Meya wa Jiji Dar azungumzia uchumi wa viwanda

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita

Dar es Salaam. Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amesema Tanzania bado inahitaji utaalamu wa masuala ya teknolojia kuelekea  uchumi wa viwanda.

Mwita ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 21, 2018 katika hafla ya kubadilishana uongozi wa  Chuo Kikuu cha United African Tanzania  (UAUT) kinachomilikiwa na Wamisionari kutoka Korea Kusini, iliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho.

Amesema Watanzania wana uwezo wa kufanya kazi na nia ya kuwa nchi ya viwanda na wanachohitaji kwa sasa ni utaalamu wa teknolojia.

“Sisi hatuhitaji fedha, tuna nguvu ya kufanya kazi na Korea Kusini mmeendelea katika eneo hilo mnaweza kutusaidi,” amesema Mwita.

Amesema Korea Kusini wamefanikiwa kufundisha watu wao tabia ya kufanya kazi kwa bidii na Watanzania,  hivyo wanaweza kufanya hivyo wakiwa na uelewa wa teknolojia.

“Tunaahidi tutaendelea kushirikiana nanyi na kujifunza zaidi teknolojia kama ambavyo wanafunzi wa Kitanzania wanavyopata mafunzo ya uhandisi yanayotolewa chuoni hapa,” amesema Mwita.

Ameuataka uongozi mpya wa chuo hicho kujitangaza ili Watanzania wakifahamu chuo hicho na kupata elimu bora ya uhandisi.

Mwenyekiti mpya wa chuo hicho, Choong Won Lee amesema atasimamia weledi wa taaluma ili wanafunzi wanaohitimu kutoka katika chuo hicho wawe na nafasi kubwa ya ushindani katika soko la ajira au kujiajiri.

 Balozi wa Korea Kusini nchini, Song Geun -Yong amesema kupitia chuo hicho, Korea Kusini inachangia kukuza uchumi wa Tanzania.