Kutokuwa na siri kulivyoitesa CCM Uchaguzi Mkuu wa 2015

Muktasari:

Lubinga amesema hakuna mfumo wowote duniani usiojengwa kwa usiri. 

Dar es salaam. Katibu wa NEC ya CCM, Siasa na Mahusiano ya Kimataifa, Ngemela Lubinga amesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 uliyumba na ulikuwa mgumu kwa sababu baadhi ya wanachama na viongozi hawakuwa wakitunza siri.

Amesema, "Umakini kwenye kutekeleza majukumu ni umakini kwenye kutunza siri, uchaguzi wa 2015 uliyumba na ulikuwa mgumu kwa sababu baadhi yetu hatukuwa na siri. Hatuwezi kujenga jamii yenye usiri kama viongozi tusipokuwa wasiri."

Amesema kutunza siri kutawaongezea heshima wanachama na viongozi wa CCM. Ngemela amesema hayo leo Jumatano, Oktoba 18, 2017 jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa baraza kuu la Jumuiya ya Wazazi Taifa ya CCM. Amesema hakuna mfumo wowote duniani usiojengwa kwa usiri.

Lubinga amesema hatua ya baadhi ya wanachama na wajumbe kutokuwa na siri inawashushia heshima wao wenyewe na kukibomoa chama hicho.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo anayemaliza muda wake, Abdallah Bulembo amesema haikuwa rahisi kumaliza miaka mitano ya uongozi wake.

"Ilikuwa ni miaka ya misukosuko, tumepita katika milima na mabonde lakini tunatembea kifua mbele kwamba tumesaidia kukiimarisha chama chetu," amesema.

Takriban nusu ya wajumbe wa baraza hilo linalokutana kupitia majina ya walioomba kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya jumuiya hiyo walitoka ndani ya ukumbi kutokana na kuomba tena nafasi ya kugombea.