Waziri wa Ireland azungumzia umuhimu wa vyombo huru vya habari

Waziri anayeshughulikia diaspora na maendeleo ya kimataifa wa Jamhuri ya Ireland, Ciaran Cannon     

Muktasari:

  • Cannon aliyetembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) jana mchana, alisema kwa kutumia uzoefu wa Ireland vyombo vya habari vilivyo huru na vyenye nguvu si tu ni chachu ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi, bali ni muhimu katika kuchochea maendeleo.

Dar es Salaam. Waziri anayeshughulikia diaspora na maendeleo ya kimataifa wa Jamhuri ya Ireland, Ciaran Cannon ameshauri uwekezaji katika vyombo huru vya habari na vyenye weledi ili kuchochea ukuaji wa demokrasia na maendeleo.

Cannon aliyetembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) jana mchana, alisema kwa kutumia uzoefu wa Ireland vyombo vya habari vilivyo huru na vyenye nguvu si tu ni chachu ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi, bali ni muhimu katika kuchochea maendeleo.

MCL inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na mtandaoni kupitia MCL Digital.

“Vyombo vya habari makini na huru vina mchango mkubwa katika kuhakikisha uwajibikaji, uwazi na kuboresha misingi mingine ya demokrasia kwa kuibua mijadala kwa jamii inayosadia kulijenga Taifa,” alisema.

Cannon alisema Serikali ya Ireland inayo furaha kuunga mkono vyombo vya habari huru, imara na vinavyofuata weledi katika shughuli zake ili kuimarisha misingi ya demokrasia.

Ili kuhakikisha uhuru wa habari unaongezeka nchini mwao, alisema hivi karibuni Serikali ilipitisha sheria ya haki ya kupata habari ambayo inamruhusu kila mwananchi kuomba taarifa anayoitaka kutoka serikalini jambo linalochochea habari za uchunguzi. “Uhuru wa habari ni moja ya mambo ambayo watu wanataka. Kwetu ukisema uminye tu uhuru huo wananchi watakugeukia vikali,” alisema.

Cannon ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku nne alielezea furaha yake ya kusikia moja kwa moja kutoka kwa menejimenti, waandishi na wahariri wa MCL jinsi wanavyotekeleza shughuli zao na kuvutiwa na namna chombo hicho cha habari kilivyoimarisha madawati ya habari za uchunguzi na takwimu.

Waandishi wa MCL ni miongoni mwa waliowahi kunufaika na ufadhili wa Serikali ya watu wa Ireland katika mafunzo ya umahiri wa habari kupitia Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).

Katika ziara yake hiyo ya siku nne, Cannon atapata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi kutoka serikalini, asasi za kiraia na vyombo vya habari.

Awali, mkurugenzi mtendaji wa MCL, Francis Nanai alimweleza waziri huyo kuwa uhuru wa habari ni nguzo muhimu ambayo kampuni hiyo inazingatia kuhakikisha inatimiza majukumu yake kwa weledi.

“Siku zote Mwananchi Communications ni sauti ya wasiokuwa na sauti,” alisema Nanai na kusisitiza kuwa kwa sasa uwekezaji mkubwa unafanywa kwenye masuala ya uandishi wa habari kidigitali.

Pia, Nanai alizungumzia uwapo wa sheria mpya zinazoviweka vyombo vya habari katika wakati mgumu kwenye utekelezaji wa majukumu yao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya MCL, Leonard Mususa alisema kutokana na mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea katika tasnia ya habari, kampuni hiyo inawekeza katika kuandaa waandishi mahiri licha ya kuwapo changamoto za rasilimali.

“Katika kipindi hiki cha digitali tunahitaji kusimama kikamilifu na kuwa chanzo cha kuaminika cha habari. Hilo ndiyo jambo tunalolitilia mkazo,” alisema Mususa.