VIDEO-Kifo mwanafunzi NIT chagusa kila kona

Muktasari:

  • Na kutokana na msiba huo Serikali imeahidi kugharimia mazishi ya binti huyo huku Rais John Magufuli akiagiza uchunguzi wa haraka.

Dar es Salaam. Kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa siku tatu zilizopita kwa kupigwa risasi na polisi kimeigusa Serikali, taasisi, vyama vya siasa, wasanii na wananchi wengine kwa ujumla.

Na kutokana na msiba huo Serikali imeahidi kugharimia mazishi ya binti huyo huku Rais John Magufuli akiagiza uchunguzi wa haraka.

Wakati Serikali ikiahidi hilo, jana nyumbani kwa ndugu wa mwanafunzi huyo eneo la Mbezi Louis jijini Dar es Salaam vilio, majonzi na simanzi vilitawala, huku Mkuu wa Polisi nchini (IGP), Simon Sirro akiwa miongoni mwa watu waliofika nyumbani hapo.

Tayari Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia askari wake sita kwa uchunguzi pamoja na silaha zao.

Akwilina aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Ununuzi na Ugavi katika chuo hicho, kifo chake kimeibua hisia tofauti katika jamii na kuzua mjadala kwenye mitandao ya kijamii.

Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) na Chama cha ACT Wazalendo, jana walimuomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba ajiuzulu ili kuonyesha uwajibikaji kwa maelezo kuwa ameshindwa kusimamia amani.

Akwilina alipigwa risasi Ijumaa iliyopita eneo la Mkwajuni, Kinondoni wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliokuwa wakielekea katika ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aaron Kagurumjuli kudai hati ya viapo vya mawakala wao.

Rais Magufuli atoa pole

Katika ukurasa wa Twitter, Rais alisema amesikitishwa na tukio hilo akitoa pole kwa familia, ndugu na wanafunzi walioguswa na msiba huo. Dk Magufuli aliagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hilo.

Akiwa wilayani Chato mkoani Geita katika uzinduzi wa gereza jana, Waziri Mwigulu aliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa aliyehusika na tukio hilo na kuwaeleza wananchi nini kilichotokea.

Serikali kugharimia mazishi

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo watahakikisha wanasimamia shughuli zote za msiba huo.

Profesa Ndalichako alisema Akwilina alipigwa risasi akiwa katika majukumu yake wakati akipeleka barua ya mafunzo kwa vitendo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

“Mafunzo yale kwa vitendo yalikuwa yanatarajiwa kuanza Februari 26 mwaka huu, hivyo kifo chake kimeleta simanzi kwa wananchi wote na Serikali kwa ujumla,” alisema Profesa Ndalichako.

“Akwilina alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa kike waliojipambanua kwa kujua umuhimu wa elimu. Alihakikisha kwamba anasoma kwa bidii kwa manufaa yake na familia yake, lakini pia alikuwa mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu.”

Katika mkutano huo, waziri huyo aliambatana na naibu waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni aliyeahidi kuwa uchunguzi wa tukio hilo utafanyika haraka iwezekanavyo kwa weledi na utaalamu ili haki itendeke.

Nyumbani kwa ndugu wa Akwilina

Mwandishi wa Mwananchi aliyefika nyumbani kwa ndugu wa Akwilina eneo la Mbezi Louis alikuta ndugu, jamaa na wanafunzi wenzake wa NIT wakiwa na nyuso za huzuni, baadhi wakishindwa kujizuia na kuangua vilio.

“Sitakuona tena mdogo wangu, wazazi masikini kule nyumbani walitumaini ungewasaidia, mbona uliniahidi mengi mama? Umeishia kupigwa risasi Mkwajuni buriani kipenzi changu,” alilia Tugolena Richard Uiso, ambaye ni dada wa Akwilina.

“Nilimwambia mdogo wangu soma kwa bidii uje utuokoe, usije kuishi maisha haya bahati nzuri ukapata mkopo asilimia mia sasa mbona hujatimiza ahadi yako? Mbona umekufa? Umetuacha na nani sasa? Uwiii nisaidieni mwenzenu.”

Tugolena alisema Akwilina alikuwa mtoto pekee aliyefikia elimu ya juu katika familia yao na asingepata mkopo kwa asilimia 100 asingeweza kuendelea na masomo.

Hadi saa saba mchana jana, ndugu wa Akwilina hawakuwa na uhakika wa kuandaa chakula kutokana na hali ngumu ya maisha.

Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo walitoa fedha zilizosaidia kununua mchele na maharage.

Mlezi wa Akwilina ambaye ni kaka yake, Festo Kawishi alisema hawajakabidhiwa mwili zaidi ya kuutambua na kwamba, wanachosubiri ni uchunguzi kama walivyoahidiwa.

