Wednesday, July 4, 2018

TBA yaijaza Hazina mabilioniMtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga

Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga 

By Kalunde Jamal , Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wametoa gawiwo la Sh2 bilioni ikiwa ni asilimia 15 ya mapato yao  ambayo wameelekezwa kuirudishia Hazina.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la TBA kwenye maonyesho ya 42 ya biashara ya kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga alisema fedha hizo ni za mwaka wa fedha uliomalizika Juni 30.

Amefafanua kuwa gawiwo hilo limetokana na utendaji kazi wa viwango vizuri na unaoaminika.

Amesema anajivunia kuwa na rasilimali ya watu iliyo bora ikiwamo wataalamu 83, wahandisi 73 na watafiti wa majengo 65.

"Cha kujivunia wataalamu wote hawa ni kutoka hapa nchini hakuna hata mmoja kutoka nje, baadhi yao walipata ujuzi nje ya nchi lakini wanafanya kazi hapa ndani,"amesema Mwakalinga.

Ameeleza kuwa wamepunguza gharama za ujenzi kwa kununua vifaa vyao vya kisasa ikiwamo magari, mashine ya kuchanganya zege na magari ya kusafirishia zege.

Ameitaja changamoto wanayokutana nayo kwenye utendaji wao kuwa ni hali ya hewa isiyotabirika. "Kwa mfano mradi wa Mloganzila, tulipouanza tu mvua zikaanza kunyesha.

Amesema hilo ndilo jambo linalowapa changamoto kwa sababu mradi inabidi usimame na kuanza kutoa matope.

Wednesday, July 4, 2018

Waziri Mkuu azindua maonyesho ya Sabasaba

 

By Jackline Masinde na Kalunde Jamal, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua rasmi maonyesho ya biashara ya kimataifa, maarufu Sabasaba huku akiwataka wafanyabiashara nchini  kutumia fursa hiyo ili kutangaza bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini.

Majaliwa ameyasema hayo leo  Julai 4  na kuwakumbusha wafanyabiashara kuwa kuna maonyesho ya  karne ya 21 yatakayofanyika  China Septemba mwaka huu.

"Naomba maonyesho haya watanzania tushiriki kwa wingi na siyo haya tu maonyesho yoyote yale yanayofanyika nchi mbalimbali tunapaswa kushiriki ili kutangaza bidhaa zetu na  kukuza soko la bidhaa za Tanzania,"amesema.

Pia amewataka Wafanyabiashara waliotoka mataifa mbalimbali hapa nchini kuendelea kuja kuonyesha bidhaa zao ili watanzanai wajifunze pia kupitia kazi zao na wao wajifunze vitu vinavyotengenezwa na watanzanaia.

Pia amewataka wafanyabiashara kutumia maonyesho ya sababsa kuwa sehemu ya kutafuta fursa kutoka nje ya nchini.

 

Wednesday, July 4, 2018

Waziri Mwijage asema maonyesho ya Sabasaba yamekidhi viwango

 

By Jackline Masinde,Mwananchi jmasinde@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amesema maonyesho ya 42 ya Kimataifa ya Wafanyabiashara yamekidhi viwango  vya DITF kwani yamewahusisha Wafanyabiashara wazawa  na wa kimataifa.

Ameyasema hayo leo Julai 4  wakati akimkaribisha mgeni rasmi katika maonyesho hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa hotuba yake.

Mwijage amesema  maonyesho hayo yamehudhuriwa na wafanyabiashara wa ndani 2900 na a nje 2500 na nchi 33.

"Maonyesho haya yamekidhi viwango vya Maonyesho ya Kimataifa ya Wafanyabiashara (DITF) na walioshiriki maonyesho hayo wanaonyesha bidhaa ambazo zimetengenezwa hapa nchini kupitia iwanda vyetu" amesema.

Wednesday, July 4, 2018

TBA yajisifu kuokoa Sh98 bilioni miradi yake saba

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeokoa Sh 398 bilioni katika miradi saba iliyotekelezwa nchini katika mwaka wa fedha 2017/18.

Katika kipindi hicho pia TBA imepeleka gawiwo serikalini la Sh2 bilion, sawa na asilimia 15 ya mapato hayo.

Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga ameyasema hayo leo katika Maonyesho ya kimataifa ya biashara(Sabasaba) yanayoendelea jijini hapa.

Mwakalinga ameiitaja miradi hiyo saba  kuwa ni pamoja na wa Chuo Kikuu cha Dar es Salam uliogharimu Sh10bilioni badala ya Sh100bilioni  zilizopangwa hapo awali, ujenzi wa Ihungo uliogharimu Sh 12 bilioni  badala ya Sh108bilioni  na mradi wa ujenzi wa hospitali ya Geita uliojengwa kwa Sh17bilioni badala ya Sh 75 bilioni.

Aliutaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa Hospitali ya Simiyu uliojengwa kwa gharama ya Sh12 badala ya sh47 bilioni.

Mwingine ni ujenzi wa hospitali ya Chato uliogharimu Sh13 bilioni badala ya 60, mradi wa nyumba za Magomeni uliogharimu Sh20bilioni badala ya Sh 86 bilioni, mradi wa Ukonga Sh10 badala ya 32.

“Wataalam wote hawa ni Watanzania,pia tunajivunia kwa kuwa na mitambo na vifaa  mbalimbali vya kisasa,pamoja na mtambo wa kuzalisha zege kwa mkoa wa Dodoma," amesema.

Wednesday, June 27, 2018

Finca yawatangazia bingo wenye wazo bora la biashara

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Benki ya Finca Microfinance imezindua programu ya kuwaongezea uwezo wajasiriamali wadogo kwa kuwapa stadi za biashara.

Pamoja na maarifa hayo, benki hiyo itatoa Sh10 milioni kwa wazo bora la biashara litakalowasilishwa na wajasiriamali hao.  

Mkuu wa idara ya masoko na mawasiliano wa benki hiyo, Nicholous John alisema programu hiyo ya miezi minne itafanyika kwa wateja wa jijini Dar es Salaam, kabla ya utaratibu wa kuipeleka mikoani.

Amesema mtu atakayekuwa na wazo bora zaidi atawezeshwa kifedha kuendeleza biashara ndogondogo.

"Shindano hili litashirikisha wateja wenye akaunti Finca na wanaopenda kushiriki watatakiwa kufungua kwa kuweka Sh20,000,” amesema.

Amesema washiriki watapaswa kujaza fomu zilizopo kwenye matawi wakibainisha watakachofanyia fedha watakazoshinda iwapo wataibuka  washindi. 

Miongoni mwa washiriki watakaojitokeza, amesema wanane watachaguliwa na jopo la majaji kushiriki katika kipindi cha runinga cha ‘kuza ofisi na Finca.’

“Mwishoni mwa shindano, mshindi mmoja ataondoka na zawadi nono ya zaidi ya Sh10 milioni," amesema.

Ofisa mkuu wa biashara wa benki hiyo, Emmanuel Mongella amesema programu hiyo ni sehemu ya kusherehekea miaka 20 ya Finca nchini.

Saturday, June 23, 2018

Wewe ni mtumiaji wa simu? Unafahamu ni asilimia ngapi ya watu duniani wanatumia simu? Vipi kuhusu mtandao?

 

Wewe ni mtumiaji wa simu? Unafahamu ni asilimia ngapi ya watu duniani wanatumia simu? Vipi kuhusu mtandao?  Huenda hufahamu upo kwenye kundi gani la watumiaji, tumia dakika mbili  tu kusoma hapa ili ufahamu yote hayo.

Friday, June 22, 2018

Zitto azidi kupigilia msumari ushuru wa korosho

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe akizungumza

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Ibrahim Yamola, Mwananchi iyamola@mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema Serikali inapaswa kuwa makini na zao la korosho kwa maelezo kuwa kitendo inachotaka kufanya cha kuchukua asilimia 65 ya fedha za mauzo ya korosho nje ya nchi, ni hatari.

 

Akizungumza katika mjadala wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 leo Ijumaa Juni 22, 2018 bungeni mjini Dodoma, amesema  mfumo wa Bunge ni mfumo wa Kamati, kwamba kamati za chombo hicho cha Dola, zinafanya kazi kwa niaba ya wabunge wote.

