Mganga mkuu ataja sababu za kushuka maambukizi ya malaria

Muktasari:

  • Wakati maambukizi ya ugonjwa huo ulikuwa asilimia 19.1 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12, kiwango hicho kimeshuka hadi asilimia 15.1 mwaka wa fedha wa 2015/16.

Kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kimeshuka kwa asilimia nne mkoani Mwanza katika kipindi cha mwaka miaka sita iliyopita.

Wakati maambukizi ya ugonjwa huo ulikuwa asilimia 19.1 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12, kiwango hicho kimeshuka hadi asilimia 15.1 mwaka wa fedha wa 2015/16.

Hayo yalielezwa juzi na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Leonard Subi wakati wa zoezi la ugawaji wa vyandarua vyenye dawa kwa wanafunzi wa shule ya msingi Sese wilayani Magu.

Pamoja na matumizi ya vyandarua, Dk Subi alitaja unyunyuziaji wa dawa ya ukoko majumbani kuwa ni mbinu nyingine iliyotumika kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.

Zaidi ya kaya 200, 000 kutoka wilaya za Sengerema na kwimba zimepata huduma ya kunyunyuziwa dawa ya ukoko majumbani.

Jumla ya vyandarua 5, 919 tayari vimegawanywa kwa wananchi mkoani Mwanza kupitia zoezi la ugawaji vyandarua katika shule za msingi na vituo vya afya.

Mshauri Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Chris Thomas aliyehudhuria hafla ya ugawaji vyandarua kwa wanafunzi aliahidi kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania kupambana na ugonjwa wa Malaria.

Naye Mratibu wa Malaria Mkoa wa Mwanza, Saula Baichumila alisema licha ya juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo, mkoa wa Mwanza bado unashuhudia vifo vitokanavyo na Malaria kutokana na watu 235 kupoteza maisha baada ya kuugua Malaria ndani ya kipindi cha miezi sita kati ya Januari hadi Juni, mwaka huu.

Akizungumza kwa kwa niaba ya Jumuiya ya shule, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi ya Sese, Jeremiah Masungasimbi alisema tangu shule hiyo ilipoingizwa kwenye mpango wa mradi wa kudhibiti malaria, mahudhurio ya wanafunzi umeongezeka kutokana na kupungua kwa magonjwa ya mara kwa mara kulinganisha na kipindi cha nyuma.