Wadau sekta ya biashara, uchumi wampa JPM changamoto sita

Mwenyekiti wa sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi (kushoto) akizungumza katika mkutano wa Kumi na Moja wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ulioongozwa na mwenyekiti wake, Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Ikulu

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuagiza utatuzi wa kero za wafanyabiashara ndani ya wiki moja, wadau wa sekta za viwanda, kilimo na biashara wameshauri mambo sita yanayohitaji kufanyiwa kazi.

Juzi, Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC), aliendesha mkutano wa Kumi na Moja wa Baraza hilo, uliobeba maudhui ya ‘Tanzania ya Viwanda na Ushiriki wa Sekta binafsi nchini’ ambao washiriki walitaja kero zinazokwamisha uendeshaji wa shughuli zao ambazo alizipokea na kuagiza mawaziri kwa kila sekta husika kuzishughulikia ndani ya wiki moja.

Jana, walipotakiwa kutoa maoni yao kuhusu mkutano huo, wadau hao walitoa mapendekezo mbalimbali kati ya hayo, sita yakijitokeza zaidi.

Profesa Haji Semboja wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema Serikali inatakiwa kufanya maboresho katika mfumo uliopo kwa sasa ili kuongeza ufanisi katika taasisi zinazolalamikiwa na wafanyabiashara.

“Mfumo kwa maana ya sheria, sera na kanuni zilizopo, zinaweza kusaidia utekelezaji wa changamoto hizo bila kuwa na vikwazo, TRA inafanya kazi kwa mujibu wa hizo sheria na taratibu, kwa hiyo inatakiwa kufanyia kazi mfumo. Uboreshaji huo usiwe na makosa kwa mfano, kitengo cha daktari wa meno unaweka daktari wa kutibu ugonjwa mwingine,” alisema.

Profesa mwingine wa uchuni UDSM, Humphrey Moshi alipendekeza kuanzishwa kwa kikosi maalumu kitakachounganisha sekta zote zinazohusika katika harakati za utekelezaji wa uchumi wa viwanda.

“Kuna haja ya kuwa na kikosi kama ilivyokuwa Big Result Now (BRN- Matokeo Makubwa Sasa), kiweze kuratibu sekta zinazohitajika kwenye uchumi wa viwanda kwa mfano; elimu, kilimo, umeme na mifugo ili kuondoa mgongano wowote wa kisera ambao utachelewesha,” alisema Profesa Moshi.

Mhadhiri mstaafu wa Shule ya Biashara UDSM, Dk Richard Mushi alisema jambo jingine ni kuanzisha mipango ya muda mrefu na mfupi akitaja malalamiko ya uagizaji wa sukari, ushuru wa barabarani, bandarini kuwa ni kero zinazotakiwa kushughulikiwa katika mpango wa muda mfupi.

“Lakini ni lazima sasa tuwe na mpango wa muda mrefu. Kwa mfano, katika umeme tuwe na mikakati, kila mwaka iwe inajulikana tunafanya nini kuhusu umeme, kujua tunapowekeza viwanda maji na umeme vipo? Tunatakiwa kuzingatia uanzishaji wa viwanda kwa kuzingatia mahitaji ya miundombinu hiyo, isiwe kuanzisha kiwanda kwa kila mkoa tu,” alisema Dk Mushi.

Aliyewahi kuwa mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Emmanuel Ole Naiko alisema eneo jingine la kufanyiwa kazi ni marekebisho katika mbinu za ukusanyaji wa mapato ili kuongeza uhusiano kati ya Serikali na wafanyabiashara.

“Methodology (Mbinu/utaratibu) siyo nzuri kwa sasa katika ukusanyaji wa kodi. Kodi inatafutwa na Polisi! Siyo nzuri, nimeishi US (Marekani), ukusanyaji wa kodi ni friendly (rafiki) sana, kila mlipaji kodi anasema na anawajibika kulipa kodi mwenyewe.”

Pendekezo jingine lilitolewa na kaimu mkurugenzi wa sera na ushauri wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Akida Mnyenyelwa akisema TRA inatakiwa kuimarisha uhusiano wake na wafanyabiashara

“Kwa ujumla mkutano umesaidia sana kujibu hoja palepale. Lakini tulieleza kero kadhaa. Kwa mfano, madai ya asilimia 15 ya kodi za wafanyabiashara wanazotakiwa kurejeshewa na TRA kupitia uingizaji wa bidhaa, warejeshewe,” alisema Akida.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Asasi za Kilimo (Ansaf), Audax Rukonge alisema jambo jingine linalohitajika ni kuongeza bajeti ya kilimo na mikopo kwa vijana na wanawake kupitia benki ya wanawake nchini ili kuchochea kasi ya uzalishaji.

Pia, alitaka Serikali iwekeze zaidi katika huduma za ugani kupitia watalaamu wa ushauri kwa wakulima.

Walivyoguswa

Mbali ya mapendekezo hayo, wadau hao wameelezea kufurahishwa kwao na jinsi Rais Magufuli alivyoendesha majadiliano na wafanyabiashara.

“Ni tukio muhimu sana katika Taifa kwa Rais kusikiliza na kutoa maamuzi palepale, kero za wafanyabiashara zikishughulikiwa maana yake, kodi itapatikana vizuri bila mgogoro, na kodi hiyo ndiyo inayotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” alisema Profesa Moshi.

Ole Naiko alisema majadiliano hayo yamesaidia ufumbuzi wa kero nyingi kwa wakati mmoja jambo ambalo lisingewezekana katika ofisi za Serikali kutokana na urasimu.

Alisema kodi ndiyo nguvu ya maendeleo nchini, lakini kwa muda mrefu imekuwa na mgogoro kati ya wafanyabiashara na TRA.