nafikiri ni suala la kisiasa lililopangwa na watu wenye kinyongo,” alisema.
Mnangagwa wakati akiwa makamu wa rais, na Grace walikuwa wanaongoza makundi mawili tofauti ndani ya chama tawala cha Zanu PF ya kuwania mmoja kuteuliwa kuwa mgombea urais kumrithi mkongwe Mugabe. Kundi lililokuwa likimuunga mkono Grace lilijitambulisha kuwa ni Generation 40 kwa kifupi G40 na la Mnangagwa lilijulikana kama Lacoste.
Kundi la G40 lilikuwa likimshambulia Mnangagwa na kuna wakati lilifanya maandamano ya kumpinga na lilichangia kufutwa umakamu wa rais. Pamoja na jaribio hilo Mnangagwa amesema Zimbabwe iko imara.

Wednesday, June 27, 2018

Polisi waanika mali walizokamata kwa waziri mkuu

 

Kuala Lumpur, Malaysia. Polisi wametangaza kuwa wamekamata mabegi ya fedha taslimu, vito vya thamani, pochi, saa na vitu vingine kutoka maeneo yenye uhusiano na aliyekuwa waziri mkuu Najib Razak vyote vikifikia thamani ya dola za Marekani 273 sawa na Sh.621.5 bilioni.
Mkuu wa polisi kitengo cha uhalifu wa kibiashara nchini Amar Singh, Jumatano aliwaambia wanahabari kwamba gharama ya vitu vyote vilivyokamatwa kutoka majumba sita ambayo yanahusishwa na Najib ni kati ya dola 224 milioni na dola 273 milioni.
"Hatukuweza kukokotoa thamani yake kwenye maeneo husika kwa sababu viwango vilikuwa vikubwa sana," alisema Singh na kuongeza kuwa mali iliyokamatwa ndiyo kubwa zaidi katika historia ya Malaysia.
Mkuu huyo wa polisi alisema iliwachukua muda wa siku tatu tena kwa msaada wa mashine sita ya kuhesabia na maofisa 22 kutoka Benki Kuu ya Malaysia kuhesabu fedha zilizokamatwa katika maeneo hayo, na akaongeza kiasi cha dola 28.9 milioni kilikamatwa kikiwa katika aina 26 tofauti ya fedha ikiwemo ringgit ya Malaysia.
Mamlaka zinamchunguza Najib ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa fedha zilizopotea kifisadi katika mfuko wa maendeleo ya miradi uitwao 1MDB uliokuwa umeasisiwa na waziri mkuu huyo.
Tangu alipoangushwa na Mahathir Mohamad katika uchaguzi mkuu wa Mei mwaka huu, Najib amezuiwa kuondoka nchini na amekuwa akihojiwa na tume ya kupambana na ufisadi hadi kufikia nyumba zake na za familia kupekuliwa.

Monday, June 18, 2018

Kabila ataka sheria ya kulinda marais wastaafu

 

Kinshasa, DR Congo. Wabunge wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanatarajiwa, kwa ombi maalumu la Rais Joseph Kabila, kukutana kwa lengo la kutunga sheria ya kuwalinda marais wanaostaafu.
Spika wa Bunge, Aubin Minaku amesema, Rais Kabila amewataka wabunge wakutane na kujadili na kupitisha sheria hiyo haraka iwezekanavyo.
Tangazo hilo linaweza kuwa ni ishara nyingine kwamba kweli Kabila anakusudia kung’atuka madarakani baada ya uchaguzi mkuu Desemba licha ya fununu kwamba anajaribu kufanya ghiliba ili akwepe kifungu kinachomzuia kugombea tena.
Waziri Mkuu Bruno Tshibala aliliambia shirika la Reuters wiki iliyopita kwamba Rais Kabila hatajitokeza tena kuwania urais likiwa ni tangazo la wazi zaidi kutoka kwa ofisa wa ngazi ya juu serikalini kuhusu suala hilo.
Lakini Kabila mwenyewe hajaweka wazi hadharani ikiwa hatagombea tena na baadhi ya wafuasi wake katika wiki za hivi karibuni walijenga uhalali wa kisheria ambao utamruhusu kugombea tena.
“Kutokana na ombi la rais wa jamhuri, kitaitishwa kikao maalumu cha Bunge,” alisema spika wa Bunge la Chini, Aubin Minaku alipozungumza na wasaidizi wake Ijumaa.
“Tutapitia mambo kadhaa yakiwemo kuangalia sheria kuhusu hadhi ya viongozi wa zamani, uteuzi wa mjumbe mpya katika mahakama ya katiba na sheria ya kodi ili kukuza sekta ya viwanda,” alisema.

Monday, June 18, 2018

Kayihura aweka wanasheria kumtetea

 

Kampala, Uganda. Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) wa zamani aliyewekwa katika kizuizi cha kambi ya jeshi ya Makindye Jenerali Kale Kayihura amekataa kutoa ushirikiano kwa maofisa wa jeshi na polisi wanaomhoji.
Badala yake mkuu huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi ameajiri wanasheria wawili kwa ajili ya kushughulikia suala lake na ametaka afikishwe kwenye mahakama ya kiraia.
Jenerali Kayihura alikamatwa wiki iliyopita kutoka shambani kwake Kashagama, wilayani Lyantonde na akasafirishwa hadi Kampala na kwa sasa anahojiwa kuhusu masuala kadhaa katika kambi ya Makindye.
Hata hivyo, vyanzo vilivyo karibu na idara ya upelelezi vinasema kwamba amekataa kutoa ushirikiano kwa timu ya wapelelezi, ambao anawatuhumu kwamba wanamuonea.
Jopo la wapelelezi wanaomhoji inadaiwa linajumuisha Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi (CDF), Jenerali David Muhoozi, Waziri wa Usalama Jenerali Elly Tumwine, Kamanda wa Upelelezi Jeshini (CMI) Brigedia Abel Kandiho, Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi wa Ndani (ISO), Frank Kaka Bagyenda, Mkurugenzi wa Kupambana na Ugaidi Abbas Byakagaba pamoja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Grace Akullo.
Vyanzo hivyo vinasema kwa siku mbili, alikuwa akishirikiana vizuri na timu ya upelelezi lakini walipoanza kumhoji maswali yanayomhusisha na kifo cha aliyekuwa msemaji wa polisi Andrew Kaweesi na ujasusi, inaelezwa alibadilika na akakataa kutoa ushirikiano akitaka akutane na wanasheria wake.
Alipofuatwa ili afafanue madai hayo, msemaji wa polisi Brigedia Richard Karemire alikataa kutoa maelezo ya kina, akiishia kusema Jenerali Kayihura ana haki ya kuonana na wanasheria wake na kwamba taarifa nyingine yoyote itakuwa inatolewa kwa utaratabu pale inapobidi.

-->