Masogange afariki dunia

Muktasari:

Mwanasheria wake amedai mara ya mwisho waliwasiliana naye siku mbili zilizopita kwa ujumbe wa simu ya mkononi.

Dar es Salaam. Msanii anayepamba video za muziki (video queen), Agnes Gerald ‘Masogange’ amefariki dunia leo.

Taarifa hizo zimethibitishwa na mwanasheria wake, Reuben Simwanza, alipozungumza na Mwananchi leo Aprili 20.

Simwanza amesema taarifa za kifo chake amezipata kupitia dada yake, saa chache zilizopita.

Kwa maelezo ya Simwanza, dada wa Masogange, Emma Gerald, ndiye aliyetoa taarifa hizo baada tu ya kutoka kumuona alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Mwanasheria huyo ambaye amedai yeye si msemaji zaidi, kuhusu nini chanzo cha kifo chake, alidai mara ya mwisho waliwasiliana naye siku mbili zilizopita kwa ujumbe wa simu ya mkononi.

 “Unajua kuumwa kweli alikuwa anaumwa, kipindi cha kesi yake magonjwa ya hapa na pale ikiwamo presha, si unajua tena mambo ya kesi hayana mwenyewe, lakini baada ya kwisha tulikuwa tunataniana kwamba sasa nina imani utakuwa powa kwani kila kitu kipo sawa,”amesema Simwanza.

Hata hivyo amesema yupo njiani kuelekea hospitali kwa kuwa hakuweza kupata maelezo zaidi kutoka kwa dada yake huyo ambaye amemsikia akiwa analia tu.

Hivi karibuni, Masogange alihukumiwa kulipa faini ya Sh 1.5 milioni  na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukutwa na hatia ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin.

Alibainika kutumia dawa hizo kati ya Februari 7 na 14, 2017.