Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita,

Muktasari:

Meya Mwita ambaye ni diwani wa Chadema, alikuwa ni mmoja wa viongozi waliohudhuria maadhimisho ya wiki ya maji yanayoendelea nchini.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameonekana kuwarushia vijembe wapinzani huku akimsifu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, kuwa ana msimamo na hayumbishwi na msimamo wa vyama.

Meya Mwita ambaye ni diwani wa Chadema, alikuwa ni mmoja wa viongozi waliohudhuria maadhimisho ya wiki ya maji yanayoendelea nchini.

Makonda alimmwagia Mwita sifa hizo baada ya Mwita kuzungumza na kumkaribisha.

“Meya nilijua utazungumzia maandamano ila niseme wazi namkubali sana Isaya, ni miongoni mwa watu ambao unaweza kukaa nao mkazungumzia maendeleo,” alisema Makonda.

Makonda alisema kwamba Mwita hana tabia kama za wenzake na muda mwingi anafikiria maendeleo.

Akizungumzia maandamano yanayozungumzwa zaidi kwenye mitandao, mkuu huyo wa mkoa alisema baadhi (bila kutaja ni nani) wanasubiri wawaingize watoto wa watu barabarani waandamane, wavunjwe miguu halafu wawatafute watu wa Ulaya wawape fedha.