Kesi ya Sugu yahairishwa kwa muda

Muktasari:

Sugu na Masonga wanakabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli Desemba 30, 2017.


Mbeya. Ubishani wa kisheria umeibuka katika kesi inayowakabili Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema),  Joseph Mbilinyi 'Sugu' na Katibu wa  Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga baada ya hoja ya wakili wa washtakiwa, Peter Kibatala kutaka kuanza na shahidi wa kwanza ambaye ni Mkuu Upelelezi Mkoa wa  Mbeya, kupingwa na Jamhuri.

Mabishano kati ya pande hizo mbili yametokea leo Februari 8, 2018 na kusababisha Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite kuahirisha kesi kwa muda na kuwaita mawakili wa pande zote na kwenda nao ofisini kwake ili wakajadiliane.

Awali, Kibatala aliieleza Mahakama hiyo kwamba wapo tayari kuendelea na utoaji ushahidi na ataanza na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya (RCO).

“Mmh! Naona kama kuna ukakasi,  eti hakimu upande wa Serikali?” amehoji hakimu Mteite.

 

Wakili wa Jamhuri,  Joseph Pande alisimama na kupinga kwa shahidi huyo kuwa wa kwanza huku akisisitiza  kwamba katika utetezi huo, watuhumiwa ndiyo wanaopaswa kuanza.

"Kimsingi anayetakiwa kuanza ni mtuhumiwa kujitetea na kama atakuwa na  mashahidi ndipo wataitwa hao mashahidi wake. Sasa hii itakuwa ni jambo la ajabu kutokea kama ataanza shahidi tofauti na mhusika mkuu (mshtakiwa),” amesema Pande.

Kibatala alisimama na kumpinga Pande akidai hakuna kifungu cha sheria kinachozuia kufanya hivyo na wala hakuna athari yoyote.

“Hapa tutakuwa tunapoteza muda bure. Hakuna katazo  lolote kisheria,” amesema Kibatala.

Kutokana na mabishano hayo Mteute amewaita mawakili hao kwa ajili ya kujadiliana, hivyo kuahirisha kesi hiyo kwa muda.

Sugu na Masonga wanakabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli ambayo wanadaiwa kuitoa Desemba 30, 2017