Friday, November 17, 2017

TRA yapeleka elimu ya kodi kwa wachimbaji

Mkurugenzi wa huduma na elimu ya mlipa kodi

Mkurugenzi wa huduma na elimu ya mlipa kodi (TRA) Richard Kayombo 

By Rehema Matowo

Geita. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wametoa elimu ya mlipa kodi kwa wachimbaji wadogo mkoani Geita ili watekeleze agizo la Serikali la kulipa asilimia tano wanapouza madini kwa mujibu wa sheria.

Mkuu wa idara ya huduma na elimu wa TRA mikoa ya Kanda ya Ziwa, Lutufyo Mtafya alisema wameamua kuwafuata wachimbaji hao maeneo yao ili kuwaelimisha watimize matakwa ya kisheria ya kulipa kodi.

Baadhi ya wachimbaji hao eneo la Rwamgasa wilayani Geita, walisema uelewa duni kuhusu sheria ya ulipaji kodi ndiyo sababu inayowafanya kutolipa kodi.

Emmanuel Samson alisema ni vyema elimu ikatolewa zaidi kwa kuwa sasa wanashindwa kuelewa, kwani awali walijua kodi ya halmashauri na ya mmiliki wa kiwanja lakini nyongeza ya asilimia tano nyingine ni mzigo kwa wachimbaji.

Tuesday, November 7, 2017

Wanawake walamba dume mikopo Kanda ya Ziwa

Katibu wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji

Katibu wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’I Issa 

By Rehema Matowo, Mwananchi rmatowo@mwananchi.co.tz

Geita. Makundi ya wanawake yamenufaika kwa kiasi kikubwa na mkopo uliotolewa na taasisi mbili za fedha kwa ushirikiano na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Katibu wa baraza hilo, Beng’I Issa alisema kuwa, asilimia 57 ya mkopo huo umeelekezwa kwa makundi yanayoundwa na wanawake, huku yale ya wanaume yakipata asilimia 43.

Miongoni mwa wajasiriamali walionufaika na mikopo hiyo wamo mamalishe, wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini, wamachinga na waendesha bodaboda.

Fedha hizo zimetolewa na Benki ya Posta na UTT Microfinance ambazo kwa pamoja zimetoa mkopo wenye riba nafuu wa Sh2.8 bilioni kwa vikundi 277 vya wajasiriamali kutoka Kanda ya Ziwa.

Hundi ya fedha za mkopo huo ilikabidhiwa kwa wawakilishi wa vikundi hivyo na waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Vijana, Jenista Mhagama wakati wa hafla iliyofanya mjini Geita juzi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhagama aliwataka wanachama 3,789 wa vikundi vitakavyonufaika na mkopo huo kutumia vyema fedha hizo kuendeleza miradi ya uzalishaji itakayowawezesha kumudu marejesho na hatimaye watu wengi zaidi kukopeshwa.

Waziri huyo aliimwagia sifa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kutoa mikopo ya zaidi ya Sh500 milioni kwa vikundi vya maendeleo vya vijana na wanawake kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani na kuziagiza halmashaur nyingine nchini kuiga mfano huo.

“Ni vyema sasa vikundi vya maendeleo vya wananchi kupitia vicoba na saccos vijielekeze kwenye kuanzisha na kuendesha viwanda vidogo na vya kati vinavyotumia malighafi inayopatikana kwenye maeneo yao,” alisema Mhagama.

Pia, aliyaagiza mabaraza ya uwezeshaji kusaidia wananchi kutambua, kufikia na kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo yao ili kujikwamua kiuchumi.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku aliwataka wanufaika kuitumia vizuri mikopo hiyo.

Tuesday, November 7, 2017

Tecno wazindua simu mpya ya Phantom 8

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kampuni ya utengenezaji wa simu ya Tecno kuzindua simu mpya aina ya Phantom 8 nchini Dubai, baadhi ya wateja wameanza kutoa ‘oda’ zao kabla ya uzinduzi hapa nchini.

Uzinduzi wa simu hiyo nchini unatarajiwa kufanyika Novemba 11 na utakwenda sambamba na kukabidhi simu kwa wateja walioweka ‘oda’ katika duka la Mlimani City jijini Dar es Salaam. Ofisa uhusiano wa Tecno, Erlick Mkomoya alisema wateja wengi wamevutiwa na uwezo wa simu hiyo iliyo tofauti na matoleo yaliyotangulia. “Baada ya kuzinduliwa Dubai, tulilazimika kuanzisha zoezi la uwekaji oda za simu hizo Oktoba 26 katika duka letu baada ya watu kuonekana kuwa na shauku ya kuzitumia pindi tu zitakapoingia nchini,” alisema Mkomoya.

