Tanesco yasogeza huduma kwa wateja mkoani Kilimanjaro

Muktasari:

Waziri wa Nishati ameagiza mameneja wa mikoa wa Tanesco kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja katika ofisi zote za wilaya na mikoa.

Mwanga. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limeanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nishati, Medard Kalemani la kuwa na vituo vya huduma kwa wateja katika maeneo mbalimbali ili kuwafikia wateja wengi.

Hivi karibuni akiwa wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro kuzindua mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dk Kalemani aliwaagiza mameneja wa mikoa wa Tanesco kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja katika ofisi zote za wilaya na mikoa nchini.

Katika kutekeleza agizo hilo, Meneja Mwandamizi wa Tanesco Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Stela Hiza ameongoza timu ya watumishi wa shirika hilo mkoa kufungua ofisi ndogo tatu katika wilaya za Same na Mwanga.

Hiza amesema kutokana na adha iliyokuwa ikiwakabili wateja ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo, shirika limewasogezea ofisi karibu.

“Tumelenga kufungua ofisi ndogo tisa katika maeneo ya wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro, tumeanza na tatu katika Kata za Hedaru, Kisiwani na Spillway iliyopo Nyumba ya Mungu wilayani Mwanga,” amesema.

Amesema katika vituo hivyo vitatu, wanatarajia kutoa huduma kwa wakazi zaidi ya 18,000.

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kilimanjaro, Mahawa Mkaka amesema lengo la kuanzishwa madawati ya huduma kwa wateja na ofisi ndogo ni kuwasaidia wateja lakini pia kuwawezesha kutoa taarifa za watu ambao wanahujumu miundombinu ya shirika hilo.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Kilimanjaro, Samuel Mandari amesema kufunguliwa kwa ofisi hizo kutasaidia kusogeza huduma karibu na jamii.

“Tunatarajia  wateja wetu sasa hawatapata usumbufu tena wa kusafiri umbali mrefu wakitafuta huduma hii, tunawaomba wazitumie ofisi hizi,” amesema.