Spika Ndugai alivyogeuka mwiba kwa wabunge CCM, mawaziri

Spika Job Ndugai

Dodoma. Imezoeleka kuona Spika Job Ndugai ‘akiwakoromea’ wabunge wa upinzani, lakini katika mkutano wa tisa wa Bunge uliomalizika jana amegeuka ‘msumari’ kwa mawaziri, wabunge wa CCM na Serikali.

Maagizo mbalimbali yaliyotolewa na Spika Ndugai, kuwaonya wabunge wa CCM na kuwakaanga mawaziri kulionekana kurudisha makali kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Mbali na Spika, pia wabunge watatu wa CCM; Hussein Bashe wa Nzega Mjini, Peter Sekuramba wa Kigoma Kaskazini na Nape Nnauye wa Mtama nao walikuwa msumari kwa mawaziri kutokana na hoja zao wakati wakichangia bungeni.

Ukiacha michango mbalimbali ya wabunge, kauli za Spika Ndugai alipokuwa akitoa maelekezo na miongozo kwa wabunge na mawaziri ni sehemu iliyolifanya Bunge liwe moto na kuchangamka.

Kauli ya kwanza ya Spika ni alipowataka wabunge wa CCM kufunguka na kuchangia kwa uhuru ili kuisaidia Serikali badala ya kupongeza zaidi na baadaye kukaa.

“Katiba iliweka utaratibu kwamba mipango ya nchi itapita hapa kwanza nyinyi muijadili. Halikuwekwa hivyo kwa bahati mbaya. Liliwekwa hivyo ili nyinyi mseme kwa niaba ya wananchi,” alisema Spika

“Katika mambo ya msingi kama haya fungukeni. Msijifungefunge hapo ooh mimi CCM. CCM haitaki mipango mibovu. Ni wakati wenu wa kusema tumsaidie waziri na tuisaidie Serikali ili tusonge mbele.”

Huku akipigiwa makofi na wabunge wa upinzani na CCM, Ndugai alisema: “Na unapoomba nafasi ya kusema hapa uwe umejiandaa. Sio ile tu naunga mkono, nafanya hivi, unakaa chini.”

Spika hakuishia kwa wabunge wa CCM bali alienda hadi kwa mawaziri ‘akiwakoromea’ na kuwataka kuacha kupiga stori bungeni na kushindwa kusikiliza maswali yanayoulizwa na wabunge huku mwisho wake ukiwa ni kutoelewa kilichoulizwa.

Onyo hilo alilitoa wakati wa kipindi cha maswali na majibu baada ya kuwataja baadhi ya manaibu mawaziri ili wajibu maswali, lakini walishindwa kusimama kwa kuonyesha hawakusikiliza kilichokuwa kimeulizwa. “Waheshimiwa mawaziri acheni kupiga stori ndani ya Bunge, ndiyo maana mnashindwa kusikiliza kinachoendelea humu, hebu punguzeni na mjikite katika kusikiliza,” alisema Ndugai.

Lakini kubwa zaidi ni pale alipoitaka Serikali iutazame muswada wa kuanzisha Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (Nasac), akisema kifungu kinampa madaraka makubwa mkurugenzi mkuu na hakifai.

Spika alisema kama kifungu hicho kingeachwa kama kilivyo, wabunge walikuwa wanatengeneza udikteta bila kujitambua, lakini Serikali baadaye ikasema kutakuwa na kamati ya kumshauri.

Kifungu hicho kilikuwa kikimpa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo madaraka makubwa ya kutoa leseni kwa mawakala na kufuta leseni, hali ambayo iliibua wasiwasi wa kutumia vibaya madaraka.

Bashe, Serukamba na Nape

Kati ya wabunge wa CCM waliochangia kwa hisia kali ni Bashe, Serukamba na Nape.

Michango yao ambayo kwa sehemu kubwa iliikosoa Serikali kuhusiana na ushiriki wa sekta binafsi, kukua kwa uchumi na kuongezeka Deni la Taifa ilimfikia hadi Rais John Magufuli.

Ni michango hiyo ambayo ilimfanya Rais Magufuli kupitia kwa waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwatumia salamu Nape na Bashe akiwaambia hajakataa wawekezaji binafsi.

Siri hiyo ilifichuliwa na Dk Mpango wakati akihitimisha majadiliano ya mpango huo ambao baadhi ya wabunge waliuchangia kwa kuukosoa kwa kuiacha sekta binafsi.

“Naomba ninong’one na Bunge lako tukufu. Mheshimiwa Rais Magufuli aliposikia huu mjadala, alinipigia simu na aliniambia hivi,” alisema Dk Mpango na kuendelea akimnukuu Rais. 