Mfanyabiashara katika soko la Kariakoo, Hamidu Rahim alisema utaratibu wa uwekaji ‘oda’ unawasaidia watu wenye kipato kidogo kumudu gharama.

Thursday, November 2, 2017

NMB kuanza kutoa mikopo ya nyumba

Mkuu wa kitengo cha mauzo wa Benki ya NMB,

Mkuu wa kitengo cha mauzo wa Benki ya NMB, Omari Mtiga akizungumza wakati wa mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam juzi. Kulia ni meneja mikopo ya nyumba, Miranda Lutege na Kushoto ni meneja mwandamizi wa wateja binafsi, Ally Ngingite. Picha na Omari Fungo 

By Tumsifu Sanga, Mwananchi tsanga@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Benki ya NMB imezindua mikopo ya nyumba itakayolipwa kwa riba nafuu ndani ya miaka 15.

Taarifa ya benki hiyo inasema wanufaika watakuwa Watanzania wanaoishi nchini hata ughaibuni wanaotaka ama kununua, kujenga au kukarabati.

Meneja wa mikopo ya nyumba wa NMB, Miranda Lutege alisema mteja aliyekidhi vigezo atapewa asilimia 80 ya thamani ya nyumba anayotaka kujenga, kukarabati au kununua.

“Kiwango cha juu cha mkopo kwa mteja ni Sh700 milioni. Mume na mke wanaweza kuunganisha kipato chao na kupewa mkopo huu kukamilisha ndoto yao ya kumiliki nyumba,” alisema Lutege.

Naye mkuu wa kitengo cha mauzo kwa wateja, Omary Mtiga alisema kabla ya kuuchukua mkopo utakaorejeshwa ndani ya miaka 15, mteja atatakiwa kuweka asilimia 10 ya kiwango anachoomba.

Kigezo muhimu cha mkopo huo ni muombaji kuwa na hatimiliki ya nyumba au kiwanja anachotaka kujenga nyumba.

Thursday, November 2, 2017

Gharama za uendeshaji zaikaanga benki ya kilimo

“Hawa watu uliwaleta kwa gharama kubwa mwaka

“Hawa watu uliwaleta kwa gharama kubwa mwaka jana na wakaondoka ukawalipa gratuity ya Sh300 milioni...labda unieleze ukijumlisha miaka miwili unafika Sh500 milioni kwa benki changa bado napata shida.”Ezekiel Maige 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeiagiza bodi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuhakikisha gharama za uendeshaji ikiwamo mishahara, mikopo na kodi za pango zinapungua.

PAC ilitoa agizo hilo juzi baada ya kupitia hesabu za benki hiyo za mwaka wa fedha 2015/16, zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akitoa maagizo hayo juzi, mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka alisema benki hiyo ni taasisi changa lakini gharama za uendeshaji ziko juu.

“Hasa mishahara, mikopo mingine ya watumishi hivyo kamati inaiagiza bodi kuhakikisha gharama hizi zinapungua,” alisema.

Kaboyoka ambaye pia ni mbunge wa Same Mashariki, alisema agizo jingine ni benki kuangalia upya gharama za pango ili kuona kama wanaweza kutumia sehemu ya jengo hilo au kutumia majengo ya Serikali kwa sababu ofisi nyingi za Serikali zimehamia Dodoma. Pia, iliiagiza bodi hiyo kujenga majengo yake kwa kutumia mashirika yanayojenga kwa gharama nafuu.

Kaboyoka aliagiza bodi hiyo kuwasilisha kwa CAG mkataba, mchanganuo na gharama kuhusu mfumo wa Tehama (software) na leseni baada ya kamati kushindwa kupata majibu ya kuridhisha.

Baadhi ya wabunge waliochangia akiwamo, Ezekiel Maige wa Msalala alisema katika vitabu vyao mafao (gratuity) ilikuwa Sh221 milioni lakini imepanda hadi Sh265 milioni.

Mbunge wa Magomeni, Jamal Kassim alisema katika vitabu inaonekana uamuzi wa kununua mfumo wa Tehama haukufanywa na benki hiyo, bali ofisi ya waziri mkuu.

Naye mwenyekiti wa bodi ya TADB, Rosebud Kurwijila alisema wataangalia suala la kuajiri ili kupunguza gharama zinazotokana na kuajiri mpya.

Kuhusu ununuzi wa Tehama, kaimu mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Francis Assenga alisema fedha za kufunga mfumo huo zilipatikana kupitia mradi wa PSP ambao upo chini ya ofisi ya waziri.

