Aga Khan kupunguza gharama za matibabu katika vituo vyake vyote

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo, James Mkumbo akikata utepe kuzindua Kituo cha Afya cha Aga Khan Polyclinic Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni mkurugenzi wa Uuguzi Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan nchini, Lucy Hwai na mkaguzi msaidizi wa Polisi Kimara, Zena Lukoya. Picha na Venance Nestory.

Dar es Salaam. Ofisa mwendeshaji mkuu wa Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan nchini, Sisawo Konteh amesema taasisi hiyo itapunguza gharama za utoaji wa huduma za afya kwa vituo vyake vyote ili kumwezesha kila mwananchi kupata huduma bora.

Konteh alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kituo cha afya cha taasisi hiyo eneo la Matangini, Kimara Mwisho.

Alisema baadhi ya wananchi wanaamini kuwa taasisi hiyo inatoa huduma kwa gharama kubwa kiasi ambacho watu wa kawaida hushindwa kuzimudu.

“Taasisi yetu haipo kwa minajili ya kufanya biashara na kutengeneza faida, bali kutoa huduma bora na nafuu za afya kwa Watanzania wote pasipo ubaguzi wowote,” alisema.

Konteh alisema ufunguzi wa kituo cha afya cha Aga Khan eneo la Kimara, umetoa fursa kwa wakazi wa eneo hilo kupata huduma za afya kwa ukaribu na kwa bei nafuu.

“Kuhusu suala la gharama, naomba wananchi wasiwe na wasiwasi huduma zetu zitakuwa za bei nafuu kiasi ambacho kila mmoja ataweza kuzimudu,” alisema na kubainisha huduma zitakazotolewa katika kituo hicho kuwa ni za upimaji wa awali wa magonjwa mbalimbali yakiwamo ya moyo.

Alisema kituo hicho kitawaleta madaktari bingwa watakaokuwa wakikitembelea na kutoa huduma mbalimbali za afya.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo, James Mkumbo ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori alipongeza utaratibu wa taasisi hiyo wa kupunguza gharama za matibabu.

“Tulizoea kusikia na kuona huduma mnazozitoa zikihusu watu wa Masaki, Posta... jambo lililotufanya tuamini kuwa Hospitali ya Aga Khan ni kwa ajili ya vigogo na si wananchi wa kawaida. Ujio wenu katika wilaya yetu na kupunguza gharama, kumefanya tufute dhana iliyokuwa imejengeka kuwa Aga Khan ni hospitali ya gharama kubwa,” alisema.

Mkumbo aliutaka uongozi wa hospitali hiyo kutafuta namna ya kuwahamasisha wananchi wa Ubungo na Kimara kwa kutoa huduma bure siku ambayo kituo hicho kitaanza kazi rasmi, “Najua leo mmefungua kituo hamjaanza huduma, ninaomba siku ambayo mtaanza mtoe ofa kwa wakazi wa Kimara kupata huduma za afya bure hasa kina mama.”

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Safaa Chonga alisema uwepo wa kituo hicho utasaidia kusogeza karibu huduma za afya kwa wagonjwa kwani wilaya hiyo ina vituo 12 tu na kituo cha Aga Khan ni cha kwanza wilayani humo.

“Tutashirikiana nanyi katika kutatua changamoto mbalimbali za afya na tunaomba kituo hiki kiwe kinapokea bima za afya zinazotumiwa na Serikali,” alisema.