“Hatuna mahali pa matanga, hapa si kwetu tupo tu tumekaa tunasubiri taarifa ya Serikali itueleze kuhusu mtoto wetu, yuko wapi na amepatwa na tukio gani ndipo sisi tuamue msiba utafanyika wapi au tutasafirisha,” alisema.

Kawishi alimuomba Naibu Waziri, Masauni awepo wakati wa uchunguzi wa mwili wa mtoto wao.

Sirro, Ndalichako msibani

Baadhi ya viongozi waliokuwepo nyumbani kwa ndugu wa Akwilina ni Profesa Ndalichako, Masauni na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro aliyeagiza kufanyika uchunguzi wa tukio hilo.

Profesa Ndalichako alitoa rambirambi ya Sh1 milioni wakati uongozi wa NIT ukitoa Sh500,000.

Polisi sita wanashikiliwa

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Kituo cha Polisi Oysterbay kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa ubunge wa Jimbo la Kinondoni uliofanyika juzi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema Akwilina alifariki baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali wakati polisi wakisambaratisha maandamano ya Chadema.

Alisema polisi imeunda timu ya upelelezi ambayo pamoja na mambo mengine inawashikilia askari sita.

“Katika uchunguzi huo Jeshi la Polisi linawashikilia askari wake sita na silaha zao zinachunguzwa ikiwa ni pamoja na kuzipeleka kwa wataalamu wa milipuko kwa uchunguzi wa kina,” alisema Kamanda Mambosasa.

Alisema baada ya purukushani ya maandamano ya Chadema saa 1:30 usiku alipata taarifa za kiintelijensia kuwa mtu mmoja amepoteza maisha na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala, huku Erick Mushi na Innocent Mushi wakijeruhiwa.

Alisema Kamanda wa Polisi Kinondoni alikwenda Hospitali ya Mwananyamala na kukuta mwili wa mwanafunzi huyo, “Ni Mchaga anayesadikiwa kuwa mwanafunzi wa NIT, alikutwa akiwa na jeraha kubwa kichwani linaloonekana kupigwa na kitu chenye ncha kali kilichoingia upande wa kulia na kutokea kushoto,” alisema.

Alisema Akwilina alikuwa kwenye daladala aina ya Nissan Civilian inayofanya safari kati ya Mabibo na Makumbusho. Aliongeza kuwa chanzo cha tukio hilo ni maandamano ya viongozi wa Chadema baada ya kufanya mkutano wa kufunga kampeni katika Uwanja wa Buibui uliopo Mwananyamala.

“Saa 11:45 jioni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipanda jukwaani na kuhamasisha wanachama kuandamana kuelekea ofisi za mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kumshinikiza awape barua za viapo vya mawakala wao,” alisema Mambosasa.

Alisema wanachama wa Chadema walipofika eneo la Mkwajuni walifunga barabara na kusababisha msongamano na kwamba, polisi walipofika eneo hilo kwa lengo la kuwatawanya, walianza kuwashambulia askari kwa fimbo na silaha nyingine na kujeruhi polisi wawili.

Alisema katika kujihami polisi walitumia silaha za kutuliza ghasia na walipoona wanashindwa walifyatua risasi hewani na kuwakamata watuhumiwa 40.

Kamanda Mambosasa alisema hawajathibitisha kama risasi iliyompata Akwilina ilipigwa na askari na kwamba watuhumiwa 40 wanachunguzwa ili kubaini kama miongoni mwao walikuwa na silaha za moto. “Polisi inaendelea kuwatafuta wafuasi wa Chadema walioshiriki kuwashawishi wenzao kushiriki kwenye maandamano. Pia tunachunguza kifo cha Daniel John aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Hananasif ambaye mwili wake ulikutwa umetupwa maeneo ya fukwe za Coco,” alisema.

Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila alisema aliyesababisha watu kuingia barabarani ni Msimamizi wa Uchaguzi Kinondoni, Kagurumjuli kwa sababu aliwanyima mawakala wa Chadema barua zao za viapo.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema alisema Mbowe hajajificha na kwamba polisi ikimtaka itampata.

TSNP, ACT walia na Mwigulu

Mwenyekiti wa TSNP, Abdul Nondo na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, Licapo Bakari wamemtaka Dk Nchemba kujiuzulu ili kuonyesha uwajibikaji Kutokana na matukio ya mauaji na utekaji kuendelea kutokea.

Wasanii maarufu karibu wote wamelaani tukio hilo kama walivyofanya wananchi wa kawaida katika mitandao ya kijamii.

Imeandikwa na Peter Elias, Elias Msuya, Herieth Makwetta, Tumaini Msowoya na Allence Juma.