Thursday, October 26, 2017

TRA yazifungia shule za Eckernforde

 

By Raisa Said, Mwananchi rsaid@mwananchi.co.tz

Tanga. Shule mbili na vyuo viwili vinavyomilikiwa na Taasisi ya Elimu ya Eckernforde ya jijini hapa vimefungiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga kwa kile kilichoelezwa kuwa zinadaiwa kodi za mwaka 2012 hadi 2016.

Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Masawa Masatu alisema mamlaka ya mapato imezifungia shule hizo pamoja na Chuo cha Eckenforde kwa kushindwa kulipa kodi kwa muda mrefu.

Meneja huyo alisema endapo watashindwa kulipa kodi mali zote za taasisi hiyo zitazitaifishwa na Serikali.

Hata hivyo, meneja huyo hakutaja kiasi cha fedha kinachodaiwa huku akitaja majengo ya taasisi hiyo yaliyofungiwa kuwa shule za msingi, sekondari, chuo kikuu na chuo cha ualimu.

Alisema kufungiwa kwa taasisi hiyo ni mwendelezo wa mamlaka hiyo kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Eckernforde Profesa John Kiango alisema wameshindwa kulipa kodi kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi hivyo kwa sasa mikakati yao ni kuhakikisha wanaongeza idadi kubwa ya wanafunzi jambo litakalowaongezea kipato kitakachowasaidia kulipa kodi kwa wakati.

Thursday, October 26, 2017

H’shauri yatenga Sh19 mil kununua miche ya kahawa

 

By Charles Lyimo,Mwananchi clyimo@mwananchi.co.tz

Moshi. Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro imetenga Sh19 milioni kwa ajili ya kununua miche ya kahawa kwa kipindi cha mwaka 2017/18 katika Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI).

Ofisa kilimo wa halmashauri hiyo, Chikira Mcharo alisema fedha hizo zitasaidia kununua miche zaidi ya 63,000 aina ya vikonyo.

“Mwaka 2016/17 tulitenga Sh15.5 milioni na tulinunua miche 42,000,” alisema Mcharo.

Alifafanua kuwa kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 Sh7.5 milioni zilitengwa kwa ajili ya kukarabati vituo vya kuuzia kahawa.

“Pia, tumeweza kukarabati mifereji ya maji 49 kati ya 200 iliyopo kwa kipindi cha mwaka 2014/17,” alisema.

Mratibu wa zao hilo katika halmashauri hiyo, Violeth Kisanga aliwataka wakulima wa zao hilo kuachana na kilimo cha zamani cha kahawa aina ya KP 423 na badala yake walime kahawa ya vikonyo kutoka TaCRI.

“Kahawa ya zamani inashambuliwa sana na magonjwa, ila hii ya vikonyo haishambuliwi sana na huzaa kwa wingi, huu ni wakati wa mkulima kubadilika ili anufaike na shamba na kahawa basi alime kahawa ya vikonyo,” alisema Kisanga.

Kuhusu mbolea ya DAP, Kisanga alisema baada ya Serikali kuona gharama ya uuzwaji wake ipo juu iliziagiza mamlaka husika kushusha bei.

Alisema tangu mwaka 2016/2017 mbolea hiyo imekuwa ikiuzwa kwa Sh51,924 kwa mfuko wa kilo 50 badala ya Sh70,000 ya awali.

Wajumbe wa Bodi ya Muungano wa Vyama vya Ushirika Uru Kaskazini ambao pia ni wakulima wa zao hilo, Felix Masao na Proti Mauki waliiomba halmashauri kuwasaidia wakulima pembejeo ikiwamo dawa kwa bei nafuu.

Tuesday, October 24, 2017

Azania kuwasitiri kwa mikopo wanachama wa NSSF nchini

Mkurugenzi mtendaji wa Azania benki, Charles

Mkurugenzi mtendaji wa Azania benki, Charles Itembe 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchi@mwananchi.co.tz

Arusha. Benki ya Azania kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), itaanza kutoa mikopo kwa wanachama wa mfuko huo ili kuboresha maisha na kuhamasisha matumizi ya huduma fedha nchini.

Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Charles Itembe alisema licha ya mikopo inayotolewa kwa mwanachama kwa udhamini wa mwajiri, pia itatolewa kwa vyama vya akiba na mikopo (Saccos).

“Tumetenga Sh50 bilioni kuzikopesha Saccos zilizopo na zitakazoanzishwa maeneo ya kazi,” alisema Itembe.

