Viongozi wakuu Chadema, akiwemo Mbowe watakiwa kujisalimisha Polisi

Muktasari:

Mbali na Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni viongozi wengine wanaotakiwa kujisalimisha  ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji; manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewataka viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kujisalimisha  kituo kikuu cha polisi.

 

Mbali na Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni viongozi wengine wanaotakiwa kujisalimisha  ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji; manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee; Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Ester Matiko ambaye ni Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake (Bawacha).

 

Akizungumza na Mwananchi leo Februari 19, 2018, kuhusu viongozi hao waandamizi kuitwa polisi, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema: “Hao ni watuhumiwa kama wameitwa ni ‘privilege’ tu, ila wanapaswa kukamatwa kwa yale yaliyotokea.”

 

Awali, taarifa ya Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliyoitoa leo Februari 19, 2018 imesema wito wa barua wameupokea saa 10:51 jioni kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam iliyoelekezwa kwa Mwanasheria, Makao Makuu ya Chadema  ikiwataka viongozi hao kufika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda hiyo leo saa 11:00 jioni bila kukosa.

 

“Tunapenda kuutaarifa umma kuwa tunawasiliana na wanasheria wetu ili kujua ratiba zao pamoja na ratiba za viongozi wanaotakiwa kuripoti polisi ili wapange jinsi ya  kuutekeleza wito huo wa Jeshi la Polisi,” amesema Mrema.

 

“Barua hiyo ya wito imeelekezwa kwa Mwanasheria ambaye sio mtendaji mkuu wa chama na pia imetolewa kwa viongozi niliowataja kana kwamba viongozi hao wapo pamoja muda wote jambo ambalo sio sahihi.”

 

Mrema amesema kwa kuwa viongozi hao wametawanyika maeneo mbalimbali ya nchi katika kutekeleza majukumu yao, ni vyema Jeshi la Polisi likayaelewa mazingira hayo wakati wakiendelea na utaratibu wa kutekeleza wito huo na kuepuka kuwa sehemu ya propaganda za kisiasa zinazoendelea.

 

Amesema wanasheria wa Chadema watawasiliana na polisi  kuwajulisha muda ambao wito huo utatekelezwa kulingana na hali halisi ya mazingira ya walipo viongozi tajwa kwa sasa.

 

“Tunapenda kuwajulisha wanachama wetu na umma kuwa viongozi wetu wapo imara na wanaendelea kuimarika zaidi,” amesema Mrema.