 

Tayari baadhi ya wabunge wametishia kufanya maandamano iwapo Serikali haitatoa asilimia 65 ya ushuru wa mauzo ya korosho nje kwa ajili ya maendeleo ya zao hilo.

 

Pia, wabunge wamepinga mabadiliko ya Sheria ya Korosho yanayokusudiwa kufanywa na Serikali ili ushuru huo upelekwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina.

 

Akizungumzia jambo hilo ambalo kamati ya Bunge ya Bajeti ililipinga katika maoni yake kuhusu bajeti ya Serikali mwaka 2018/19, iliyoyawasilisha bungeni Juni 18, 2018, Zitto amesema ni vyema jambo ambalo wabunge wanakuwa na mashaka nalo, likafanyiwa kazi.

 

“Leo ukija bungeni uwapinga wabunge wanaolima korosho, kesho utakuwa na jambo lako utakosa wa kukuunga mkono na busara ni kukaa kimya,” amesema Zitto na kubainisha kuwa korosho na mazao mengine kama pamba na kahawa yamesaidia kuongeza pato la kigeni kwa Taifa.

 

 

Saturday, June 16, 2018

Sababu tano kwa nini uchague mtandao wa Telegram

 

Karibu kila mwenye ‘smartphone’ anatumia ‘application’ ya WhatsApp. Hii inatajwa kuwa programu ya mawasiliano kwa njia sauti, video na ujumbe wa maandishi yenye watumiaji wengi zaidi duniani.

Lakini zifuatazo ni faida tano za kukufanya uuchague mtandao wa Telegram ambazo huwezi kuzipata kwingine.

Uhifadhi wa mtandaoni

Telegram huhifadhi vitu mtandaoni na si kwenye simu

Tuma faili la ukubwa hata wa GB 1.5

Kwa watu wanaotumia WhatsApp wanafahamu kwamba huwezi kutuma faili lenye ukubwa wa kuzidi MB 16 kupitia mtandao huo.

 

Mawasiliano ya siri

Hii ni aina ya kutumiana meseji ambayo watumiaji wanakuwa wanaweka muda wa kufutika kwa mesjei zao, na muda unapofikia, meseji hujifuta zenyewe, na zinapofutika, hakuna namna ya kuziona tena.

 

Kundi la wanachama hadi 5,000

Kwa njia ya kawaida, kundi la WhatsApps linaweza kubeba wanakikundi 256 tu. Wakati kwenye Telegram, kundi lina uwezo wa kuwa na idadi ya wanachama hadi 5,000 na zaidi katika Super Groups.

 

Kujisajili bila namba

Kama ambavyo ni lazima kujisajili kwa kutumia nambari ya simu kwenye WhatsApp, ndivyo unavyoweza kujisali kwenye Telegarm pia.

 

 

 

Friday, June 15, 2018

Bajeti EAC zajikita kuibeba sekta ya kilimo

Waziri wa Fedha wa Rwanda, Dk Uzziel

Waziri wa Fedha wa Rwanda, Dk Uzziel Ndagijiman 

EAC. Jana macho na masikio ya wananchi yalikuwa kwa mawaziri wa fedha wa nchi za Afrika Mashariki ambao walikuwa gumzo kila kona ya nchi zao wakisubiriwa kwa hamu kusoma bajeti kuu ya mwaka 2018/2019.

Nchi hizo ambazo zimeweza kusoma bajeti hiyo ni pamoja na Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda.

Kwa nchi zote hizo sekta ya kilimo imepewa kipaumbele katika bajeti hiyo.

Mbali ya sekta hiyo, pia sekta zingine ambazo zilipewa kipaumbele ni pamoja na afya na elimu.

Hatua hiyo ni baada ya kila wizara kuwakilisha makadirio ya matumizi na mapato huku ikiibuka mijadala mizito ambayo wakati fulani ilisababisha mvutano kwa wabunge wa nchi hizo.

Nchini Kenya bajeti hiyo ilisomwa saa tisa alasiri na Waziri wa Fedha, Henry Rotich ambayo kwa jumla ilikuwa ni ya Sh66 trilioni (Ksh3 trilioni).

Bajeti ya Kenya ilijikita zaidi kwenye ajira na kilimo.