Licha ya Saccos zilizopo maeneo ya kazi, Itembe alisema ipo programu inayozihusisha za hiari ambayo itamwezesha mwanachama kupata mkopo hadi wa Sh20 milioni.

“Huu ni mpango wa majaribio iwapo utafanikiwa tutaupa kipaumbele,” alisema.

Benki hiyo inamilikiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa asilimia 98. Benki ya Maendeleo Afrika Mashariki (EADB) kwa asilimia 1.5 na wanahisa wengine 48 wakimiliki asilimia moja.

Mpaka Juni mwaka jana, mifuko hiyo ilikuwa na jumla ya wanachama milioni 2.23 ambao michango yao ilikuwa Sh2.15 trilioni huku wastaafu 126,358.

Naye Meneja mwandamizi wa huduma za rejareja wa Azania, Jacskon Lohay aliwataka Watanzania na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kuchangamkia mikopo hiyo na huduma nyingine wanazotoa.

Tuesday, October 24, 2017

Mikopo sekta binafsi yaporomoka mwaka wa fedha ukianza

Dar es Salaam. Licha ya mapato ya Serikali kuongezeka ndani ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha, mikopo ya sekta binafsi imeendelea kusuasua.

Wakati taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zikionyesha kuongezeka kwa makusanyo tangu Julai mpaka Septemba, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwaka ulioishia Julai inaonyesha iliongezeka kwa asilimia moja pekee.

Ripoti ya Agosti ya BoT inayoonyesha mwenendo wa mikopo ya benki za biashara kwenda sekta binafsi, ilipungua ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 15.2 uliokuwapo kipindi kama hicho mwaka jana.

“Kupungua kwa mikopo hiyo, kulitokana na tahadhari zilizochukuliwa na benki za biashara kukichangiwa na kupungua kwa rasilimali zake na amana za wateja,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti inafafanua kuwa sekta nafuu kidogo inajidhihirisha kwenye ujenzi na ukandarasi, hoteli na mighahawa ambazo ziliimarika.

Ripoti inaonyesha baada ya Juni kupungua kwa asilimia 22.1, mikopo ya sekta ya uchukuzi na mawasiliano kwa Julai ilishuka kwa asilimia 25.

Pia, hali kama hiyo ilijionyesha kwenye kilimo ambacho kwa Julai mikopo yake ilipungua kwa asilimia 9.4, baada ya kupungua kwa asilimia 0.2 Juni.

Baada ya kupungua kwa asilimi 5.8 Juni mwaka jana, mikopo binafsi iliongezeka kwa asilimia 8.3 wakati ile ya hoteli na migahawa ikiongezeka kwa asilimia 24.4, baada ya kukua kwa asilimia 7.9 Juni.

Ukuaji ujenzi, ukandarasi

Ujenzi na ukandarasi nayo ilikua kwa asilimia 16.7 Julai baada ya kufanya hivyo kwa asilimia 5.5 Juni.

“Mikopo ya biashara ilikuwa mingi zaidi, asilimia 20 ikifuatiwa na binafsi kwa asilimia 19.7,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Hata mwaka ulioishia Juni kwa ujumla, mikopo ya ndani iliyotolewa kwa sekta binafsi na umma ilipungua kwa Sh887.1 bilioni ikilinganishwa na ongezeko la Sh4.192 trilioni kwa mwaka ulioishia Juni 2016.

Hata hivyo, mwaka ulioishia Julai, BoT inasema mikopo ya Serikali kutoka benki za biashara iliongezeka kwa Sh1.246 trilioni.

Tuesday, October 24, 2017

Serikali yaifutia TTCL deni la Sh76 bilioni

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi asimtowe@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati kampuni zote zikitakiwa kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Serikali imeifutia deni la Sh76 bilioni Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kuligeuza mtaji ili iweze kuimarisha uwezo na kutekeleza majukumu yake kwa ushindani.

Kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 5(3) na 9 cha Sheria ya Fedha, Waziri wa fedha na mipango, Dk Philip Mpango alibadilisha deni hilo kuwa mtaji Agosti.

Taarifa iliyotolewa na Msajili wa Hazina, Dk Oswald Mashindano inasema lengo la kugeuza mkopo huo kuwa mtaji ni kuitaka TTCL kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, tija na weledi ili kuongeza ushindani katika soko.

Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoca) ya mwaka 2010 inazitaka kampuni zote za mawasiliano kujiorodhesha DSE. Mwisho wa kufanya hivyo ilikuwa Juni, lakini ni Vodacom pekee iliyokamilisha agizo hilo huku nyingine zikiwa bado.