Walimu wazichapa shuleni

Muktasari:

Tukio hilo limetokea jana Jumatano saa 2.45 asubuhi mwaka na limeripotiwa kituo cha polisi Mugumu

 

Serengeti. Walimu wawili wa Shule ya Msingi Kitarungu wilayani Serengeti wamezipiga ‘kavukavu’ ofisini huku wanafunzi wakishuhudia.

Tukio hilo limetokea jana Jumatano saa 2.45 asubuhi mwaka na limeripotiwa kituo cha polisi Mugumu, mkurugenzi mtendaji na serikali ya kijiji hicho.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Thomas Marwa ambaye alijeruhiwa katika ugomvi huo amesema akiwa ofisini akiandaa matokeo ya mtihani alivamiwa na mwalimu Yared Amosi na kumshambulia kwa makonde usoni.

“Kutahamaki akawa ameishanipiga ngumi tatu usoni na kunijeruhi jicho, nikalazimika kupiga kelele kuomba msaada," amesema.

Imeelezwa chanzo cha kushambuliwa ni kufuatia kumbana mwalimu kushindwa kutunga mtihani wa sayansi kwa darasa la tano, utoro kazini na ameishamwandikia barua ya onyo.

Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Yohana Getari amesema baada ya kusikia kelele alilazimika kukimbilia shuleni na kukuta ugomvi huo na mwalimu mkuu baada ya kupata upenyo alikimbia.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,  Juma Hamsini amesema tukio hilo ni utovu wa nidhamu na ameandika barua Tume ya Utumishi wa Walimu kuchukua hatua haraka kwa atakayebainika kuwa chanzo cha ugomvi huo.

Polisi wilayani hapa wamesema wanaendelea na uchunguzi na wakikamilisha watatoa taarifa ikiwemo kumfikisha mahakamani mhusika.