Mwongozo wa Benki Kuu kuzinufaisha benki za biashara, taasisi za fedha

Muktasari:

Sekta ambazo ziliathirika zaidi kutokana na kupungua kwa mikopo ni kilimo, viwanda, biashara, mikopo ya mishahara na sekta ya hoteli na utalii, ambazo huchangia kiwango kikubwa kwenye uchumi.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mwongozo mpya ambao utawezesha benki za biashara na taasisi za kifedha kuongeza utoaji wa mikopo kwenye sekta binafsi.

Kwa sasa, kiwango cha utoaji wa mikopo kwenye sekta binafsi kimedorora katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kutokana na changamoto za kiuchumi ambazo zimesababisha benki kukosa imani kwa wakopaji.

Sekta ambazo ziliathirika zaidi kutokana na kupungua kwa mikopo ni kilimo, viwanda, biashara, mikopo ya mishahara na sekta ya hoteli na utalii, ambazo huchangia kiwango kikubwa kwenye uchumi.

Hiyo ilisababisha shughuli nyingi za kiuchumi kudorora na kushindwa kuchangia kikamilifu katika pato la Taifa na pia kushindwa kuzalisha ajira mpya kwa ajili ya Watanzania.

Mwongozo huo pia utaziwezesha benki na taasisi za fedha kuandaa utaratibu wa kuratibu viwango vya mikopo chechefu (iliyo katika hatari ya kutolipika) ambacho kimefikia zaidi ya wastani wa unaotakiwa kisheria wa asilimia tano.

Mikopo chechefu imekuwa changamoto kwa sekta ya benki kwani kwa mujibu wa ripoti za BoT, Desemba kiwango hicho kilifikia asilimia kumi na moja.

Kwa mujibu wa mwongozo mpya, wakopaji wanaonufaika na mikopo kwa sasa, hasa wenye rekodi nzuri ya urejeshaji, watapata unafuu kwani wataendelea kuvumiliwa pale uwezo wao wa kurejesha utakapopungua.

Kwa wakopaji wapya, hali huenda ikawa tofauti kwani benki na taasisi za fedha zimeagizwa kuhakikisha kwamba utoaji wa mikopo unazingatia kupunguza hatari za kibiashara pale mkopaji atakaposhindwa kulipa.

Pia, wakopaji wapya huenda wakapitia mchakato mrefu na ‘mgumu’ kwani wanatakiwa kuwaridhisha wakopeshaji kabla ya kukubaliwa kukopa.

Hatua hiyo itapunguza kwa kiwango kikubwa mikopo isiyo na dhamana ambayo imekuwa ikitolewa kwa wakopaji binafsi kupitia mishahara.

Ukuaji wa utoaji mikopo kwenye sekta binafsi ulipungua katika kipindi cha miezi 24 iliyopita na kufikia chini ya asilimia moja kutoka asilimia 24 ya mwanzoni mwa mwaka 2016, kwa mujibu wa ripoti BoT za kila mwezi za mapitio ya uchumi.

Mwongozo huo pia umeambatana na kuondolewa kwa kanuni nne zilizomo kwenye Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2014 ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo pamoja na kupambana na mikopo chechefu.

Katika barua yake kwa benki na taasisi za kifedha nchini, naibu gavana (uthabiti na ukuzaji wa sekta ya kifedha), Dk Benard Kibesse alisema benki pia zimeagizwa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu juu ya mikakati yao ya kufikia malengo ya mwongozo.

Barua hiyo ya Februari 19 inaonyesha kuwa BoT inataka kupunguza madhara ya kiuchumi yanayotokana na kupungua kwa mikopo na kuongezeka kwa ile chechefu.

Dk Kibesse alisema benki na taasisi za fedha zimeagizwa kuandaa na kutekeleza mikakati maalumu itakayosababisha kuongeza kwa mikopo kwenye sekta binafsi na kupunguza mikopo chechefu. BoT pia imesema haitaki kuona mikopo chechefu mipya.

Badhi ya kanuni zilizoondolewa ni zile zinazolenga masuala ya namna ya utoaji wa mikopo, urejeshaji wa mikopo, na ufutaji wa mikopo chechefu kwenye hesabu za benki.

Benki zimeagizwa kuanzisha mkakati wa kupunguza mikopo chechefu na kuanzisha utaratibu endelevu wa urejeshaji wake na kutenga kazi za idara ya mikopo na idara nyingine za benki.

Kwa wale wakopaji ambao wana rekodi nzuri ya kurejesha mikopo, pia wamepewa nafasi ya kupangiwa utaratibu wa marejesho iwapo watakumbana na hali ngumu itakayosababisha kushindwa kulipa hadi mara nne kutoka mara mbili za awali.