Vijana ACT-Wazalendo walia na ajira nchini

Muktasari:

ACT wamesema ombi lao hilo linatokana  wafanyakazi wengi kuachishwa kazi katika binafsi na serikalini

Dar es Salaam. Ngome ya vijana ya Chama cha ACT Wazalendo imewataka mawaziri wenye dhamana ya kusimamia viwanda, ajira na fedha kukaa pamoja kutafakari tatizo la ajira kwa vijana na kuweka mazingira bora ya ufanyaji wa biashara ndogondogo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Machi 10, 2018, Katibu wa Sera na Tafiti wa Ngome ya vijana wa chama hicho,  Kitentya Luth amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kushuhudia wimbi la waajiri sekta binafsi na Serikali kupunguza wafanyakazi.

"Hata sekta ya elimu na viwanda ambazo awali zilikuwa zinatoa ajira nyingi nazo hali ni mbaya. Walimu hawajapata ajira kwa zaidi ya miaka mitatu, jambo hilo linasababisha mkwamo katika elimu lakini pia vijana hao wanashindwa kujikwamua kimaisha," amesema Luth.