Wizara yaeleza sababu wanawake kuathirika zaidi na VVU

Muktasari:

Wizara ya Afya yaeleza sababu saba za mwanamke kuwa katika hatari zaidi ya kupata maambuki za virusi vya Ukimwi (VVU).

Dodoma. Wizara ya Afya imetaja sababu saba za mwanamke  kuwa katika uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kuliko mwanaume.

Akizungumza leo Februari 9, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Mtambwe (CUF), Khalifa Mohamed Issa , Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema moja ya sababu hiyo ni maumbile ya mwanamke.

Mbunge huyo ametaka kujua sababu za kitaalamu ambazo zinasababisha wanawake kuathirika zaidi kuliko wanaume.

Dk Ndugulile amesema maumbile ya mwanamke ni rahisi kupata michubuko wakati wa tendo la ndoa na hivyo kurahisisha virusi hivyo kupenya.

"Aidha maumbile ya mwanamke hupokea mbegu za wakati wa tendo la ndoa, iwapo mwanamke atafanya mapenzi na mwanaume mwenye VVU  lazima ataambukizwa,” amesema.

Ametaja sababu nyingine ni  mazingira hatarishi ambayo husababisha hatari zaidi kwa wanawake kuambukizwa ikiwamo kufanya biashara ya ngono na kuanza mapenzi katika umri mdogo.

Dk Ndungulile ametaja mfumo dume katika jamii kuwa unawapa fursa wanaume  kuamua kufanya ngono na wanawake wengi, kutokutumia kondomu, kuoa wasichana wenye umri mdogo na kufanya ukatili wa kijinsia.