“Waziri, mwambie ndugu yako mheshimiwa Nape na mheshimiwa Bashe kuwa nawataka sana hao wawekezaji kwenye ujenzi wa standard gauge railway (reli ya kisasa).

“Wawalete hata kesho niko tayari kuwapa reli ya kutoka Kaliua –Mpanda au Isaka-Mwanza au reli ya Mtwara-Mchuchuma hadi Liganga waijenge.”

“Hayo ni maneno ya mheshimiwa Rais, natumaini waheshimiwa husika will raise up to this challenge from his excellence the president (wataifanyia kazi changamoto ya mheshimiwa Rais,” alisema.

Awali akichangia bungeni, Nape alisema miradi mikubwa ya Serikali itakayotekelezwa italipaisha deni la Taifa hadi Sh103 trilioni.

Alisema kwa sasa deni hilo limesimama katika Dola26 bilioni (sawa na Sh56 trilioni), lakini miradi mikubwa mitatu itakayotekelezwa na Serikali itagharimu Dola 21 bilioni hivyo kufanya jumla ya deni kuwa sawa na Sh103 trilioni. “Ujenzi wa reli ya kati kwa tathmini yake unaweza kugharimu Dola 15 bilioni, Stieglers Gorge utagharimu Dola 5 bilioni na uboreshaji wa shirika la ndege Dola bilioni 1,” alisema Nape.

“Kwa hiyo unazungumzia Dola bilioni 21. Ukijumlisha na deni la Taifa la (Dola) bilioni 26 unazungumzia Dola bilioni 47. Kwa vyovyote vile hii ime-burst (imepita kikomo).

“Kama inakwenda ku-burst maana yake tunakwenda kutokopesheka. Kwa nini tunataka kung’ang’aniza kuchukua pesa ya Serikali. Hebu tufikirie upya. Dk Mpango rudini mkafikiri upya.”

Katika mchango wake, Serukamba ambaye alionekana kama kuwafungulia njia wabunge wa CCM, alisema mipango yote mitatu ni kama imeigizwa akitumia neno la ‘copy and paste’.

“Ukipitia yote wamebadilisha lugha, lakini kinachosemwa ni kile kile. Deni la Taifa linapanda kwa Sh4 trilioni kwa mwaka. Maana yake tumeamua kama Serikali kila kitu kinafanywa na Serikali,” alisema.

Serukamba, Bashe, Freeman Mbowe na wabunge wengine waliungana kwa kauli moja kuikosoa Serikali kwa kutoishirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa baadhi ya miradi ya kibiashara. “Hatuwezi kuendelea. Halipo Taifa duniani ambalo kila kitu wanajenga kwa fedha za Serikali. Tumekwenda Moscow uwanja wa ndege wa kimataifa umejengwa na mtu binafsi,” alisema Serukamba.

Alisema Serikali inasema inatekeleza miradi kwa ubia na sekta binafsi (PPP), lakini katika kitabu cha waziri wa Fedha na Mipango hakuna mradi ulioonyeshwa. “Serikali hii haiamini katika sekta binafsi. Nataka Bunge hili tukubaliane waziri wa Fedha atuambie, Serikali hii haikubaliani na sekta binafsi. Kama tumerudi kwenye ujamaa tuambiane,” alisema.

“Namuonea huruma sana Rais. Anahangaika lakini wenzake hawamwambii ukweli. Humu ndani waziri anaongelea kukusanya kodi peke yake. Tunakusanya kodi kwa nani?

“Leo mabenki yanakufa. Mabenki yote yanaonyesha kushuka kwa faida, hata mabenki makubwa, hata uchumi unaofanya vizuri tunaangalia ufanisi wa sekta ya mabenki na ufanisi wa soko la mitaji.”

Mbowe alisema: “Mahusiano kati ya Serikali na sekta binafsi sio mazuri. Hatutajenga uchumi wa nchi hii kwa mtutu wa bunduki. Hatujenga uchumi wa nchi hii kwa ubabe na vitisho.”

“Ni lazima Serikali itambue kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi na Serikali ni bodi. Hakuna Taifa lolote limeendelea duniani kwa kuipuuza sekta binafsi. Hakuna Taifa lolote duniani liliendelea kwa kufikiria sekta binafsi ni wezi. Kufanya biashara nchi hii chini ya awamu ya tano ni kiama. Wafanyabiashara wote wa ndani na nje wanalia,” alisema.

Kama ilivyo kwa wabunge wengine, Bashe naye alisisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi na kusisitiza sekta binafsi ijengewe mazingira wezeshi kuwekeza katika miradi ya kilimo.