Teknolojia imeiwezesha Serikali kuona kila Shilingi inayoingia nchini kwa siku

Muktasari:

Mpaka sasa, Serikali imejenga kilomita 7,560 za mkongo wa Taifa kutokana na mkopo nafuu iliyoupata kutoka China. Aidha, sekta binafsi kupitia umoja wa kampuni za simu imejenga kilomita 1,401.26. Vilevile, kampuni ya Halotel nayo imejenga kilomita 18,000.

Kuongeza usimamizi na udhibiti wa mapato yake, naibu waziri huyo anasema, Serikali inakusudia kujenga vituo vingine viwili Dodoma na Zanzibar. Kwa hiki kilichopo, anasema asilimia 25 hutumika kuhifadhi data za Serikali na asilimia 75 za sekta binafsi.

Mpaka sasa, Serikali imejenga kilomita 7,560 za mkongo wa Taifa kutokana na mkopo nafuu iliyoupata kutoka China. Aidha, sekta binafsi kupitia umoja wa kampuni za simu imejenga kilomita 1,401.26. Vilevile, kampuni ya Halotel nayo imejenga kilomita 18,000.

Mkongo wa Taifa umefika kwenye mikoa yote na mipakani mwa nchi za jirani zisizopakana na bahari za Uganda, Rwanda, Zambia, Burundi na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kutokana na maeneo mengi nchini kuunganishwa kwenye mkongo huo, taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha matumizi ya intaneti yameongezeka kutoka zaidi ya watumiaji milioni 19.86 waliokuwapo Desemba 2016 hadi milioni 23 Desemba mwaka jana.

Naibu waziri anasema hadi mwaka 2020, matumizi ya intaneti yataongezeka zaidi kutokana na kushamiri kwa mifumo ya kieletroniki katika sekta zote kama vile ukusanyaji wa malipo kwa njia ya mtandao, matokeo ya mitihani, usajili wa vyuo vikuu na vya ufundi, afya na elimu mtandao, usajili wa vizazi na vifo (Rita) na Usajili wa Biashara (Brela).

Uchumi

Sekta ya mawasiliano ni mtambuka ambayo huziwezesha taasisi za umma na binafsi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Licha ya mkongo wa Taifa, Serikali pia imejenga miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ikiwamo minara ya mawasiliano ya simu za mkononi kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano.

Wakati taarifa ya tathmini ya mwenendo wa uchumi na ustawi wa jamii mwaka 2017 ikionyesha uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 6.8, shughuli za habari na mawasiliano zilikua kwa asilimia 13.1 na kuifanya sekta ya pili kati ya sita zilizokua kwa kasi kubwa zaidi.

Mawasiliano vijijini

Wakati matumizi ya simu za mkononi kufanikisha huduma za fedha zikiipa Tanzania sifa nje ya mipaka yake, yapo baadhi ya maeneo hayana mtandao huo wa mawasiliano.

Hata hivyo, hali inaendelea kuwa nzuri kwani asilimia 94 ya wananchi wote nchini wanapata huduma za mawasiliano na Serikali imetoa ruzuku kwa kampuni za simu nchini kujenga minara na kufikisha huduma hizo maeneo ambayo hayajaunganishwa.

“Hadi sasa, Serikali imetoa Sh95 bilioni kufikisha mawasiliano vijijini na tayari kata 451 zimepata mawasiliano kupitia ruzuku ya Serikali,” anasema Nditiye.

Anafafanua kuwa, katika mwaka wa fedha wa 2017/18, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umetoa zabuni ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika kata 75 zenye vijiji 154, ambapo kata nane zenye vijiji 15 zimekamilika na mpaka Juni, 67 zilizobaki zitakuwa zimekamilika pia.

Serikali ina makubaliano na kampuni ya Viettel inayomiliki Halotel, kufikisha huduma ya mawasiliano kwenye vijiji 4,000 na tayari, mpaka Februari, walikuwa wameviunganisha vijiji 3,712 na ujenzi unaendelea kwa vijiji 288 vilivyosalia mwaka 2018/19.

Mustakabali

Pamoja na mafanikio yaliyobainishwa, juhudi bado zinatekelezwa kuhakikisha sekta ya mawasiliano inaongeza tija kwa Taifa na maisha ya wanananchi kwa ujumla.

Kufikisha huduma hizo maeneo yote nchini, katika mwaka wa fedha 2018/19 wizara husika imepanga kutekeleza miradi kadhaa ya kipaumbele.

Miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni kuendeleza ujenzi wa mkongo wa Taifa kwa dhamira ya kufikisha huduma zake makao makuu ya wilaya zote nchini.

Wakati wilaya zote zikitarajiwa kuunganishwa kwenye mkongo huo, mkakati wa kusimamia na kudhibiti mapato ya Serikali unao umepewa kipaumbele. Kufanikisha hilo, Serikali inaratibu ujenzi wa vituo vya kutunza data, Dodoma na Zanzibar.

Vilevile, Serilaki itaendelea kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi katika miji yote nchini.

Mwaka mmoja uliopita, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania (TPC) ilizindua huduma ya ‘Posta Mlangoni’ jijini Dar es Salaam.

TCRA ilisema itashirikiana na wenyeviti wa serikali za mitaa kufanikisha uwekaji wa anuani hizo za makazi katika Mkoa wa Dar es salaam wenye jumla ya mitaa 573.

Changamoto

Kukua kwa teknolojia, kama ilivyo maeneo mengine, kuna changamoto zake ambazo ni lazima zishughulikiwe.

Changamoto kubwa ni upatikanaji wa mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo yakiwamo ya mipakani ambako kuna mwingiliano baina ya kampuni za Tanzania na nchi jirani.

Kwa mfano, maeneo ya mwambao wa maziwa makuu kama vile Ziwa Nyasa kutoka Ludewa mkoani Njombe hadi Kyela mkoani Mbeya ambapo wananchi waishio kwenye baadhi ya kata kama vile Lupingu wanakabiliwa na changamoto hii.

Kwenye mbuga za wanyama na hifadhi za Taifa, ujenzi wa minara ya mawasiliano unahitaji kibali cha tathimini ya mazingira kutoka Baraza la Mazingira la Taifa jambo linalofanya kazi ichukue muda mrefu kwa nia ya kulinda mazingira na viumbehai vilivyomo.

Maeneo mengine ni yenye changamoto za kijiografia kama vile milima mirefu na mabonde ambako minara iliyojengwa haitoshi kutawanya mawasiliano kwa wananchi. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuiongeza minara kufanikisha mawasiliano ya uhakika.

“Serikali inatoa ruzuku kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuzipatia fedha kampuni za simu kufikisha mawasiliano kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara hivyo kutokuwa na faida kiuwekezaji,” anasema Nditiye.

Ukiachana na changamoto za kitaaluma hasa zinazohusu miundombinu, watumiaji wa huduma za mawasiliano wamekuwa wakipotoka mara kadhaa na kusababisha kero, karaha, hasaha au aibu kwa watu binafsi, taasisi au kampuni.

Tayari Sheria ya kudhibiti makosa ya mtandaoni imeshatungwa na kinachofanywa sasa, bila kujali matumizi mabaya yanayofanywa, inaendelea kuweka miongozo itakayoboresha mawasiliano kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano.

Kuongeza uhakika wa huduma, Nditiye anasema: “Serikali inasimamia utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa usalama wa mitandao.”