Mbunge wa zamani NCCR akanusha kuhamia CCM

Muktasari:

Mkosamali amesema unaweza kumsaidia Rais ukiwa upinzani

Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali amekanusha taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa amejivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na CCM.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumamosi Desemba 16,2017 amesema ana imani na upinzani imara. Ametaka kupuuzwa kwa taarifa kuwa anakwenda CCM kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli.

“Msimamo  wangu upo palepale na kama wamezusha ni wao na sababu zao. Watu wamenipigia simu kuniuliza kuhusu jambo hili. Sijaeleza lolote kuhusu kuhama NCCR. Watanzania tunahitaji upinzani imara, kuhama hatumsaidii Rais unaweza kumsaidia ukiwa hukuhuku upinzani,” amesema.