Mwaka jana, Waziri Rotich aliondoa kodi ya mahindi yanayoagizwa kutoka nje ili kurahisisha uagiza wa bidhaa hiyo. Pia aliondoa kodi ya utengezaji wa dawa za kuua wadudu na magari ya utalii yanayotengenezwa nchini Kenya.

Kama moja ya njia ya kuzuia uchezaji kamari, Serikali iliongezea kodi ya sekta hiyo hadi asilimia 50 kutoka asilimia 7.5.

Kadhalika, Uganda nako Waziri wa Fedha, Matia Kasaija alitangaza bajeti akitenga Sh16 trilioni (Ush32.7 trilioni), huku vipaumbele vikielekezekwa kwenye sekta za utalii, miundombinu, elimu, michezo, afya, ulinzi na kilimo.

Waziri wa Fedha wa Rwanda, Dk Uzziel Ndagijiman alitaja vipaumbele vya bajeti ya nchi hiyo akidai itajikita kwenye kilimo na viwanda.

Alisema bajeti imeongezeka kwa asilimia 16 ikilinganishwa na iliyopita ya mwaka 2017/2018.

Waziri huyo alisema bajeti kuu ya mwaka huu wa fedha itakuwa Sh6 trilioni (Rwf2.4 trilioni).

Alisema bajeti hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Julai Mosi imelenga kuinua uchumi.

Dk Ndagijiman alisema uchumi wa Rwanda unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.2.

Thursday, June 14, 2018

Tirdo sasa yatakiwa kufanya kazi saa 24

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara,

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Elisante Ole Gabriel. 

By Hadija Jumanne, Mwananchi hjumanne@mwananchi.co.tz

Mapinduzi ya viwanda hayajaanzia katika mitambo, bali yanaanzia katika fikra za watu

Dar es Salam. Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Elisante Ole Gabriel, amelitaka Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda nchini (Tirdo), kufanya kazi usiku na mchana ili wadau wa biashara na viwanda wapate huduma wakati wote.

Profesa Ole Gabriel alisema hayo alipotembelea shirika hilo na kuongeza kuwa ili wafanyabiashara na wawekezaji wa sekta ya viwanda waweze kupata huduma muda wowote, ni lazima Tirdo wafanye kazi usiku na mchana.

“Tunahitaji sana utafiti wenu. Kutokana na umuhimu huo, nawaomba mfanye kazi saa 24 kwa siku saba za wiki, ikiwezekana Profesa Mtambo (Mkumbukwa) muweke zamu kwa wafanyakazi ili wadau wetu wa viwanda na biashara waweze kupata huduma wanapohitaji.

“Mapinduzi ya viwanda hayajaanzia katika mitambo, bali yanaanzia katika fikra za watu, kwa kubuni shughuli zitakazowaingizia kipato, lakini tumeona Tirdo inaisaidia sana Serikali kujua ni eneo gani tunatakiwa kuanzisha kiwanda kulingana na eneo husika,” alisema Profesa Ole Gabriel.

Alibainisha kuwa mikakati ya wizara kwa sasa ni kuhakikisha inaunganisha mnyororo wa thamani wa kilimo na viwanda.

Mkurugenzi Mkuu wa Tirdo, Profesa Mkumbukwa Mtambo alisema silaha kubwa ya ushindani katika uchumi wa viwanda na biashara ni kutumia taasisi zinazofanya utafiti kuhusu maendeleo ya viwanda.

Profesa Mtambo pia alisema kwamba kupitia fedha za maendeleo walizopewa, Sh100 milioni zimetumika kununua mashine ya kisasa ya kupima sumu kuvu na kuangalia usalama wa chakula.

Awali, Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Tirdo, Dk Anselm Mosha alisema kwamba mashine hiyo itakuwa na uwezo wa kupima sumu kuvu kwenye vyakula vya nafaka kama, mahindi, karanga, ufuta, makopa ya mihogo na matunda.

“Pia, mashine hii inapima masalia ya viuatilifu katika mazao mbalimbali, hasa ya mbogamboga na matunda, lakini pia masalia ya sumu za dawa zinazotoka kwenye nyama na maziwa,” alisema Dk Moshi.

-->